< <
4 / total: 9
Pepo: Makazi ya kudumu ya WachaMungu - Harun Yahya
Pepo:
Makazi ya kudumu ya WachaMungu
   

 


Sura ya Tatu
Ramani ya Maisha ya Peponi

Kama lilivyo umbile la ulimwengu lenye maumbile kadhaa zikiwemo sayari, nyota, miezi na mengineyo, Pepo na Moto ni sehemu ya maumbile halisi makubwa kabisa ya umbile halisi la Akhera. Mwenyezi Mungu ameujaalia uhai wa mwanaadamu kuwa wa namna mbili. Uhai wa muda mfupi yaani wa ulimwengu huu wa maisha ya mtihani, na uhai wa dumu daima huko Akhera wa maisha halisi ya raha za  kufaulu Peponi au adha na taabu za kufeli, Motoni.

Katika Qur'an Mwenyezi Mungu anayaelezea maisha halisi mazuri yenye starehe timilifu na yenye kudumu milele.  Yule mtu asiyejuwa kima cha starehe hii au asiyejuwa namna Qur'an ilivyoelezea starehe hii yumkini itamwia vigumu kupata picha ya Pepo na aina ya maisha yaliyopo huko. Mafundisho haya yanawasimulia watu habari za Pepo ambayo Mwenyezi Mungu amewazawadia.  Yanataja neema kubwa kubwa zilizomo humo na yanaelezea starehe zake kwa kila mtu.  Yanawataarifu kuwa Pepo ni aina mojawapo kati ya aina mbili za maisha yaliyoandaliwa kwa ajili yao katika ulimwengu ujao na kwamba kila kilicho kizuri kila kistareheshacho, kila kiburudishacho kitakuwa mali yao kwa kiasi ambacho kipo nje ya uwezo wa kufikiri tulionao.

Mafunzo haya yanabainisha kuwa Peponi ni mahali ambapo neema zimeumbwa kwa ukamilifu na ambamo watu wataneemeshwa kila kitu ambacho roho na nyoyo zao zitakitamani na  ambamo watu watakidhiwa kila haja na wataondoshewa kila shaka na huzuni, kila dukuduku na sononeko.  Kila aina ya starehe na kila neema ipo peponi na itatolewa kwa ukamilifu ambao hapo kabla hakuna aliyeuona wala kuujua Mwenyezi Mungu ameziandaa neema hizo kama zawadi ambazo zitatolewa kwa wale tu anaowaridhia.   Mafunzo haya yanaelezea kila kitu na kila jambo la Peponi. Kwa mujibu wa Qur'an, hivyo usomapo mistari hii jaribu kujenga picha ya mahala hapo pema, kumbuka kwamba Qur'an ni ukweli mtupu, kwa kuzingatia hilo tutafakari ubora  wa makazi hayo halisi yanayotusubiri na tufanye kila jitihada ili ustahili kuyapata.   Elewa kwamba Mwenyezi Mungu anakupa vyote hivi kwa rehma zake na vitakuwa vyetu moja kwa moja. Sasa iwapo bado tunashindwa kuhiyari kupata neema hii ya starehe za milele basi tukumbuke kuwa chaguo lililobaki ni jahanam ambamo mmejaa mateso ambayo daima itakuwa hofu, huzuni, majonzi, masikitiko na majuto.

