< <
8 / total: 9
Pepo: Makazi ya kudumu ya WachaMungu - Harun Yahya
Pepo:
Makazi ya kudumu ya WachaMungu
   

 


Sura ya Saba
Neema na Mapambo ya Peponi

Sifa kubwa ya vitu vya Peponi ni zile raha zake tofauti tofauti na starehe zenye mvuto vyote vikiwa ni kazi ya Allah (S.W) yenye ujuzi na usanii usio na mfano.  Makazi atakayotunukiwa mja aliyefuzu ni nyumba au jumba ambamo mna kila kitu tayari vikiwemo, viti vilivyonakshiwa madini ya thamani na kupangwa vizuri sehemu zilizo juu.  Nguo zilizo tayari ambazo  zimetengenezwa  kwa hariri nzito na hariri laini na kupambwa na vito vya dhahabu na fedha.  Katika Qur'an Allah (S.W) ametoa maelezo mengi kuhusu Pepo lakini maneno aliyoyatumia yanawawezesha waumini kupata picha ya jumla kwa kulinganisha na hali yao ya maisha hapa Duniani.  Katika Pepo, kila muumini atapata kila alichokihisi, na kwamba huko kuhisi kile atakachokitaka, itakuwa ni neema nyingine aliyotunukiwa na Allah (S.W). Kwa ufupi atatunukiwa aina zote za neema, vivutio na makazi mazuri vyote vikiwa vimeumbwa kwa makusudio halisi ya kumstarehesha yeye. Vyote avionavyo mwanaadamu katika vyakula, matunda, vinywaji, mavazi  ni taswira ndogo tu ya vile atakavyovikuta Peponi. Mbali na neema zilizotajwa katika Qur'an, Allah (S.W) amewaandalia Waumini mengi yaliyo nje ya ufahamu, yasiyojulikana wala kuwa na mfano wake katika maisha haya kama ambavyo Mwanaadamu kabla ya kuja hapa duniani hakuwa akifahamu lolote juu ya maisha haya na vyote vilivyomo. 

"…..Wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, tutawaingiza katika mabustani yapitayo mito mbele yake kwaajili ya kukaa humo milele.  Humo watakuwa na wake waliotakasika na tutawaingiza katika vivuli vizuri kabisa (4:57).

   Peponi ni pahali pema pa maisha ya milele ambapo Allah (S.W) amepaandaa kama malipo kwa waja walioamini kama tulivyoona hapo mwanzo. Qur'an inaielezea kwa ufupi Pepo kwa kuyataja majumba ambayo watu wataishi humo, chakula na vinywaji watakavyo kunywa, nguo watakazovaa na vitu vizuri vizuri vitakavyokutwa humo.  Tofauti na wengi wanavyodhani kuwa peponi kuna maisha ya kiroho, kwa hakika uhai na maisha ya Peponi, baada ya maisha ya ufu ya barzakh, ni uendelezo wa maisha kama haya ya Dunia. Akiwa Peponi Mwanaadamu hataishi kiroho bali ataishi akiwa na umbile lake kamili bali lililobora zaidi ya hili alilonalo sasa.  Hata hivyo maisha hayo ni mazuri mno hayawezi kulinganishwa na haya ya duniani ila kuna mambo yanayolingana.  Kutokana na mambo haya, pale waumini wanapoyafariki maisha haya ya dunia na kwenda  Akhera huwa hawapati hofu wala ugeni, hiyo ni kusema watayazoea maisha hayo kirahisi tu.  Maisha yao mapya ya milele yatakuwa ya kweli kuliko kivuli cha haya  waliyoishi hapa.  Kwa maneno mengine watakuwa na vyakula na vinywaji bora, nguo maridadi kabisa, majumba mazuri, wake na waume.  Kama isemavyo Qur'an, wataingia Peponi pamoja na wanawake ambao Allah (S.W) amewazawadia kama malipo yao na watakaribishwa kwa shangwe na shamra shamra. Kwa wenye fikra dhaifu, bora wakumbuke kuwa mke huolewa na mume huowa

Ingieni bustanini Peponi nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo (43:70). 

