Dalili Za Kiyama

SHUSHA KITABU

Download (DOC)
Maoni

SURA ZA KITABU

< <
4 / total: 5
Dalili za Kiyama - Harun Yahya
Dalili za Kiyama
   

 


Mitetemeko ya ardhi 

Hapana shaka kuwa katika historia, hakuna majanga ya asili ambayo yamewaathiri watu kwa kiasi kikubwa kama mitetemeko ya ardhi. Mitetemeko ya ardhi hutokea mahali popote na wakati wowote. Kwa karne zote mitetemeko ya ardhi imesababisha maafa na hasara kubwa ya mali. Kwa sababu hii tetemeko la ardhi ni janga linalohofiwa mno. Hata teknolojia ya karne ya Ishirini na Ishirini na moja imeweza kwa kiasi kidogo sana kuzuia uharibifu wa tetemeko la ardhi.

Tetemeko la ardhi la mwaka 1995 kule Kobe laweza kuwa somo kwa wale wanaodhani kuwa teknolojia itaweza kudhibiti maumbile. Itakumbukwa kuwa tetemeko hili la ardhi lilitokea bila kutarajiwa kwenye eneo kubwa la viwanda na usafirishaji. Licha ya ukweli kwamba lilidumu kwa sekunde ishirini tu, kama lilivyoripoti gazeti la Time, bado lilisababisha hasara ya dola bilioni 100. Kadhalika tetemeko la ardhi ndani ya bahari lililofahamika kama Tsunami fukweni mwa nchi za Indonesia, Thailand na ukanda mzima wa Pwani ya Asia, lilikuwa la aina yake kupata kutokea katika historia ya mwanaadamu.

Katika miaka michache iliyopita mitetemeko mikubwa ya ardhi imetokea mara kwa mara na ndio matishio makubwa ya maisha ya watu duniani kote. Tukiangalia takwimu zilizokusanywa na kituo cha taarifa za matetemeko ya ardhi cha Amerika mwaka 1999 tunaona kuwa mitetemeko ipatayo 20, 832 ilitokea sehemu mbali mbali duniani. Matokeo yake watu wanaokadiriwa kufikia 500,000 walikufa. Matukio yote haya yanakumbushia maneno ambayo Mtume (s.a.w) aliyasema miaka 1400 iliyopita:

Kiama hakitasimama mpaka pale mitetemeko ya ardhi itakapotokea mara kwa mara. (Bukhari).

Katika Qur’an kuna aya kadhaa zinazobainisha uhusiano kati ya mitetemeko ya ardhi na zama za mwisho. Sura ya 99 inaitwa suratil Zil Zaala ambayo maana yake ni mtikisiko au tetemeko la ardhi. Sura hii yenye aya nane inaelezea mtetemeko mkubwa wa ardhi na inasema kuwa kufuatia mtetemeko huo siku ya hukumu itakuwa imefika. Watu watafufuliwa makaburini na kutoa hesabu ya amali zao kwa Mwenyezi Mungu na kupata malipo yao hata kwa jambo dogo sana walilolifanya:

Itakapotetemeshwa ardhi kwa mtetemesho wake mkubwa. Na itakapotoa ardhi mizigo yake, na binadamu akasema (wakati huo) (oh!) ina nini leo ardhi? Siku hiyo itatoa habari zake zote kwa kuwa Mola wake ameifunulia (ameiamrisha kufanya hayo). Siku hiyowatu watatoka (makaburini) vikundi vikundi ili waonyeshwe vitendo vyao. Basi anayefanya wema hata kwa kiasi cha uzito wa mdudu chungu ataona jazaa yake na anayefanya uovu hata kwa kiasi cha uzito wa mdudu chungu ataona jazaa yake. (99:1-8).

Umasikini

Inafahamika kuwa umasikini ni ukosefu wa chakula, makazi, mavazi, huduma za afya na mahitaji mengine ya msingi kwa sababu ya kipato duni. Licha ya fursa zinazopatikana kutokana na maendeleo ya teknolojia, umasikini hivi leo ni moja kati ya matatizo makubwa kabisa yanayoukabili ulimwengu. Katika mabara ya Afrika, Asia, Amerika Kusini na Ulaya Mashariki watu wengi wanahangaika na njaa kila siku. Kwa sababu ya mgao mbaya wa rasilimali za ulimwengu umasikini umesababisha uwepo mgawanyiko kati ya nchi za kaskazini ya jangwa la sahara ambazo ni za ulimwengu wa kwanza na nchi za kusini maskini ambazo ni za ulimwengu wa tatu.

