< <
3 / total: 9
Pepo: Makazi ya kudumu ya WachaMungu - Harun Yahya
Pepo:
Makazi ya kudumu ya WachaMungu
   

 


Sura ya Pili
Kutamani Maisha ya Raha

Ni kipi hasa Mwanaadamu anachokistaajabu, anachokihusudu, anachokitaka, anachokihitaji, anachokitamani au kukipenda zaidi katika maisha? Nyumba nzuri, jumba kubwa la fahari, mavazi ya gharama kubwa, mapesa, utajiri au mali na jaha?Ni  hisia zipi ambazo mtu huzipata anaposimuliwa habari inayohusu mahali fulani ambako kila kizuri atakacho na akipendacho ataweza kukipata tena kwa kudumu nacho milele?  Bila shaka anafurahi sana na atapenda kufika mahali hapo tena ikiwezekana sasa hivi.  Yumkini hakuna mtu ambaye aweza kufanya ajizi au kukataa kwenda kuishi mahali pazuri pa namna hiyo.

Hebu sasa fikiria jambo hili: Je kuna mtu yeyote ambaye amewahi kusimulia habari kuhusu pale mahali penye neema nyingi au palipo jaa neema zisizo na hesabu. Pale ambapo kila kizuri, kila kitamu, kila kinono, kila kipendacho roho kitasogezwa miguuni mwake?

Bila shaka si mara moja wala mbili na si mtu mmoja wala si wawili, lazima watakuwa wamewasimulia  wengine kuhusu kuwepo kwa maisha fulani, nayo ni maisha ya peponi ambako kila anachokihitajia mtu kimekwisha andaliwa kwa ajili yake.

Kila mtu ana khabari kwamba baada ya mauti kuna maisha haya ya milele ya peponi.  Wale watakaostahiki kuingia humo watakuta kila kitu wanachokitamani.  Watapata malipo yao ambayo ni ya kuishi mahala pema penye neema na starehe za kudumu.   Waumini watakaofuzu majaribio au watakaofaulu mtihani wa maisha haya ya dunia, hao Mwenyezi Mungu amewaahidi makazi mapya na ya kipekee. Muda mfupi wa saa, moja, siku moja au miaka mia anayoishi mtu hapa duniani kwa upande wake, ni fursa ndogo tu ya kutafutia makazi hayo mazuri.

Sasa nini basi kinachowakosesha watu hamasa ya khabari hii njema ya pepo? Ni nini kinachowazuia wasitamani Pepo, nini kinachowatia uzito kufanya jitihada za kuipata?  Kwa nini watu, licha ya kujua kuwa watapata neema za milele kama malipo ya Mola wao lakini bado hawajiandai kwa ajili ya neema hizo?

Kwa hakika sababu kubwa kabisa ni kwamba baadhi ya watu hawana yakini kuwa pepo ipo:  Wengine hawaamini kabisa, wengine wameifanya ni kitu cha kufikirika na wengine wamekuwa wakiihusisha na mambo ya kiroho kwa ile tafsiri potofu ya roho.  Zinaweza kuwepo sababu nyingine za watu kutoamini au kuitilia mashaka Pepo. Jambo la msingi ambalo sote hatuna budi kulitilia maanani ni kuwa mashaka haya wakati mwingine yanatokana na uhaba, uchache au ukosefu wetu wa elimu na pengine mtindo au njia zinazotumika katika kuelezea uyakini na uhalisia wa maisha yajayo.

Mazingira ya Peponi

Kwa hakika si dhambi Waislamu kuishi maisha ya starehe na ya kitajiri hapa duniani muda wa kuwa wanazingatia mipaka ya Allah na wanamcha ipasavyo, kwani rasilimali za dunia(nguo nzuri, chakula kinono, majumba mazuri) zimeumbwa kwa ajili ya waja wa Mwenyezi Mungu kama tusomavyo katika Qur'an:

Sema: Ni nani aliyeharamisha mapambo ya Mwenyezi Mungu ambayo amewatolea waja wake. Na (nani aliyeharamisha) vitu vizuri katika vyakula? Sema vitu hivyo vimewahalalikia Waislamu(hapa) katika maisha ya dunia (na) vitakuwa vyao peke yao siku ya kiama. Namna hii tunazieleza aya kwa watu wajuao(7:32).

Maisha ya Muumini si yale ya kuvaa ovyo ovyo na wala si kuishi katika uchafu wa hali zote. Haitarajiwi kujikunyata bali umaridadi wa mavazi, makazi mazuri, elimu nzuri yenye manufaa, matibabu, kula na kunywa vizuri. Qur'an inatoa mfano wa Nabii Suleiman(a.s) ambaye Allah(s.w) alimpa utajiri mkubwa. Inaelezwa mali, kasri la kitajiri na kazi zake za sanaa kama ifuatavyo:

"Na kwa Suleiman(tukatiisha)upepo(uliokwenda safari yake ya asubuhi (mwendo wa ) mwezi mmoja na safari yake ya jioni) wa mwezi mmoja. Na tukamnyunyizia Chem Chem. Ya shaba. Na katika majini(kulikuwa na) waliofanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake. Na kila anayejitenga na amri yetu miongoni mwao Tunamuonjesha adhabu ya moto uwakao. Walikuwa wakimfanyia apendalo kama ngome,  masanamu na mabunguu makubwa kama mahodhi na masufuria makubwa sana yasiyoondolewa mahali pake. Tukawaambia: Fanyeni amali nzuri enyi watu wa Daud kwa kushukuru(neema mlizopewa). Na ni wachache wanaoshukuru katika waja wangu.(34:12-13).

