< <
5 / total: 9
Pepo: Makazi ya kudumu ya WachaMungu - Harun Yahya
Pepo:
Makazi ya kudumu ya WachaMungu
   

 


Sura ya Nne
Habari Njema Kwa Wamchao Mwenyezi Mungu

Katika  sura ya kwanza tulielezea kuwa waumini wenye ikhlasi wanaojitupa kwa Allah (s.w) watafaidi neema zake katika Dunia hii kabla ya kuingia peponi.  Moja ya neema hizo muhimu ni miadi ya habari njema ya Pepo.  Aya kadhaa zinaizungumzia ahadi hii ya Allah (S.W);

"Wao wana mema katika maisha ya duniani na katika Akhera.  Hakuna mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu, huku ndiko kufuzu kukubwa" (10:64).

Nyoyo za waumini zinahamasika kwa habari hii njema kwamba amali zao zitapata malipo mbele ya  Allah na kwamba neema wanazozisubiri zipo jirani tu na zimejaa uhondo juu ya uhondo.

Qur'an pia inasema kuwa waumini watapata habari njema kutoka kwa Malaika. Wale waja wanaomuamini Allah kikwelikweli pasipo kumshirikisha na chochote na ambao wanatii  amri na mawaidha ya Qur'an na ambao wanaishi maisha yao kwa kufuata mafundisho yake, wao hufurahia kwa matumaini habari hii njema.

Kwa hakika habari hii ni furaha isiyoelezeka kwa waumini wote wanaotumai kuingia peponi kama tunavyosoma katika Qur'an:

"Wale wanaosema: Mola wetu ni Allah na kisha wakashika njia. Hao Malaika huwashukia na kuwaambia, msikhofu wala msihuzunike bali pokeeni habari njema za Pepo mliyoahidiwa".(Fussilat,30-32)

Allah (S.W) Aliwapa Manabii kazi ya kutangaza habari hii njema. Mwenyezi Mungu Anamuamrisha Mtume (S.A.W) kutangaza kuwa, waumini watapata ujira mkubwa kutoka kwake (Ahzab.47).

Katika Surati Yasin, aya ya 11, inabainishwa kuwa wale waliotii Qur'an na kumuogopa Mwingi wa Rehma watapata msamaha na ujira mkubwa kutoka kwake. Aya ya 17 ya surat Az Zumar inasema kuwa wale wanaoepukana na ibada ya miungu bandia na kumuelekea Allah (S.W) wapashwe habari njema.  Na katika surat Yunus aya ya 2, Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake,  awape habari njema wale wanaoamini kwamba wanayo malipo makubwa mbele yake. Tunapozitazama sifa za wale walioelekezwa katika aya hizo, tunaona kuwa hao ni wale waumini wa kweli walio karibu mno na Mola wao, wanaotambua nafasi zao kama binaadamu na wanaotii maamrisho ya Qur'an na ya Mtume (S.A.W) na wanaomuogopa Allah (S.W).

Ahadi ya Allah

Wale watakaosimama mbele ya Mwenyezi Mungu hali ya kuwa ni waumini, Allah Anawapa ahadi ya Pepo, humo watakaa milele.  Na hapana hata chembe ya shaka kuwa ahadi hii itatimizwa, na wale waumini wenye yakini,katu hawana shaka na ukweli huu. Isitoshe ikiwa wao wamezisalimisha nafsi zao Kwake, wanatumai kuwa madhambi yao yatasamehewa na wataruhusiwa kuingia Peponi.  Aya ifuatayo inabainisha hili;

"Isipokuwa wakitubu na kudumu kuamini na kufanya yaliyo mema.  Hao wataingia peponi wala hawatadhulumiwa chochote.  Pepo za milele ambazo (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa Rehema amewaahidi waja wake katika siri (yake). Bila shaka ahadi yake ni yenye kutimizwa (19:60-61).