Neema na Israfu

Katika jamii za leo watu wengi wana mawazo na hisia lizofichikana vichwani mwao, kwa vile mawazo na hisia hizo ndizo zinazosababisha wabuni dhana, badala ya kuziita dhana za sayansi au tekinolojia kana kwamba ni elimu ngeni isiyopata kuwako kabla.   Katika mafundisho ya Qur'an tunaelezwa kuwa Pepo kama mahala bora kabisa penye starehe, kwamba maisha ya humu ni ya raha tupu na utulivu. Watu wengi hivi leo, maisha kama hayo kwa hapa duniani huonekana si ya kiislamu. Haya ni matokeo ya kuyatenganisha maisha hayo na Mwenyezi  Mungu katika mafundisho yake ya "kiroho".   Hivyo kwa sababu hii ya uelewa huu wa ndivyo sivyo kuna wakati katika jamii watu wengi hudhani kuwa maisha ya starehe, na ya juu na vyote vinavyohusiana na maisha hayo "si vya kiisalmu". Vitu kama nguo za bei kubwa, chakula bora, burudani, dhifa, majumba mazuri, mapambo na kazi nzuri za sanaa huonekana kama ni vitu vya kijahili na huviondoa katika maisha ya kiislamu. Ni vizuri na ni halali kuishi kwa viwango vya juu lakini bila ya kupoteza daraja za misingi, nguzo, faradhi na sunna za dini yetu.

Mara nyingi huyaita maisha yaliyojaa vitu hivi kuwa ni ya kifisadi na kuwashutumu wale wanaoishi maisha hayo huku wakizitaja jamii zinazoishi maisha hayo kama ni jamii zilizokosa murua.   Neno "safahati" linatokana na neno safihi ambalo hufasiriwa kama ukosefu wa murua, ulevi wa maisha, utovu wa akili unaotokana na kuishi maisha ya utajiri na starehe na ambavyo sivyo.  Maisha ya peponi ambayo Mwenyezi Mungu amewapendelea zaidi waja wake ina kila aina ya raha, starehe na umakinifu, yote haya ni maisha yanayokwenda sanjari na mafundisho ya dini ya Allah.

Watu hawawi mafisadi kwa sababu ya nguo nzuri, majumba mazuri, mazingira yenye mapambo na utajiri wa mali. Kama watu wana maadili ya Qur'an na imani nzito wanaweza kuishi wakiwa matajiri wakubwa kabisa bila yakuwa mafisadi, kwa vile wao wanakitazama kila kitu kwa mafundisho ya kiislamu, wao huiona starehe yote inayowazunguuka kama neema, upendeleo na mitihani.     Kwa maneno mengine wanatambua kuwa vitu hivi ni hidaya kutoka kwa Allah(s.w), kwahiyo wao humshukuru Mwenyezi Mungu kwa utajiri, starehe, mali na hadhi aliyowapa na tangu hapo neema zote zimeumbwa kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Iwapo tutatumia njia ya tafakuri katika jamii zetu za leo, basi tutasema tu kuwa wale wanaoishi maisha ya ufisadi wamekengeuka kwasababu wao hawaoni kuwa jitihada zao pia ni neema kutoka kwa Allah(s.w). Kama wangelizitazama neema hizi kama ni neema basi mtazamo huo ungewapelekea kumshukuru Mwenyezi Mungu na kisha kuzitumia neema hizo  kama Allah alivyopanga au alivyokusudia, wakiepuka israfu na wakizitumia kwa utaratibu anouridhia.   Kwahiyo basi utajiri waweza kuainishwa kwa namna mbili baadhi ya matajiri ni waumini wanaozihesabu mali zao zote kama neema kutoka kwa Allah wakati wengine hukengeuka kwa kudhani kuwa zile mali zote walizonazo ni za kwao, wakimsahau Mwenyezi Mungu na hivyo kutumbukia kwenye ufisadi. Tukumbuke, kigezo ambacho Allah amekiweka kutupima waja wake imani ni mali, utajiri na umasikini.

Hali ya Wanaomcha Mwenyezi Mungu

Qur'an inasema kuwa waumini ni wale wanaosema:

"Mola wetu ni Mwenyezi Mungu", kisha wakenda mwendo mzuri, hao huwateremkia malaika, Msiogope wala msihuzunike, na furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa"(41:30).

Pia Qur'an inasema kuwa waumini wanajua kuwa:

"Hatuikalifishi nafsi ya mja ila kwa kiasi cha uweza wake, hao ndio watu wa Peponi. Wao watakaa humo milele(7:42).

Waumini huamini kudra kwamba Allah hufanya na kutimiza kila jambo. Hivyo huliridhia kila jambo liwatokealo kuwa linatoka kwa Allah kama isemavyo aya hii:

"Sema; halitusibu ila alilotuandikia Mwenyezi Mungu"(9:51).