Katika sura nyingine, Qur'an inasema hivi:

"Akaambiwa liingie jumba(langu)"(Malkia) alipoliona alidhani ni eneo la maji, akapandisha nguo mpaka katika miundi yake(ili ayavuke hayo maji(Suleiman) akasema hakika hili ni behewa lililosakafiwa kwa vioo. Akasema(yule Malkia) Mola wangu, mimi nimedhulumu nafsi yangu na sasa najisalimisha pamoja na Suleiman kwa Mola wa walimwengu(27:44).

Mafunzo muhimu yaliyopo hapa ni kuwa utajiri, umaridadi, elimu na neema alizopewa Suleiman zilimvuta Mwanamama Malkia Bilqis katika kumpenda Suleiman na kuikubali dini ya Mwenyezi Mungu hivyo ikamfanya ajilaumu nafsi yake kwa kuishi kifisadi akidhani kuamini Mwenyezi Mungu na kuishi kama atakavyo kungelishusha hadhi yake na kumfanya aishi maisha ya chini, dhalili. Lingine ni kwamba Suleiman alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mali hizo kubwa kubwa kwani yeye alijuwa kuwa zote hizo zilikuwa neema za mola wetu. Alisema:

"Navipenda vitu vizuri kwa ajili ya kumkumbuka Mola wangu"(38:32)

Hapa Qur'an inatubainishia mtazamo wa Suleiman juu ya neema. Mfano wa Suleiman unatuhakikishia kuwa kuchuma na kumiliki mali ni mambo yaliyohalalishwa maadamu tu mali hizo ziwe nyenzo za kumuabudia Allah. Kwa hiyo waumini wanatakiwa kutafuta na kutumia mali kama atakavyo Allah. Mali ni neema za Mwenyezi Mungu(s.w) hivyo itakuwa busara kwa wale walionazo kuzitumia vile anavyoamrisha mwenye neema zake(Allah). Kama mali hazitazamwi kama neema za Allah basi hapo ndipo penye ufisadi. Qur'an inatoa mifano mingi ya jinsi wale waliokengeuka wanavyoitazama mali. Mmoja wa watu hao ni Qarun. Huyu alikuwa tajiri aliyekufuru:

"Hakika nimepewa haya kwa sababu ya elimu yangu(28:78).

Mtazamo wa namna hii juu ya mali hauwezi kuwakurubisha watu kwa Allah badala yake unawatoa katika njia yake na kuwaondolea imani: (Qur'an) inasema:

"Bila shaka Mwanaadamu anamkanusha Mola wake. Naye anayajua haya ana mapenzi makubwa kabisa ya kupenda mali(100:6-8).

Kwa hiyo, Waislamu hawanabudi kuutazama utajiri kwa maelekezo ya Qur'an na wachume mali kwa lengo la kutafuta radhi za Allah na kuutumikia Uislamu. Lazima wazitamani neema zote za Allah kwa sababu neema hizo zimeumbwa kwa ajili ya wale wenye imani na Ikhilasi ambao hufanya kila jitihada kumridhisha na kumtumikia Allah.

Daima tuwe wenye kushukuru kwa neema hizi na tuige mfano wa Suleyman(a.s).

"Na tukampa Daud(mtoto anayeitwa) Suleiman, aliyekuwa mtu mwema na alikuwa mnyenyekevu mno.(kumbukeni) alipopelekewa jioni farasi walio kimya wasimamapo wepesi wakimbiapo. Basi akasema "navipenda vitu hivi vizuri kwa kumkumbuka Mola wangu(38:30-32).

Wale wanaoishi kwa Muongozo wa Qur'an, wakiwa na mtazamo uliyoelezwa hapo juu ndio watakaostahiki kuingia peponi. Wameishi vizuri duniani na wataishi vizuri zaidi akhera. Zaidi ya raha na sterehe zake ziburudishazo nyoyo na macho, maisha ya Akhera yanaongezwa na sifa ya umilele.

Watu wenye mtazamo wa Suleiman juu ya starehe za dunia ndio watakaofaidi starehe za Akhera. Kwa hiyo basi tunapoyatazama maisha ya Akhera kwa wale watakaofaulu ndiyo yenye starehe za kila namna vivyo hivyo lazima tuwe na mtazamo huwo juu ya maisha  ya Ulimwengu ambayo ni sehemu ya maandalizi ya maisha ya Akhera. Badala ya kuchukulia utajiri, starehe na burudani zenye kuzingatia mipaka ya Allah kama ni ufisadi waumni hawanabudi kujua kuwa kila neema ni takrima ya Allah waithamini, waifaidi kwa namna bora na washukuru kwayo. Neno takrima kwa asili na usuli wake, lina sifa tu ya wema na ukarimu na halijakuwa na ila ya rushwa wala shere ya mtu kumnunua mwingine kama wafanyavyo wafadhili au wahisani wa kisiasa.

 
   
    
3 / total 9
You can read Harun Yahya's book Pepo: Maskani Ya Waumini online, share it on social networks such as Facebook and Twitter, download it to your computer, use it in your homework and theses, and publish, copy or reproduce it on your own web sites or blogs without paying any copyright fee, so long as you acknowledge this site as the reference.
About this site | Tengeneza kurasa yako ya nyumbani | Add to favorites | RSS Feed
Mambo yote yanaweza kuynakiliwa, kuchapwa na kusambazwa kwa kurejea katika kurasa hii
(c) All publication rights of the personal photos of Mr. Adnan Oktar that are present in our website and in all other Harun Yahya works belong to Global Publication Ltd. Co. They cannot be used or published without prior consent even if used partially.
© 1994 Harun Yahya.www.harunyahya.com
page_top