Qur'an inawaelezeya wanawake wa Peponi kama Mahurul-ayn. Mbali na hivyo upungufu wa dunia hii haupo kabisa Peponi;

Tutawaumba kwa umbo bora zaidi (56:35).

Umbile hili litakuwa na sifa zote bora zinazowafikiana na Pepo.  Pale tunapolitafakari umbile linalowafikiana  na sifa za Peponi, vigezo hivi vya uzuri wa wanawake hawa vinakuja fikirani; nywele zao zitakuwa safi na laini muda wote, ngozi yao itakuwa nyororo na ng'avu na harufu nzuri itakuwa ikitoka kwenye viwiliwili vyao  (Allahu A'alam). Sifa nyingine ya wanawake watakaoozwa waumini Peponi ni kwamba wanarika (hirimu) moja;

 Na pamoja nao watakuwepo wake zao watulizao macho kwa waume zao, hirimu zao (umri mmoja na wao). (38:52).

Wanasemwa kuwa wana macho haya;

 Na pamoja nao watakuwa wanawake wenye macho mazuri makubwa (37:48).

 Kuhusiana na hili aya nyingine inasema hivi;

 Watakuwamo humo wanawake watulizao macho yao; Hajawagusa Binadamu wala Jini yeyote kabla ya (waume zao) (55:56).

Wanawake hawa wanatajwa kama mayai yaliyohifadhiwa;

 Wanawake hao kama mayai yaliyohifadhiwa (37:49).

  Na kuhusu macho yao Qur'an inasema:

 Na wanawake wenye macho mazuri na makubwa kama kwamba ni Lulu zilizofichwa (56:22-23).

Aya hizi zinatuthibitishia ukweli na imani kuwa wanawake hawa wameumbwa na wamehifadhiwa sehemu maalum kwa ajili ya waume zao tu.  Neno kufichikana linaashiria kuwa ni vigumu kuwapata kwani thamani yao ni kubwa.  Kule kufananishwa kwao na yai au lulu kuna maana kuwa haiba yao ni nzuri mno mwenye kuijuwa ni Mwenyewe Muumba aliyewaumba na kuwapandikizia madaha na mbwembwe za umbile la kiwanauke kwa wanawake hao wa Peponi. Hamu na raha  anayokuwa nayo mwanaume kwa mwanamke anayempenda aliye wake peke yake, kadhalika kwa mwanamke kwa mwanamme anayempenda na wanaooneshana ukarimu, huruma, mahaba na mapenzi ya kila namna huipa nafsi ya kila mmoja raha isiyoelezeka.  Bila shaka chanzo cha hisia hizi kali lazima iumbwe katika nafsi ya Muumini kulingana na sifa za Peponi.  Katika suratil Rahmani aya ya 70 Allah amewaelezea wanawake maalumu wa Peponi kuwa ni wazuri wa tabiya, warembo na wazuri wa sura:

Wamo humo wanawake wazuri (wa tabia), wazuri (wa sura na miili) (55:70).

Katika sura hiyo hiyo inabainishwa kuwa wake hawa wa waumini wapo kwa ajili ya waume zao tu.  Neno hawajaguswa na mtu au Jini linashadidia ubikira wao.  Suratil Wakiya aya ya 36 inatilia mkazo jambo hili kwa kusema kuwa tumewafanya kuwa waliotakasika. Sura ya 55:72 inasema wana macho meupe mazuri makubwa wanaotawishwa majumbani. Allah anawazungumzia hivi waumini na wake zao Peponi;

"Kwa yakini watu wa peponi leo wamo katika shughuli zao wamefurahi, wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fahari (36:55-56).

Pepo nje ya dhana

Mwenyezi Mungu anaelezea jozi ya waumini waume na wake zao Peponi kama ifuatavyo:

"Kwa yakini watu wa peponi leo wamo katika shughuli zao, wakiwa wamefurahi ; wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea katika viti vya fahari". (36:55-56).