Kwa vile wanaotaka kumridhisha Allah, husema:

"Mwenyezi Mungu anatutosha. Naye ni mlinzi bora kabisa. Basi wakarudi na neema za MwenyeziMungu na fadhila(zake), hakuna ubaya uliowagusa na wakafuata yanayomridhisha Mwenyezi Mungu(3:173-174).

Lakini kwa vile hapa duniani ni mahali pa mtihani, Waumini watakabiliwa na matatizo kama njaa, ugonjwa, kukosa usingizi, ajali au hasara ya mali. Wanaweza hata kupata mitihani migumu zaidi kama umasikini na hali ngumu kama isemavyo aya hii:

"Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, na hali ya kuwa hamjajiwa na mfano wa (yale yaliyowafika) wale waliopita kabla yenu? Yaliwapata mashaka na madhara na wakatetemeshwa sana hata Mitume na waliaoamini pamoja nao wakasema "Nusura ya Mwenyezi Mungu itafika lini? Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu iko karibu(2:214).

Mitihani hiyo haikuwayumbisha Mitume na waumini kutokana na ile imani yao thaabiti juu ya Mola wao na kutokana na ile dhamiri yao ya kuitekeleza Qur'an. Mwishoni mwa aya hiyo, Allah (s.w) anawaahidi Waumini kuwa msaada wake upo jirani nao. Katika aya nyingine Allah (s.w) anasema:

"Na Mwenyezi Mungu atawaokoa wale wamchao kwa ajili ya kufuzu kwao. Hautawagusa ubaya wala hawatahuzunika(39:61).

Hivyo, Waumini wote wanajua kuwa matatizo, shida na taabu zote zimeumbwa kwa minajili ya kuwatahini imani zao na kama ni wenye subira na wanyenyekevu, matatizo hayo yatawapa fursa nzuri ya kukomaa kiimani. Isitoshe mitihani hiyo ndiyo itakayowapatia malipo ya milele katika maisha ya Akhera. Kwa sababu hiyo, watayakabili matatizo hayo hadi kupata tena hali bora, furaha na raha. Katu matatizo hayo hayatoteteresha msimamo wao wala kuathiri hisia na dhamiri zao. Kinachotakiwa ni ibada ya subira.

Badala yake hamasa yao itazidi kuongezeka kwani wanajua kuwa watapata ujira wao kwa ile subira na ule unyenyekevu wao mbele ya Mola wao. Kwa upande wa makafiri mambo yako kinyume na hivyo. Wale wanaokanusha Qur'an hutaabika na adha za rohoni(hupata mateso ya moyo) sambamba na adha za kimwili ambazo huzipata katika maisha ya Dunia hii.

Khofu, huzuni, kukata tamaa, roho juu, wasi wasi, mfadhaiko, kuhamanika, kusononeka, woga na hisia mbaya nyinginezo watazongwa nazo hapa hapa na ambazo ndizo mwanzo wa taabu za motoni.

Mwenyezi Mungu anawaelezea watu hawa katika aya ifuatayo:

"Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu kamuongoza humfungulia kifua chake Uislamu na yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumuhukumu kupotea, humfanya kifua chake kizito, kinaona taabu kubwa(kufuata Uislamu); kama kwamba anapanda mbinguni, Namna hivi Mwenyezi Mungu anajaalia uchafu juu ya wale wasioamini(6:125).

Lugha ina mambo. Vipofu wa baadhi ya nchi hujiita wasioona. Upofu si tusi wala si ila. Ni majaaliwa kama urefu, ufupi, uwete, uziwi nakdhalika. Neno Kafiri nalo si tusi. Ni mtu aliyekufuru. Aliyemkana Allah (s.w). Ama yule ambaye Mwenyezi Mungu kamwongoza ni yule aliyejitanguliza kumcha na kumnyenyekea muumba wake. Akaomba aongozwe Naye. Kila aombaye hujiombea nafsi yake. Mwenyezi Mungu hapendelei, habagui.