Ubeberu na Ubepari usio na mipaka unazuia mgawanyo wa kipato ulimwenguni kote na unakwaza maendeleo ya nchi changa na nchi zinazoendelea. Wakati ambapo kuna watu wachache wanaofurahia kipato kinachozidi mahitaji yao, kuna idadi kubwa ya watu wanaohangaika na matatizo ya umasikini na ufukara. Katika Ulimwengu wa leo umasikini umefikia hatua mbaya au kiwango kibaya sana.

Ripoti ya mwisho ya UNICEF ilieleza kuwa mmoja kati ya kila watu wanne duniani anaishi katika tabu na shida isiyoelezeka. Watu bilioni 1.3 duniani wanaishi kwa wastani wa chini ya dola moja kwa siku. Watu bilioni 3 duniani wanaishi kwa dola mbili kwa siku. Takribani watu bilioni 1.3 hawapati maji safi. Watu bilioni 2.6 hawapati maji salama.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la chakula duniani, (FAO), Mwaka 2000, watu milioni 826 duniani kote hawapati chakula cha kutosha. Kwa maneno mengine mmoja katika kila watu sita ana njaa. Katika miaka kumi iliyopita dhulma katika mgawanyo wa kipato imeongezeka kwa kiwango kisichosemeka.

Ripoti za umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, katika mwaka 1960 asilimia 20 (20%) ya watu wanaoishi katika nchi tajiri kabisa duniani walikuwa na pato lilozidi mara thelathini pato la nchi 20 masikini kabisa. Hadi kufikia mwaka 1995 iliongezeka mara 82. Kikiwa ni kielezeo cha kutoweka kwa haki ulimwenguni, mali za matajiri 225 wakubwa kabisa ulimwenguni ni sawa na pato la mwaka la asilimia 47 (47%) ya nchi masikini ulimwenguni.

Takwimu za sasa zinaonyesha yale ambayo Mtume (s.a.w) aliyasema juu ya kuongezeka kwa umasikini. Katika hadithi inabainishwa kuwa umasikini na njaa ni miongoni mwa dalili za kipindi cha kwanza cha zama za mwisho:

Masikini wataongezeka (Amal Al Diin Al Qazwin, Mufid Al Ulum wa Mubid Al humum)

Kipato kitagawanywa kwa matajiri tu, hakuna mafao kwa masikini. (Tirmidhi).

Ni dhahiri kuwa kipindi hicho kilichobashiriwa na Mtume (s.a.w) kinawiana na hali ya wakati wetu wa leo. Tukiangalia karne zilizopita tunaona kuwa shida na tabu zilizoletwa na ukame, vita na majanga mengine zilikuwa za muda mfupi na ziliishia katika eneo moja moja. Lakini umasikini na shida za leo ni za kudumu na sugu. Kwa hakika Mola wetu ni Mwingi wa Rehma, yeye hadhulumu watu lakini kwa sababu ya ukosefu wa shukurani wa wanadamu na maovu wanayoyafanya, umasikini na tabu vimeongezeka. Kwa hakika hali ya mambo ya kusikitisha inaonesha wazi kuwa dunia imetanzwa na uchoyo na ubinafsi.

Kuporomoka kwa maadili,  kushamiri kwa ushoga na ukahaba

Katika zama zetu za leo kuna janga kubwa linalohatarisha uhai wa jamii ulimwenguni. Mithili ya virusi vinavyoua mwili, janga hili linasababisha msiba mkubwa wa kijamii. Janga hilo ni mmomonyoko wa maadili ambayo husaidia kustawisha jamii. Ushoga, Ukahaba, uhusiano haramu wa kijinsia kabla ya ndoa na nje ya ndoa, Filamu za ngono, Picha za ngono, unyanyasaji wa kijinsia na ongezeko la maradhi ya zinaa, mashindano ya kukaa uchi maarufu ulimbwende, uuzaji na utumiaji wa vileo na dawa za kulevya miongoni mwa vijana ni miongoni mwa ishara kubwa za kuporomoka kwa maadili.

Mambo haya ndiyo yamekuwa yakizishughulisha jamii. Idadi kubwa ya watu haijali hatari hii inayozidi kuwa kubwa na wanaiona kama jambo la kawaida tu. Lakini takwimu zinaonesha kuwa kila siku ipitayo kiwango cha hatari kinazidi kuongezeka. Ongezeko la maradhi ya zinaa ni kigezo kikuu cha kusaidia kuonesha ukubwa wa matatizo yanayomkabili mwanadamu.

Kwa mujibu wa rekodi za Shirika la Afya ulimwenguni magonjwa yanayotokana na zinaa yanachukuwa sehemu kubwa ya maradhi. Ripoti zinaonesha kuwa kati ya kesi mpya za magonjwa ya zinaa zinazokadiriwa kufikia milioni 333 kila mwaka ulimwenguni kote, Ukimwi ndio tatizo kubwa zaidi.