Huko waumini wote wana wake zao wenyewe ambao wameumbwa vizuri wakiwa na sifa zote za uanauke na uzuri.  Ni Wacha Mungu na wenye rika moja na waume zao:

 "Tutawaumba kwa umbo (bora zaidi). Na tutawafanya vijana kama kwamba ndio kwanza wanaolewa. Wanapendana na waume zao walio hirimu moja na wao".(56:35-37)

Hii inatupa elimu ya kuwa, hapa Duniani waume na wake walio waumini wanatakiwa kujengeana huba na mapenzi siyo kwa sababu ya maslahi ya kidunia bali kwa ajili ya kutafuta radhi za Allah (S.W).  Katika suratil Ar-Rahmani  aya ya 70 Allah anasema ; "Wamo humo wanawake wazuri (wa tabia ) na wazuri wa sura pia". Aya hii inabainisha kuwa wanawake hao wana haiba ya kupendeza, hawajaguswa kimaumbile na ni wasafi wa nafsi zao, wenye bashasha, wakarimu na wenye kila aina ya mvuto.  Hapa yaweza kusemwa kuwa wana zile sura zenyewe hasa,  zisizo na kasoro yoyote, ni wazuri wa sura na tabia.  Katika suratil  At-tur, aya ya 20,  Mwenyezi Mungu anasema ; "Watakuwa wameegemea juu ya viti vya fahari vilivyopangwa safu safu, na Tutawaoza wanawake wanaopendeza wenye macho ya vikombe".

Kwa kweli kufanya maongezi huku mkiwa mmekaa  kwenye viti vya fahari kwa kuelekeana kuna raha ya aina yake.  Pale tunapozungumza na mtu kwa kawaida huwa tunamtazama usoni mwake. Kwa hiyo kufanya maongezi mazuri na wanaume au wanawake wenye sura nzuri, wanaozungumza maneno ya kufurahisha katika makazi mazuri ambako Allah (S.W) anashukuriwa na kuhimidiwa, kutampa mtu starehe isiyoelezeka. Bila shaka, sifa za wanawake hawa haziishii usoni mwao tu, kwani kuanziya kichwani hadi vidoleni wameumbwa kwa urembo mkubwa.  Surati Sad, aya ya 52 inasema ;

"Na pamoja nao watakuwemo wake zao watulizao macho kwa waume zao hirimu zao".  

Qur'an inawafananisha wanawake hao na Yakuti na Marijani  madini ya thamani ambayo yanapendeza mno machoni ;

"Kama kwamba wao (wanawake hao) ni Yakuti na Marijani ".(55:58).

Kwa kuwafananisha na madini haya, Qur‘an inashadidiya uzuri wa wanawake hao, hapa inajenga taswira kwa kuwafananisha na Yakuti na Marijani, maana yake ni kuelezeya jinsi walivyo warembo, rangi yao nzuri inayomeremeta. Kwa mlingano huu tu na kwa maelezo mengi mengineyo, waumini wanaweza kuelewa jinsi malipo aliyowaandalia Mwenyezi Mungu yalivyo makubwa   kwa hiyo basi watu wwajipinde kutafuta radhi za Allah (S.W) na waombe rehema zake ili waingizwe peponi. Katika Qur ‘an Mwenyezi Mungu ameziweka bayana neema za peponi kwani zipo nje ya uwezo wa kufikiri  na hata kudhani. Peponi Allah (S.W) anawaruzuku waumini neema zisizo na hesabu ambazo jicho halijaziona wala sikio halijasikiya.

"Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe (vya dhahabu) : na vitakuwamo ambavyo nafsi inavipenda na macho yanavifurahia, na ninyi mtakaa humo milele". (43:71).