Ipi? Uwapi  Ukweli kuwa Allah Amewaahidi waumini Pepo, unawapa furaha na kuwatia hamasa isiyosemeka.  Wao wanajua kuwa Allah Ameweka Pepo kwa ajili ya waja wake waliomuamini na kwamba amewafanya wao kama warithi wa Pepo hiyo. Hapa ipo aya nyingine inayoelezea ahadi hiyo;  Je mtu yule tuliyemuahidi ahadi nzuri tena atakapoipata atakuwa sawa na yule tuliyemnufaisha kwa maisha ya duniani tu, kisha siku ya kiama awe miongoni mwa watakaohudhurishwa Motoni? (28:61). Iwapo Allah amewaahidi Pepo waja wowote wale wenye kumcha, basi hao watapata neema za milele kwa rehema zake.  Na pale waumini watakapoingia Peponi, watatoa shukurani zao kwa kusema hivi;

"Nao watasema Alhamdulillah (sifa njema na shukurani zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye Ametutimizia ahadi yake na Ameturithisha ardhi(ya huku peponi), Tunakaa katika mabustani haya popote tupendapo "Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao (mema), (39;74).

Waumini ambao wamepewa habari njema wakati wa maisha ya Dunia ambao Allah (S.W) Amewaahidi Pepo ya maisha yao haya ya dunia watapata kile walichotumai kukipata. Hatimaye wakati huo uliosubiriwa kwa muda mrefu utafika, wataingia pale mahala pema  palioje na mafikio bora kuliko mafikio yoyote.  Katika maisha yao yote walikuwa wakiomba kupata na walijitahidi kwa kila hali ili wastahiki kuingia. Ni pahala penye kila kitu, palipoandaliwa kwa ajili ya waumini na milango yake iko wazi kwa ajili yao. Aya ifuatayo inatoa picha ya jinsi watakavyoingia peponi.  Mabustani ya milele wataingia wao (pamoja) na waliofanya mema miongoni mwa wazee wao na wake zao na kizazi chao. Na Malaika watakapoingia katika kila mlango wanawasalimu,

"Salamun Alaykum", iwe amani juu yenu, kwa sababu mlisubiri. Basi ni mema yaliyoje matokeo ya nyumba ya Akhera kwa wanaomcha Mungu (13:23-24).

Watakaribishwa Peponi kwa salamu za amani na heshima, hao ndio watakaolipwa ghorofa (za peponi) kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo hishima na amani (25:75).

"Na hakika wanaomcha Mwenyezi Mungu watakuwa katika mabustani na chem chem.,yaingieni salama usalimini"(15:45-46).

Sasa kimebaki kitu kimoja nacho ni kuziona starehe za hayo makazi ya milele waliyoandaliwa waumini na kutunukiwa kila aina ya neema. Allah (S.W) amezijaza imani nyoyo za waumini na kuzitia nguvu kwa roho itokayo kwake na atawaingiza katika mabustani yenye mito itiririkayo chini yake, wakae humo milele. Mwenyezi Mungu amewaridhia, hilo ndilo kundi la Mwenyezi Mungu na kwa hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu Amethibitisha kikweli kikweli nyoyoni mwao imani na Akawatia nguvu kwa roho zitokazo Kwake na atawaingiza katika mabustani yapitayo mito mbele yao humo watakaa daima, Mwenyezi Mungu amekuwa radhi nao, na wao wamekuwa radhi Naye.

"Hao ndio kundi la Mwenyezi Mungu.  Sikilizeni hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo linaloshinda (linalofaulu)". (58;22).

Kifo cha Muumini ni chepesi, hesabu nyepesi

Si Waumini wala makafiri wanaoweza kujuwa lini na wapi watakapofia. Ukweli huu unafafanuliwa na Qur'an;

Kwa hakika ujuzi wa kiama uko kwa Mwenyezi Mungu tu; Naye huteremsha mvua (wakati autakao) na Anayajua yaliyopo matumboni (hakuna anayejua isipokuwa Yeye) na nafsi yeyote haijui ni nini itachuma kesho, wala nafsi haijui itafia ardhi gani. Bila shaka Mwenyezi Mungu Ndiye Mjuzi, Ndiye mwenye khabari (ya mambo yote) (31:34).