Takwimu za Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) zinaonesha kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi tokea pale ulipoanza imefikia watu milioni 18.8. Ripoti za shirika hilo kwa mwaka 2000 zinaielezea hivi hali ya mambo: “Ukimwi una nafasi ya kipekee katika kuleta athari mbaya za kijamii, kiuchumi na katika mipango ya sensa ya maendeleo”.

Miongoni mwa mambo mabaya kabisa yanayozidi kushamiri ni ushoga. Katika baadhi ya nchi jambo hili limehalalishwa kama ndoa, linapewa heshima zote za ndoa na limeundiwa vyama na jumuiya. Duniani kote uovu huu unapingwa. Kushamiri kwa ushoga hivi leo kunatukumbusha hatima ya watu wa Lut waliokithiri katika uovu huu. Kama isemavyo Qur’an walipoukataa wito wa Lut kuiendea njia sahihi, Mwenyezi Mungu aliuangamiza mji na watu wake kwa maangamizi makubwa.

Ni dhahiri kuwa zile hadithi zinazoelezea zama za mwisho na mporomoko wa maadili zinathibitika hivi leo. Hadithi moja inasema kuwa kutoweka kwa aibu katika dhambi ya ukahaba ni dalili ya kiama:

Kutashitadi maingiliano haramu ya kijinsia wazi wazi (Bukhari).

Saa hiyo itafika wakati uzinzi utakapokuwa umeenea sana (Al-Haythami, kitab al fitan)

Kufifia kwa maadili na hisia ya aibu kunaelezwa kwa maneno haya:

Saa ya mwisho haitasimama hadi pale watu watakapofanya uzinzi njiani (njia wanazopita watu) ( Ibn Iban na Bazzar).

Yafaa kukumbuka kuwa hivi sasa matukio ya ukahaba yanayochukuliwa na kamera za siri yamekuwa yakioneshwa katika Internate, vituo vya Televisheni na katika magazeti yanayoitwa ya ngono na udaku. Makahaba wanaingiliana na wateja wao wazi wazi katikati ya mitaa. Hali kadhalika kuna Filamu na picha nyingi zinazosambazwa ulimwenguni kote ambazo zinaonesha uzinzi unavyofanyika wazi wazi. Takriban katika miji mingi duniani makahaba wamekuwa wakisimama na wateja wao na kufanya mambo ya ajabu barabarani hasa nyakati za usiku.

Hii ni dalili nyingine ya kiama iliyobainishwa katika hadithi. Mamilioni ya watu wanaishuhudia wenyewe dalili hii duniani kote. Hadithi zifuatazo zinaonyesha kuwa kuibuka kwa ushoga kuwa jambo la kawaida la maisha ni ishara kuu ya zama zinazokaribia siku ya mwisho:

Wanaume watawaiga wanawake na Wanawake watawaiga wanaume. (Allama Jalaluddin Swiyuti, Durre- Mansuri).

Watu watazama katika ushoga na usagaji (Al Mutaqi al Hindi, Muntakhab, Kanzul Ummaal).

Vitendo vya wanaume kuwaiga wanawake na wanawake kuwaiga Wanaume vimekuwa vingi hivi leo. Tunashuhudia Wanaume wanaosuka nywele zao na pia tunashuhudia Wanaume wanaowasuka nywele wanawake kwenye Masaluni na majumbani. Imekuwa ni aina ya ajira kwa wanaume hawa hasa Wamasai kupita mitaani kusuka nywele akina Mama.

Pia tunashuhudia Wanaume wakivaa hereni masikioni na vidani shingoni. Tunashuhudia teknolojia ikitumika vibaya kubadilisha maumbile ambako kumeleta kiroja cha mwanaume kubeba uzazi na kujifungua! Kwa upande mwingine tunashuhudia Wanawake wakivaa mavazi ya Wanaume, wakijaribu kuiga usemaji wa kiume. Wakioa wanawake wenziwao na wakifanya kazi za mitulinga. Tunashuhudia wanawake wakivaa mavazi yenye kuonesha vivazi vyao vya ndani na maungo mateke ili kushawishi uzinzi.

Kukanusha dini sahihi na maadili ya Qur’an

Hadithi zinazozungumzia dalili za siku ya mwisho zinatupa maelezo ya kina juu ya wakati ambao dalili hizi zitadhihirika. Twaweza kufahamikiwa kutokana na hadithi za Mtume (s.a.w) kuwa awamu ya kwanza ya zama za mwisho ni kipindi ambacho kitaonekana kuwa cha kidinidini, lakini kumbe ni kipindi ambacho kitaikataa kabisa dini ya Allah na maadili ya Qur’an.

