| Dibaji
Kuandaliwa kwa Kitabu hiki kumelenga kumpa msomaji picha halisi juu ya maisha ya Jahannam. Jahannam inawakilisha tabaka za Moto wenye mwako mkubwa utakaobabua na kuunguza miili ya viumbe walioishi duniani kwa kukana na kukiuka maamrisho ya Muumba. Maisha ya Motoni ni adhabu watayokapewa watu na majini ambao matendo yao hapa duniani yalikuwa maovu ya ukafiri, shirki, udhalimu na ufisadi.
Kitabu hiki kinatoa picha ya jumla na ya kweli juu ya Jahannam ili kuwapa khofu na woga wale wote watendao maovu hapa duniani. Ukumbusho huu umekusudiwa, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, uwe msukumo wa kuyaeleka mema ili iwe tashiwishi kwa kiumbe ya kujiokoa kutumbukia Jahannam ambalo ni umbile lenye jiografia ya kutisha. Maudhui ya kitabu hiki yamelengwa kumjenga msomaji aweze kuepuka makatazo na kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu(SW).
Dhana na taswira inayojengwa na maudhui ya kitabu hiki, ni njia za kumsaidia msomaji kuweza kuuchambua ukweli juu ya maisha haya. Inatarajiwa taswira hiyo iwe kichocheo cha kufanya utafiti wa kina ili kupata usahihi juu ya dhana, itikadi na maelezo mengi yatolewayo juu ya adhabu ya moto.
Kwa kuwa ufahamu juu ya maisha ya Motoni umezungukwa na hakika za kiimani, basi maelezo yaliyotolewa kitabuni humu yanawianishwa na maisha halisi ya ulimwengu huu. Kitabu hiki kimelenga kusaidia kumpa msomaji uhalisia wa kile ambacho amekuwa akikisikia na pengine kudhani na kuitakidi kuwa ni ngano au simulizi za watu wa zamani zisizo na uhalisia!
Tunamuomba Mwenyezi Mungu aikubali jitihada hii, atusamehe upungufu wetu na atie Tawfiiq maudhui ya kitabu hiki yafahamike vyema ili sote tuweze kuishi kulingana na atakavyo Muumba tuweze kujiepusha na adhabu mbaya ya Motoni.
|