Pamoja na hayo, Qur'an inatuarifu kuwa jinsi mauti yatakavyowajia waumini, namna roho zao zitakavyotolewa na nini kitakachotokea kwao wakati wa sakaratimauti. Tunavyofahamishwa hapa ni kuwa waumini huyaonja mauti kwa kutolewa roho kwa ulatifu. Pale waumini wanapokufa roho zao huchukuliwa kutoka Duniani na kupelekwa makazi mengine. Mwenyezi Mungu Anaielezea safari hii nyepesi katika Surati An-Nazi'ati, aya ya 2 ambapo Anawataja  wale Malaika watoao roho kwa upole. Aya nyingine inatuambia kuhusu mazungumzo ya Malaika pale wanapokuja kuchukua roho ya Muumini.

Wale ambao Malaika huwafikisha katika hali njema wakasema "Amani itakuwa juu yenu, ingieni peponi kwa sababu ya yale mema mliyokuwa mkiyatenda (16:32).

Aya ifuatayo inaeleza kifo cha Muumini: hautawahuzunisha huo mtaharuki mkubwa, na Malaika watawapokea (na kuwaambia) "Hii ndiyo ile siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa (21:103).

Ni dhahiri kuwa, Waumini ambao wameishi maisha mema katika Dunia hii watakuwa na kifo kizuri na chepesi na maisha yao ya ulimwengu ujao, huanza pale pale wanapofikiwa na Malaika. Tokea hapo na kuendelea, uhusiano wao na Dunia utasita (utakoma) na watapelekwa mahala walipopangiwa ambapo kutoka huko watakuja mbele ya Mwenyezi Mungu. Baada ya roho za Waumini kuchukuliwa kwa upole na Malaika sasa inakuja awamu ya hesabu za  amali pale watu wote watakapokusanyika mbele ya Mwenyezi Mungu wakiwa na yale  waliyoyatenda. Mlolongo wa matukio ulioanza siku ile ya kufufuka utaendelea kwa kila mtu kufufuka akiwa na kiwiliwili kipya na kukusanyika ukingoni mwa moto wa Jahanamu. Baadaye mashahidi wote wataletwa ndani.

Daftari la amali la kila mtu litafunguliwa na kila mtu  atahesabiwa kulingana na kile alichofanya Duniani. Baada ya hapo Waumini wote watanusurishwa na moto wa Jahanamu kwa rehema za Mwenyezi Mungu na kuingizwa Peponi. Qur'an inaelezea hatima ya Ulimwengu na hali ya Waumini siku hiyo katika aya kadhaa. Mwisho wa Dunia utakuwa pale litakapopigwa baragumu la kwanza. Dunia na Ulimwengu utahilikishwa  na kubomolewa moja kwa moja. Milima itavunjwa vipande vipande, bahari zitawaka moto na mbingu zitaondoshwa. Litakapopigwa baragumu la pili watu wote watafufuliwa na kukusanywa mahali pamoja kwa ajili ya kuhesabiwa amali zao. Kila walichokifanya hata kiwe kiduchu kiasi gani kitaleta hizaya kwa Makafiri. Lakini furaha na raha tupu kwa Waumini, kwani Mwenyezi Mungu Anaielezea siku hiyo kuwa ni siku ambayo Allah hatomdhalilisha Mtume na walioamini pamoja naye;

Enyi mlioamini tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli; huenda Mola wenu Akakufutieni  maovu yenu na kukuingizeni katika Pepo zipitazo mito mbele siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamdhalilisha Mtume (S.A.W) wala wale walioamini pamoja naye; nuru yao itakuwa inakwenda mbele yao na pande zao za kulia na huku wanasema; Mola wetu! Tutimizie nuru yetu, na utughufirie, hakika wewe ni mwenye uwezo juu ya kila kitu (66:8).

Mwenyezi Mungu anaahidi; Bila shaka sisi tunawanusuru Mitume wetu na wale walioamini katika maisha ya dunia na siku watakaposimama mashahidi (kushuhudia amali za viumbe) (40;51).