Ni kipindi ambacho yale mambo yaliyobainishwa katika aya za Qur’an yatafumbiwa macho, dini itatumbukia katika mifarakano, migogoro, hamasa na ushabiki. Ibada zitafanywa kwa ria na dini itatumika kama biashara ya kujipatia faida na maslahi ya kidunia. Ni katika kipindi hiki ambapo Imani haitategemea elimu na utafiti bali itakuwa mwigo wa kufuata mkumbo tu na hamasa ya mtu. Katika kipindi hiki watu wanaoitwa Waislamu watakuwa wengi mno wakati ambapo wanazuoni wa kweli na Waislamu wenye Ikhlasi watakuwa wachache mno.

Zifuatazo ni dalili zilizotajwa na Mtume (s.a.w) Karne 14 zilizopita, dalili ambazo zinathibitika wazi wazi katika wakati tulionao:

Kwa mujibu wa Qur’an, Mtume (s.a.w) anasema kuwa watu wake wameitelekeza Qur’an:

Na Mtume alikuwa akisema, Ewe Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya Qur’an hii kuwa kitu kilichoachwa. (25:30).

Inabainishwa katika hadithi kuwa katika zama za mwisho muongozo wa Qur’an utatupiliwa mbali na watu watajitenga nao:

Karibia ya kusimama kwa saa kutakuwa na zama ambazo elimu ya (Qur’an) itatoweka na giza totoro litagubika… (Bukhari).

Utakuja wakati wa uma wangu ambapo hakutabaki chochote kilichobaki katika Qur’an isipokuwa sura yake ya nje tu na hakutabaki chochote cha Uislamu isipokuwa jina lake tu na wao watajiita kwa jina hili ingawaje ni watu waliombali kabisa na Uislamu. (Ibn Babuya, Thawab ul-A’amal).

Mfano umetolewa katika suratil Jumaa aya 5:

Mfano wa wale waliopewa Taurat, kisha hawakuichukua kwa ktuitumia ni kama Punda anayebeba vitabu vikubwa vikubwa…Hapana shaka kuwa aya hii inatoa onyo kwa Waislamu, ikiwakumbusha kuwa wajihadhari wasije wakatumbukia katika dhambi ileile nzito. Qur’an imeshushwa kama kitabu cha muongozo ambao watu waufuate.

Mtume (s.a.w) kasema kuwa licha ya ukweli kuwa Qur’an itasomwa lakini elimu na hekima iliyomo ndani yake hatazingatiwa. Hii di dalili nyingine ya ule wakati wa zama za mwisho:

Utakuja wakati juu ya umma ambapo watu watasoma Qur’an lakini haitakwenda kokote isipokuwa itaishia kwenye makoo yao (haitaingia nyoyoni.) (Bukhari).

Mtume wa Allah alisema jambo fulani kisha akasema utatokea wakati ambapo elimu haitakuwepo tena. Aliuliza Ziyadi: Ewe Mtume wa Allah itatowekaje elimu licha ya ukweli kuwa tutakuwa tukiisoma Qur’an na kuwafundisha watoto wetu kuisoma na watoto wetu nao watawafundisha watoto wao kuisoma hadi siku ya kufufuliwa? Hapo Mtume akasema je Mayahudi na Wakristo hawasomi Taurati na Biblia na kutotenda kwa mujibu wa yale yaliyomo humo? (Ahmad, ibn Majah, Tirmidhi).

Watu kuitumia dini kwa malengo ya kidunia na kujivika ngozi ya kondoo waonekane wema.

Kufuata maadili ya Wayahudi na Wakristo

Ni dalili moja wapo ya kiama kuwa baadhi ya Waislamu watafuata nyendo za Wayahudi na Wakristo tena watawaiga kimasonge. Mtume (s.a.w) kasema:

“Kwa hakika mtafuata nyendo za watu waliokuwepo kabla yenu shubiri kwa shubiri na dhiraa kwa dhiraa (Inchi hadi Inchi) kiasi ambacho hata wakitumbukia kwenye shimo la Kenge nanyi pia mtawafuata humo” tukauliza, ewe Mtume wa Allaha, una maana kuwa ni Wayahudi na Wakristo? Akajibu, kama si wao ni nani tena? (Bukhari) kutokana na hadithi hiyo tunaona kuwa kabla ya zama za mwisho kutakuwa na mielekeo mibovu ya kifikra na kimaadili na kwamba tawala zitakazokuwepo zitajitenga mbali na ukweli na haki jambo litakalosababisha mfarakano mkubwa na kuwatoa watu katika mafundisho ya Mwenyezi Mungu.

Jambo la kuzingatia hapa ni kuwa maadili ya Wayahudi na Wakristo ndio maadili ya magharibi au ya Wazungu, na mifumo ya maisha iliyojitenga na Qur’an ndio mifumo ya Magharibi inayotawala dunia hivi leo.

