| Neno la Mfasiri
Kuandaliwa kwa Kitabu hiki ni jitihada ya kujaribu kutoa picha halisi na muelekeo sahihi unaofunzwa na Uislamu kinadharia juu ya maisha ya Peponi. Pepo ni umbile tukufu ambalo ni zawadi watakayotunukiwa watu na majini watakaofuzu mtihani wa maisha ya ulimwenguni kwa matendo yao mema kulingana na alivyoamrisha Muumba. Kitabu hiki kinatoa picha ya jumla na ya kweli juu ya umbile la Pepo na maisha ya Peponi ili kuwaongezea tamaa na hamu wale wote wanaofanya jitihada ya kumcha Mwenyezi Mungu. Hamu na tamaa ambazo kwa Tawfiiq ya Mwenyezi Mungu zitawapa hamasa ya kuzidisha na kudumisha matendo mema, yatakayowafanya wafanikiwe na wawe miongoni mwa wakazi wa umbile la Pepo lenye jiografia ya ajabu. Maudhui ya kitabu hiki yanamjenga msomaji aweze kukabiliana na changamoto za kuepuka makatazo na kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu kwa matarajio ya kufaulu na kuingia Peponi.
Dhana na picha ya kimawazo inayochorwa na kitabu hiki, ni nyenzo za kumsaidia msomaji kupata taswira na kuuchambua ukweli juu ya maisha haya. Inatarajiwa nyenzo hizo ziwe msukumo wa kufanya utafiti wa kina ili kupata usahihi juu ya dhana, itikadi na maelezo mengi yatolewayo juu ya maisha yajayo yenye uhai wa milele. Usaidizi wa nyenzo hizo, utamuwezesha msomaji kubaini hakika juu ya maisha ya Peponi na kuweza kuyasawiri kifikra akiwa na hakika nayo.
Kwa kuwa ufahamu juu ya maisha ya Peponi umezungukwa na hakika za kiimani, basi ulinganishi uliofanyika kitabuni humu unawianishwa na maisha halisi ya ulimwengu huu. Katika baadhi ya sura au sehemu, yametolewa maelezo linganishi ili kumuwezesha msomaji kupima na kutafakari ili kupata uoni huru unaotokana na hakika za kimsingi zenye hoja madhubuti. Kitabu hiki kimelenga kusaidia kumpa msomaji uhalisia wa kile ambacho pengine amekuwa akikisikia, kujifunza na kukiamini muda wote bila ya kuwa na walau tawira yake.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu aikubali jitihada hii, atusamehe upungufu wetu na atie Tawfiiq wasomaji wake waweze kuyafahamu vyema maudhui ya kitabu hiki na ili kwayo, waweze kuishi kulingana na atakavyo YEYE, wapate kufaulu na kuzawadiwa Pepo tukufu katika maisha yajayo ya Akhera baada ya haya ya Ulimwengu. |