Tunaweza kupata picha ya jumla ya jinsi Pepo ilivyo kutokana na fununu kuwa neema za pepo zinafanana na zile za Dunia hii, ingawa vifananavyo huweza kutafatautiana pakubwa,

"Na wabashirie walioamini na kufanya vitendo vizuri, kwamba watapata mabustani yapitayo mito mbele yake; kila mara watakapopewa matunda humo kuwa ni chakula watasema; haya ndiyo yale tuliyopewa zamani (ulimwenguni ). Kwani wataletewa (matunda hayo) hali ya kuwa yamefanana na (yale waliyokuwa wakiyajua ulimwenguni . wataletewa kwa sura hiyo lakini utamu mwingine  kabisa ): na humo watapata wake waliotakasika na watakaa milele".(2: 25).

Kwa hayo maelezo na mifano iliyomo katika Qur'an, tunapata ufahamu fulani  wakati tungali tukiishi katika dunia hii.  Hata hivyo Mwenyezi Mungu katupa ufahamu huu kwa ajili tu ya kutupa picha Pepo ikoje lakini kwa kweli starehe na neema zake ziko nje kabisa ya ufahamu wetu.  Kwa mfano ndani ya Pepo mna mito ya maji yasiyotibuka na mito ya maziwa ambayo ladha yake haibadiliki kamwe na mito ya vinywaji na mito ya asali. Jiografia hiyo haipo kabisa katika maumbile ya ulimwengu huu, Suratil Muhammad, aya ya kumi na tano inabainisha kuwa pepo inakusanya yote yaliyo mazuri ambayo hayawezi kulinganishwa na ya dunia hii:

Mfano wa pepo walioahidiwa wacha Mungu ni huu,  imo mito ya maji yasiyovunda,  na mito ya maziwa yasiyoharibika ladha yake na mito ya mvinyo wenye ladha kwa wanywao na mito ya asali iliyosafishwa; tena humo watapata matunda ya kila namna , na samahani kutoka kwa Mola wao. Basi je hao watakuwa sawa na wale watakao kaa mtoni na kunyweshwa maji yachemkayo yatakayo kata chango zao.

Aidha Hadithi inabainisha uzuri huo wa Pepo usio fikirika, Allah (S.W) kasema :Nimewaandalia waja wangu wanichao vitu ambavyo havijaonwa na jicho wala kusikiwa na sikio wala hata kufikiriwa na mwanadamu (Muslim). Katika aya moja: Mwenyezi Mungu anasema waumini wataishi katika Pepo kama wageni wake rasmi na waalikwa  waliokaribishwa:

"Lakini waliomcha Mola wao watapata Mabustani (pepo) yanayopita mito mbele yake.  Watakaa humo milele.  Ndio makaribisho yao yatokayo kwa Mwenyezi Mungu.  Na vilivyopo kwa Mwenyezi Mungu ni  starehe nzuri kabisa kwa watu wema (kuliko starehe hizi wanazozipata wabaya duniani)". (3:198).

Katika aya hii Allah anaielezea Pepo kama ni sehemu ya raha, furaha , uhondo na starehe kubwa.  Pale Dunia itakapofika mwisho wake na tukifaulu mtihani na kuyapata makazi haya halisi, kwa kweli, tutakuwa tumepata neema kubwa kweli kweli.

 
   
    
8 / total 9
You can read Harun Yahya's book Pepo: Maskani Ya Waumini online, share it on social networks such as Facebook and Twitter, download it to your computer, use it in your homework and theses, and publish, copy or reproduce it on your own web sites or blogs without paying any copyright fee, so long as you acknowledge this site as the reference.
About this site | Tengeneza kurasa yako ya nyumbani | Add to favorites | RSS Feed
Mambo yote yanaweza kuynakiliwa, kuchapwa na kusambazwa kwa kurejea katika kurasa hii
(c) All publication rights of the personal photos of Mr. Adnan Oktar that are present in our website and in all other Harun Yahya works belong to Global Publication Ltd. Co. They cannot be used or published without prior consent even if used partially.
© 1994 Harun Yahya.www.harunyahya.com
page_top