Muumini na Kafiri

Mtume wa Mwenyezi Mungu kasema:

Kabla ya saa ya mwisho kutakuwa na vurugu vurugu tupu ambapo mtu atakuwa Muumini asubuhi na Kafiri jioni yake au atakuwa Muumini jioni na Kafiri asubuhi yake. (Abuu Daudi)

Kuna vielezeo vingi vinavyoonesha hali hiyo hivi leo. Mtu anaweza kuswali swala tano lakini akawa muasherati, anaweza kushinda kutwa nzima anaswali lakini usiku anazini, anaweza kushinda na swaumu kutwa nzima lakini usiku yuko na hawara au kimada, mwingine anaweza kuwa sala tano lakini muongo, mwizi, tapeli, mla rushwa, mla riba na kadhalika. Mseto huu wa Uumini na Ukafiri unaonekana kwa watu wengi hivi leo japo kwa sura tofauti.

Kutozingatia halali na haramu

Dalili nyingine ya kiama ni kuwa watu hawatazingatia yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu katika Qur’an. Mtume (s.a.w) kasema:

Utafika wakati ambapo mtu hatojali kama vitu avipatavyo ni vya halali au ni vya haramu (Bukhari).

Wanazuoni wenye nyuso mbili

Mtume (s.a.w) kasema: Katika zama za mwisho baadhi ya watu wanaokubalika kama wanazuoni watakuwa wanafiki kweli kweli wenye nyuso mbili;

Mbwa Mwitu watasoma katika zama za mwisho. Wale watakaoziona zama hizo waombe nusra kwa Mwenyezi Mungu kutokana na uovu wa wanazuoni hao. Kutakuwa na mafisadi kweli kweli. Unafiki ndio utakaoshitadi. (Tirmidhi, Nawadil al Usul.)

Kutatokea watu katika zama za mwisho ambao watajinufaisha kwa kutumia dini (Tirmidhi)

Kutumia dini kwa malengo ya kidunia

Mtume wa Allah kasema;

Katika zama za mwisho watu wataitumia dini kitapeli kwa malengo yao ya kidunia na kujivika ngozi za kondoo hadharani kuonesha unyenyekevu. Ndimi zao zitakuwa tamu kama sukari lakini nyoyo zao zitakuwa nyoyo za Mbwa mwitu. (Tirmidh).

Watu hawatoheshimu mipaka ya sheria za Kiislamu. Hawatochelea kuutumia Uislamu kwa ajili ya kujipatia maslahi yao. Watu watajali zaidi kuonekana wanatenda mambo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wakiwa hawana chembe ya wema, huruma na usaidizi kwa wanaowahubiria. Watakuwa wakiwakamua wafuasi wao kutoa kwa kutumia aya na mahubiri ya kukhofisha na kutumainisha hali yakuwa wao wenyewe hawana ukweli katika nafsi zao.

Katika zama za mwisho za umma wa walioamini, watu watapamba Misikiti lakini wataziacha nafsi zao katika maangamizi, watu ambao watashindwa kuitunza dini ya Mwenyezi Mungu kama wanavyozitunza nguo zao, watatelekeza majukumu ya dini yao kwa sababu ya shughuli zao, watu hawa watakuwa wengi.

Kutotekeleza amri ya kutenda mema na kuepuka mabaya

Miongoni mwa dalili za kukaribia kiama ni kuwa watu wanaojua kuwa Mwenyezi Mungu amewaamrisha kutenda mema na kuepuka uovu hawatatekeleza jambo hilo: Siku ya mwisho haitasimama mpaka watakapobakia watu ambao hawatajali mema na kamwe hawatozuia maovu (Ahmad).

Karibu na kusimama kwa kiama mambo mema yatapungua (Bukhari) Katika hadithi nyingine inabainishwa dalili ya kiama kuwa Waislamu walioamini watadhoofishwa kwa msukumo wa watenda dhambi:

Saa itafika pale sauti zitakapopazwa misikitini (Tirmidh)

Saa itafika pale viongozi watakapokuwa madhalimu (Al Haithami, Kitab al Fitan)

Mtume (s.a.w) kasema, katika zama za mwisho, kutakuwa na watu wachache sana wanaoweza kuitwa waumini:

Utafika wakati kwa watu wangu ambapo misikiti itajaa watu lakini watakuwa hawana muongozo sahihi (Ibn Babuya, Thawab ul A’mal

Hadith moja inasema kuwa waislamu wa kweli watalazimika kuficha imani zao na kufanya ibada kwa siri:

Wakati utafika ambapo wanafiki wataishi kwa siri miongoni mwenu na wenye imani watajaribu kuhuisha dini yao kwa watu wengine

Katika Hadith ifuatayo inabainishwa ishara ya zama za mwisho kuwa Misikiti itafanywa sehemu za mikusanyiko ya kijamii tu.