Siku ya mwisho Waumini wa kweli watapokea daftari na amali za matendo ya Duniani kwa upande wa kulia. Hesabu yao itakuwa nyepesi kama inavyosema Qur'an na watapewa stahiki yao ya kuingia Peponi;

"Basi,  ama yule atakayepewa daftari lake kwa mkono wake wa kuume (kulia) atasema (kwa furaha) Haya someni daftari langu (nililopewa sasa hivi). Hakika nilijua kuwa  nitapokea hesabu yangu (kwa vizuri, kwani nilikuwa nafanya mazuri). Basi yeye atakuwa katika maisha ya raha katika Pepo tukufu. Vishada vya matunda yake vitakuwa karibu (vinachumika bila tabu). (waambiwe) kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya vitendo mlivyofanya katika siku zilizopita (69;19-24).

Waumini wanapata kile alichoahidi Mwenyezi Mungu, watafurahi siku hiyo; (waambiwe) "ingieni (peponi) kwa salama". Hiyo ni siku ya kukaa daima (katika starehe za huko Peponi) (50;34).

Na hali yao inaelezwa hivi; Ama atakayepewa daftari lake katika mkono wake wa kulia, basi yeye atahesabiwa hisabu nyepesi. Na atarudi kwa watu wale, hali ya kuwa ni mwenye furaha. (84;7-9)

Pale watakapopewa hesabu yao, Waumini watajawa na  furaha ya kunusurika. Aya inasema; "Yaingieni salama, usalimini (kwa salama na muwe katika amani) (15;46)

Hili pia linaelekezwa katika aya nyingine:

 "Ewe nafsi yenye kutua! Rudi kwa Mola wako, hali ya kuwa utaridhika na Mwenyezi Mungu aridhike na wewe. Basi ingia katika kundi la waja wangu (wazuri) uingie katika Pepo yangu (89:27-30).

Hapo basi, Mwenyezi Mungu Amewasamehe madhambi yao wale waja waliowapa rehema na kuyabadili mabaya yao kuwa mema na kuwapa ruhusa ya kuingia Peponi.

Waja hawa wanasema; Akaambiwa "Ingia Peponi". Akasema, laiti watu wangu wangejua (haya niliyoyapata) wangejua jinsi Mola wangu Alivyonisamehe na Akanijaalia miongoni mwa walioheshimiwa (36:26-27)

Katika aya nyingine, Mwenyezi Mungu anatangaza habari hii njema kwa watu wa Peponi; Mwenyezi Mungu Atasema:

 "Hii ndiyo siku ambayo wakweli utawafaa ukweli wao. Wao watapata bustani zipitazo mbele yake mito. Humo watakaa milele. Mwenyezi Mungu Amewawia radhi; nao wawe radhi naye. Huku ndiko kufaulu kukubwa (5:119).

"Enyi waja wangu (mlio wazuri)! Hamtakuwa na khofu siku hiyo wala hamtahuzunika (43:68) Katika aya nyingine Allah Anatutaarifu Na Pepo italetwa karibu kwa wamchao Mwenyezi Mungu, haitakuwa mbali nao (50:31)

 
   
    
5 / total 9
You can read Harun Yahya's book Pepo: Maskani Ya Waumini online, share it on social networks such as Facebook and Twitter, download it to your computer, use it in your homework and theses, and publish, copy or reproduce it on your own web sites or blogs without paying any copyright fee, so long as you acknowledge this site as the reference.
About this site | Tengeneza kurasa yako ya nyumbani | Add to favorites | RSS Feed
Mambo yote yanaweza kuynakiliwa, kuchapwa na kusambazwa kwa kurejea katika kurasa hii
(c) All publication rights of the personal photos of Mr. Adnan Oktar that are present in our website and in all other Harun Yahya works belong to Global Publication Ltd. Co. They cannot be used or published without prior consent even if used partially.
© 1994 Harun Yahya.www.harunyahya.com
page_top