Mwenyezi Mungu hapa Anabainisha kuwa yeye hupenda kuwasamehe madhambi na makosa yao wale wanaomuelekea kwa unyenyekevu na taadhima na kwamba waja wanaoamini na kutubia, yeye atawapa neema nzuri nzuri katika maisha haya ya dunia na watapata radhi zake kama isemavyo Qur'an:

"Na ili muombe msamaha kwa Mola wenu kisha mtubie(mrejee) kwake. Atakustarehesheni kwa starehe nzuri kwa muda maalum. Na Akhera atampa fadhila yake kila mwenye fadhila. Na kama mtakengeuka basi nakukhofieni adhabu ya hiyo siku kubwa(11:3).

Kwa maneno mengine, kuomba msamaha kwa Allah (s.w) na kumuelekea Yeye katika kuomba toba ni miongoni mwa mambo yaliyoamrishwa kwa Waislamu wote. Mambo haya yanaonesha jinsi waumini wanavyojitambua kuwa wao hawana uwezo wowote bali ni viumbe dhaifu tu mbele ya Allah (s.w). Wanatambuwa upungufu na kasoro walizonazo kama viumbe na hivyo wao sio maasumu. Hivyo wanaomba rehema za Allah (s.w). Kama alivyosema Mola wetu, Yeye huwalipa waumini kwa maadili yao mema na kuwapa maisha mema hadi kufa na baada ya kufa kwao.

Katika aya hii Mwenyezi Mungu Anayelezea hivi maisha ya Waumini katika Dunia hii:

"Na wanapoambiwa wale wanaomcha Mwenyezi  Mungu: Ni nini Aliyoteremsha Mola wenu? Husema (Ametuteremshia kheri( kutuambia kuwa) wale waliofanya wema katika dunia hii watapata wema, hakika nyumba ya Akhera ni nzuri kabisa na ni bora kabisa, hiyo ni nyumba ya WachaMungu.(16:30).

Pale starehe zote zinapolinganishwa na zile za Akhera,za Dunia hii,  huonekana upuuzi mtupu. Kwa hiyo kama ni kuchagua,  basi ya kuchagua ni maisha ya Akhera. Mwenyezi Mungu Huwazidishia neema wale waumini ambao tayari wamezielekeza nyoyo zao katika maisha yajayo.

Katika swala zao, Waumini hao huomba maisha mema ya Akhera na pia humuomba Allah (s.w) maisha mema ya hapa Duniani. Mifano ya maombi hayo inatolewa katika aya zifuatazo:

"Mola wetu! Tupe mema duniani na tupe mema Akhera na utulinde na adhabu ya moto(2:201).

Waja wa Allah (s.w) wanaomuamini kwa Ikhlaswi ndio wanaotajwa kuwa Makhalifa wa dunia hii.

"Mwenyezi Mungu Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri kuwa atawafanya Makhalifa katika ardhi kama Alivyowafanya Makhalifa wale waliokuwako kabla yao, na kwa yakini Atawasimamishia dini yao Aliyowapendelea, na Atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu hawanishirikishi na chochote. Na watakaokufuru baada ya hayo; basi hao ndio wavunjao amri zetu(24:55).

 
   
    
4 / total 9
You can read Harun Yahya's book Pepo: Maskani Ya Waumini online, share it on social networks such as Facebook and Twitter, download it to your computer, use it in your homework and theses, and publish, copy or reproduce it on your own web sites or blogs without paying any copyright fee, so long as you acknowledge this site as the reference.
About this site | Tengeneza kurasa yako ya nyumbani | Add to favorites | RSS Feed
Mambo yote yanaweza kuynakiliwa, kuchapwa na kusambazwa kwa kurejea katika kurasa hii
(c) All publication rights of the personal photos of Mr. Adnan Oktar that are present in our website and in all other Harun Yahya works belong to Global Publication Ltd. Co. They cannot be used or published without prior consent even if used partially.
© 1994 Harun Yahya.www.harunyahya.com
page_top