Utafika wakati ambapo watu watatumia misikiti kama vijiwe tu vya kukutania.

Katika zama mwisho, watatokea watu watakaosoma Qur’an kwa ajili tu ya kujinufaisha badala ya kupata radhi za Allah:

Na aombe thawabu kwa Allah yule asomaye Qur’an. Kwa sababu katika zama za mwisho kutakuwa na watu wengi watakaosoma Qur’an na kutafuta malipo kwa watu wengine. (Tirmidhi).

Dalili nyingine ni kuwa Qur’an itasomwa kwa ajili ya kujifurahisha (kujiburudisha) tu kama vile wimbo:

Wakati Qur’an itakaposomwa mithili ya uimbaji wa nyimbo na wakati mtu atakapoheshimika (atakaposifika) kwa kuimba namna hiyo hata kama hana ilimu ( Al-Tabarani, Al-Kabir)

Baadhi ya watu watakaotambuliwa kama Waislamu watakuwa na uelewa potofu juu ya kadari, wakati ambapo wengine wataamini nyota kuwa zinaweza kuwapatia ujuzi wa kujua maisha yao ya baadae. Hii ni dalili ya zama za mwisho:

Saa itafika wakati watu watakapoamini nyota na kukanusha Qadari

(Al-Haythami, Kitab al Fitan)

Licha ya ukweli kwamba Mwenyezi Mungu ameharamisha riba hivi leo riba ndio mtindo wa maisha. Katika Hadith ifuatayo hii inaelezewa kama dalili mojawapo ya ya kiama:

Bila shaka kitakuja kipindi ambacho hakuna hata mtu mmoja atakayesalimika na riba. Endapo mtu ataepuka riba kwa njia ya moja kwa moja basi hatoweza kuukwepa moshi (athari) utakaotokana nayo. Kwa kiasi fulani athari zake zitamfika tu. (Imesimuliwa na Abu Huraira)

Hapa labda tutoe ufafanuzi kidogo. Katika ulimwengu wetu wa leo riba imejikita katika mifumo ya fedha na uchumi wa kitaifa na kimataifa. Aidha sekta za kiserikali na binafsi zinashiriki katika uchumi wa riba. Mabenki na makampuni binafsi ya kitaifa na kimataifa hasa yale yanayoendesha shughuli za ukopeshaji wa fedha au bidhaa yanatoza riba kwa viwango mbalimbali. Karibu Asasi zote za utoaji wa mikopo ya fedha zinatoza riba.

Kwa hali hiyo hakuna mtu ambaye anaweza kudai kuwa yeye amesalimika na riba. Maadam mfumo wa uchumi wa Taifa haukusalimika na riba basi sote tunahusika na jambo hili. Hivyo hadithi ya Mtume (s.a.w) inawafikiana kabisa na mazingira yetu.

Dalili nyingine ya zama za mwisho ni kuwa Hija itafanywa kwa ajili ya kusafiri tu, kufanya biashara, kujionesha tu na kuombaomba.

Wakati huo utafika pale matajiri watakapokwenda Hija kwa malengo ya kusafiri kwa minajili ya kujifurahisha, biashara, kujifaharisha na kujionesha, na masikini kwenda kuomba.

Imesimuliwa na Anas (r.a )

Tatizo kubwa ambalo Wanaadamu wanakabiliana nalo hivi leo ni kusambaratika kwa jamii. Kuporomoka huku kwaonekana katika vipengele mbali mbali vya maisha. Kuvunjika kwa familia, ongezeko la talaka na uzazi haramu ndio mambo ambayo yanapelekea kusambaratika kwa taasisi ya familia. Maisha hivi leo yamekuwa ya misukosuko, mashaka, huzuni, wasiwasi na vurugu tupu.

Watu waliokosa maadili ya kiroho wanaona kuwa ili kuondokana na adha ya dunia basi bora wajitumbukize katika ulevi wa pombe na dawa za kulevya. Wengine wanaona kuwa hakuna ufumbuzi wa hali ngumu inayowakabili basi njia wanayoona itawatowa matatizoni ni kujinyonga. Moja ya Ishara kubwa za kuanguka kwa jamii ni kule kuongezeka kwa mambo ya haramu.

