Nani Mwenyezi Mungu?

SHUSHA KITABU

Download (DOC)
Maoni

SURA ZA KITABU

< <
1 / total: 5
Nani Mwenyezi Mungu? - Harun Yahya
Nani Mwenyezi Mungu?
   
Muujiza katika Uumbaji wakeNeno la Mfasiri

Tangu zama za zama, watu wamekuwa wakiutafakari Ulimwengu na chanzo cha uhai na wametoa mawazo yao mbali mbali juu ya suala hili. Tunaweza kuyagawa mawazo hayo katika makundi mawili. Mosi, yale yanayofafanuwa Ulimwengu kwa mtazamo wa kukanusha uumbaji na pili yale yanayoona kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Aliyeumba maada na Ulimwengu kutokana na Ombwe Tupu na kuupangiya utaratibu. Viumbwa vyote hai na visivyo hai, vinavyoonekana na visivyoonekana, vilitokana na kazi ya Mwenyezi Mungu. Wanadamu, Majini, Wanyama, Mimeya, Magimba (galaksi), Nyota, Sayari, miyezi na vimondo vyote vimeumbwa na Mwenyezi Mungu. Usanii bora, mahesabu, urari, mizaniya, uwiyano na mpangiliyo unaoonekana katika Ulimwengu na kwa viumbwa hai ni vielezeo vya Imani hii.

Kwa wakanushaji, wao wanadai kuwa sayansi na mantiki viko upande wa itikadi isiyoamini Mungu. Wameshikilia kuwa Mwenyezi Mungu hayupo kwa sababu hatambulikani kwa milango yetu mitano ya fahamu. Wameiendeleza hoja hii kwa kudai kuwa Ulimwengu unatokana na maada na kwamba maada ndiyo kitu pekee kilichopo. Wanadai kuwa bahati nasibu ndiyo iliyosababisha Ulimwengu ujiunde wenyewe na uhai kutokea kwa kujianzisha wenyewe kidogo kidogo kutokana na vitu visivyo na uhai. Kwa maneno mengine, viumbwa vyote hai Ulimwenguni viliibuka tu kutokana na vyanzo vya asili na bahati nasibu kwa kanuni ya kila tukiyo na sababisho lake. Yakiwa ni matokeo ya ngano hiyo, dhanna ya kumkana Mungu huchukuliwa kama ndiyo “jambo la kawaida”, yaani jambo lisilohitaji jitihadi za kiakili kwani halihitaji uthibitisho. Ni muumini anayebebeshwa dhima hiyo, ambaye anahitajika kuthibitisha imani yake na hivyo ndiye anayejitahidi kujihami. Muumini anapotafuta jawabu ya maswali haya anakutana na nadhariya kem kem au hiyana za wanafalsafa ambazo ndizo zijengazo imani za watu wanaomkanusha Mwenyezi Mungu wakiwemo wanasayansi. Mtazamo wa falsafa ya ukanushaji unashikilia kuwa Ulimwengu na maumbile yake hayakuumbwa bali ni wa milele na unajiendesha pasi na haja ya kuwa na Muumba.

Ama kwa Waumini, wao ithibati yao ni kwamba Mungu Muumba ndiye Aliyeumba Ulimwengu kwa Kun -Fayakun, yaani kukitaka kitu kiwe na kikawa! Aidha utendaji kazi usiyo na dosari wa kila kitu ni kielezeo chao cha uwezo mkubwa kabisa wa kuumba Alionao Mwenyezi Mungu. Kokote na popote mtu ageukiapo, anakutana na ishara zinazobainisha wazi wazi kuwapo kwa Muumba. Kwa hakika hakuna uwezekano wowote wa Ulimwengu na vilivyomo kutokea kwa bahati nasibu.

Kwa min-ajiri hiyo, kitabu hiki kinachambua kwa kina maumbile ya angani, kuonesha maajabu yake ili kujibu maswali ambayo tangu zama za awali za maisha ya Mwanaadamu hapa Duniani, kila Mwanaadamu amevutwa nayo na kuyatafakari; kwamba ni namna gani Ulimwengu tunaoishi ulivyotokea, ni kwa jinsi gani mpangiliyo, uwiano na utaratibu madhubuti ulivyojitokeza na ukiendelea kudumu kama ulivyo ukidhibiti maumbile yote? Na ni namna gani Dunia tuishiyo ilivyowiana na viumbwa inavyovibeba pamoja na maumbile mengine yaliyo nje yake hivyo kuifanya Dunia kuwa makazi munasibu yenye kuwezesha maisha ya viumbwa vyenye uhai. Majibu maridhawa yapatikanayo ndani ya kitabu hiki yanaoana na hitimisho la Wanasayansi na Wanafalsafa wakweli kwamba ulinganifu huu na utaratibu madhubuti ni ushahidi toshelevu wa kuwapo kwa Muumba ambaye ndiye mtawala wa Ulimwengu na vyengine vyote ambaye akili ya Mwanaadamu ni muhali kuweza kumdiriki. Kwamba ni Muumba huyo, Mweledi, Hodari Aliyewezesha kuwepo hayo yote ambaye sifa zake za kiungu ni pamoja na kutokuwa na mwanzo wala mwisho kinyume na ilivyo kwa viumbwa.

Hiki ni kitabu cha Tawhiid ambacho makusudio yake siyo tu kuwanufaisha wanafunzi bali wote watakaochukua taabu kukisoma kwa mazingatio, ambao kwa Taufiiq ya Mwenyezi Mungu, wamedhamiria kujenga imani thaabiti juu ya Muumba wao. Kwa ajili hiyo, maudhui ya kitabu hiki yatakuwa na manufaa zaidi iwapo wasomaji watayasoma kifamilia au kivikundi ili kwa pamoja, waweze kutafakari na kujadili mada hii muhimu kwa maslaha ya maisha yao ya hapa Duniani na maisha ya baada ya kifo, akhera.

Tunataraji, kwa msaada wake Mwenyezi Mungu, ujumbe huu utawafikia walengwa kwa namna ile iliyokusudiwa na Waandishi. Matarajio hayo ni pamoja na kuona wasomaji wakibadili tabia na mienendo yao baada ya kukiri kuwa wao ni viumbwa vyenye kutegemea mwongozo na maelekezo ya Muumba katika maisha yao yote.

Abdiin Hussein Kifea

Dar es Salaam

Tanzania


    
1 / total 5
You can read Harun Yahya's book Nani Mwenyezi Mungu? online, share it on social networks such as Facebook and Twitter, download it to your computer, use it in your homework and theses, and publish, copy or reproduce it on your own web sites or blogs without paying any copyright fee, so long as you acknowledge this site as the reference.
About this site | Tengeneza kurasa yako ya nyumbani | Add to favorites | RSS Feed
Mambo yote yanaweza kuynakiliwa, kuchapwa na kusambazwa kwa kurejea katika kurasa hii
(c) All publication rights of the personal photos of Mr. Adnan Oktar that are present in our website and in all other Harun Yahya works belong to Global Publication Ltd. Co. They cannot be used or published without prior consent even if used partially.
© 1994 Harun Yahya.www.harunyahya.com
page_top