Kiwango cha uhalifu kimeongezeka kwa kiasi kinachowashangaza mabingwa wa maswala ya jamii. Ripoti ya uhalifu na haki ulimwenguni, “Universal Crime and Justice,” Iliyotayarishwa na kituo cha udhibiti wa jinai cha umoja wa mataifa, United Nations’ International Crime’ imetoa tathmini ya jumla ya uhalifu ulimwenguni. Ripoti hiyo inasema:

Kimsingi, kama ilivyokuwa katika miaka ya themanini, kiwango cha uhalifu pia kiliendelea kuongezeka katika miaka ya tisini. Kila mahali ulimwenguni, katika kila kipindi cha miaka mitano, theluthi moja ya watu wanaoishi mijini wamekumbwa na mikasa ya uhalifu. Kote ulimwenguni vitendo vya wizi, ujambazi, utapeli, uasherati vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku. Matukio haya, pamoja na sababu nyinginezo, yamekuwa yakihusishwa na athari mbaya za kiuchumi.

Kiwango cha utumiaji wa dawa mbali mbali za kulevya nacho kimeongezeka katika miaka ya karibuni. Watu hasa vijana wamekuwa wakibwia unga na kujidunga sindano zenye dawa za kulevya. Kwa kweli tatizo hili limeleta madhara ya kiafya, athari mbaya za kifamilia na kijamii.

Kwa hakika sababu za matatizo yote haya zimeelezwa katika Qur’an pale inaporejea historia ya jamii zilizopita.

Kuporomoka kwa jamii na matatizo mbali mbali ni matokeo ya wanadamu kumsahau Mwenyezi Mungu na lengo halisi la maisha na hivyo kuyatupa maadili ya kiroho.

Matukio yote ya kuporomoka kwa jamii tunayoyashudia hivi leo tayari yalikwishabashiriwa na Mtume (s.a.w) karne 14 zilizopita.

Mtume (s.a.w) amesema kuwa miongoni mwa dalili za zama za mwisho ni pale watu watakapokabiliana na vita na mabadiliko ya kijamii (Ahmad Diya”al diin al Kamush Khanawi, Ramuzi al ahadith). Zifuatazo ni hadith zinazohusiana na awamu ya kwanza ya zama za mwisho:

Kutakuwa na miaka ya udanganyifu ambapo mtu mkweli hatoaminiwa na muongo ataaminiwa (Ibn Kathir).

Kutakuwa na miaka ya vurugu. Watu watamuamini muongo na kutomuamini yule anayesema ukweli. Watu hawatamuamini mtu mkweli na watamuamini yule ambaye ni fisiki. (Ahmad). Siku ya kiama haitakuja mpaka watu duni kabisa wawe watu wenye furaha kabisa (Tirmidh).

Kama inavyosomeka katika hadithi hizo kutakuwa na ongezeko la watu waovu ambapo wale wanaoonekana wakweli kumbe ni waongo na wale wanaoonekana waongo kumbe ndio wakweli. Hizi ni dalili za zama za mwisho.

Hadithi moja inabainisha kuwa kutakuwa na watu wachache sana wakweli na kiasi kidogo sana cha pesa kitakachopatikana kwa kuzingatia kanuni na sheria za dini yetu:

Katika zama za mwisho watu watakuwa wakifanya biashara lakini hakutakuwa na mtu yeyote mkweli (Bukhari na Muslim).

Ushahidi wa kweli utatupiliwa mbali na ushahidi wa uongo na kusingiziana ndivyo vitakavyoshamiri. Hii ni dalili nyingine ya zama za mwisho. Kwa hakika katika saa ya mwisho kutakuwa na ushahidi wa uongo na ufichaji wa ushahidi (Ahmed na Hakim).

Kutakuwa na shutuma za uongo za mambo machafu na masingiziano. (Tirmidh)

Kigezo pekee ambacho kwacho watu watapimwa ubora wao ni mali, hashima itategemea mtu ni tajiri kiasi gani:

Kabla ya saa ya mwisho kufika, kutakuwa na salamu maalumu kwa watu wa tabaka fulani. (Ahamad)

Hakutakuwa na hukumu mpaka pale salamu zitakapotolewa sio kwa watu bali kwa watu mahususi. (Mukhtasari Tazkira Khutub).

Inasemwa katika hadithi kuwa dalili nyingine ni kuvurugika kwa uhusiano wa kijamii baina ya watu:

Ni wale watu ambao mtu anawajuwa tu ndio watakaopewa salamu (Ahmad Diyal al diya’al Din al Kamushi Khanawi, Ramuzi al ahadithi)

Katika hadithi ifuatayo inaelezwa kuwa nafasi za kazi zitatolewa kwa watu wasio na sifa: Pale madaraka na mamlaka yatakapokwenda mikononi mwa watu wasio na sifa, basi hapo muisubiri ile saa (kiama). (Bukhari).

Dalili nyingine ya zama hizo itakuwa ni kuvunjika kwa uhusiano wa wanafamilia, marafiki, majirani na kuvurugika kwa jamii na maadili:

Mtu kutokuwa na mapenzi na Mama yake na kumfurusha Baba yake (Tirmidh).

Kwanza kutakuwa na sokomoko kwa mtu kuhusiana na familia yake, mali yake, nafsi yake, watoto wake, jirani zake (Bukhari na Muslimu).

Dalili nyingine ya zama za mwisho ni kuwa vijana watakuwa waasi na mapenzi na heshima kati ya vijana na wazee vitapungua:

Wakati wazee watakapokosa huruma kwa vijana, na wakati vijana watakapokosa heshima kwa wazee… Watoto watakapokuwa na jazba… Basi hapo hukumu ipo jirani.

(Imeripotiwa na Umar (r.a)).

Hadithi nyingine zinaonyesha dalili nyingine ya zama za mwisho kuwa talaka na idadi ya watoto wa nje ya ndoa vitaongezeka:

Talaka itakuwa ni jambo la kila siku (Allamah Safarini, Ahwal Yaum al Kiyama).

Kutakuwa na wingi wa watoto wa haramu (Al Muttaqi Al Hindi, Muntakhab Kanzul Ummaal).

Kwa kutenzwa na itikadi ya Ulahidi na mtazamo wa kidunia, watu wataikumbatia dunia kupindukia na wataghafilika na maisha ya akhera. Hii ni dalili nyingine ya zama za mwisho:

Uchoyo na Uroho utaongezeka. (Muslim, ibn Majah).

Wakati huo, watu wataiuza dini yao kwa kiasi kidogo cha maslahi ya dunia (Ahmad).

Hadithi nyingine inasema kuwa watu watalaaniana na kuapizana: Katika siku za mwisho kutakuwa na watu ambao pale wakutanapo hulaaniana na kutukanana badala ya kusabahiana (kwa salamu) (Allama) (Jalaludiin) Suyuti, Durre Mansouri).

Dalili nyingine ya zama hizo ni utesi na dharau kwa watu wengine:

Kutakuwa na wingi wa wasutaji, vizabizabina, Wambea, wagombanishaji, waamsha fitina na watu wenye dharau katika jamii. (Al Mutaqi Al Hindi, Muntakhab Kanzul Ummaal)

Dalili nyingine ya Kiama ni rushwa:

Udanganyifu na ulaghai yatakuwa mambo ya kawaida (Allama Safarini Ahwal Yaum al Qiyama)

Rushwa itaitwa zawadi na itaonekana kama halali tu: (Ammal Al diin al Qazwini, Mufid al ulumi wa Mubid al Humum).

Mtume (s.a.w) kasema, mauaji yataongezeka sana katika zama za mwisho: Kiama hakitasimama hadi pale mauaji yatakapozidi. (Bukhari)

Kukua kwa Sayansi na Teknolojia

Mtume Muhammad(saw), kama sote tujuavyo aliishi karne kumi na nane zilizopita. Kumbukumbu za Historia zinaonesha kuwa wakati Qur’an ilipofunuliwa jamii ya Waarabu haikuwa na teknolojia ya kuwawezesha kufanya tafiti za dunia au ulimwengu.

Kwa sababu hiyo kuna tofauti kubwa kati ya kiwango cha sayansi na Teknolojia cha wakati wa alioishi Mtume(s.a.w) na wakati huu wetu. Tofauti hii ilianza kuwa kubwa hasa zaidi mwanzoni mwa karne ya ishirini. Kielezeo cha wazi cha hilo ni mageuzi makubwa ya kiteknolojia yanayoonekana katika wakati wetu huu ambayo, hayakupata kuonekana sio tu wakati wa Mtume bali hata katika miongo michache iliyopita. Licha ya tofauti hiyo, bado katika karne ya saba Mtume(s.a.w) alizungumzia mambo mengi ya hakika juu ya maisha. Hapa tutaziangalia Hadithi zinazoelezea kiwango cha maarifa ya sayansi na Teknolojia katika zama za mwisho. Tutaona kuwa yale aliyoyabainisha Mtume(s.a.w) karne kumi na nne zilizopita yanadhihirika leo.

 
   
    
4 / total 5
You can read Harun Yahya's book Dalili Za Kiyama online, share it on social networks such as Facebook and Twitter, download it to your computer, use it in your homework and theses, and publish, copy or reproduce it on your own web sites or blogs without paying any copyright fee, so long as you acknowledge this site as the reference.
About this site | Tengeneza kurasa yako ya nyumbani | Add to favorites | RSS Feed
Mambo yote yanaweza kuynakiliwa, kuchapwa na kusambazwa kwa kurejea katika kurasa hii
(c) All publication rights of the personal photos of Mr. Adnan Oktar that are present in our website and in all other Harun Yahya works belong to Global Publication Ltd. Co. They cannot be used or published without prior consent even if used partially.
© 1994 Harun Yahya.www.harunyahya.com
page_top