Nani Mwenyezi Mungu?

SHUSHA KITABU

Download (DOC)
Maoni

SURA ZA KITABU

< <
4 / total: 5
Nani Mwenyezi Mungu? - Harun Yahya
Nani Mwenyezi Mungu?
   
Muujiza katika Uumbaji wakeSura ya Pili Mlipuko Mkubwa ulioumba Ulimwengu ( ‘the Big Bang’)

 

Kabla Mwenyezi Mungu hajaumba Ulimwengu, hapakuwepo umbile lenye jina hilo katika yale yaliyokwishaumbwa wakati huo. Tumeona pia kuwa ni Mwenyezi Mungu Aliyeumba kila kitu bila ya kuigiza mahali. Na tukaona kuwa Wanaadamu hawaumbi ila huunda, yaani huigiza katika vile ambavyo tayari Mwenyezi Mungu ameviumba. Mwenyezi Mungu Ameufanya Ulimwengu uwepo kutoka kwenye ombwe tupu. Je tukio hilo kubwa na la ajabu la kuumbwa Ulimwengu lilitokeaje.

Mabilioni ya miaka iliyopita, Ulimwengu ulikuwa kiduara kidogo. Sasa ni namna gani kijiduara hicho kilivyotokea na kupanuka kufikia Ulimwengu huu tulionao. Watu wanaweza kuvuta fikira juu ya mlipuko wa kitu chochote kile. Kwa mfano, muwindaji anajaribu kukiwinda kijidudu kidogo pengine mfano wa kunguni. Katika uwindaji huo akajaribu kutega bomu kwenye nyumba ili kuweza kukidhibiti kijidudu hicho. Katika utegaji huo, ifikiriwe ni nini kitatokea iwapo bomu hilo litalipuka. Ni wazi udongo utasambaa huku na kule, matofali kurushwa mbali, kwa hakika hapatapatikana kitu.Tunafahamu kuwa kabla ya mlipuko huo, matofali na udongo huo vilikuwa pamoja. Lakini baada ya bomu kulipuka vyote vitasambaa huko na kule mbali kabisa. Hivi ndivyo tunavyofahamu mlipuko wowote ule unapotokeya.

Mabilioni ya miaka huko nyuma kabisa, Ulimwengu huu ulifanyika baada ya mlipuko wa aina hiyo. Chembe chembe nyingi na ndogo sana zilitokea kutokana na mlipuko huo. Kama ilivyokuwa katika ile nyumba ya muwindaji, chembe chembe hizi zikasambaa huku na kule. Lakini la kustaajabisha kabisa, baada ya mlipuko na kusambaa huko, chembe hizo zikaanza kujikusanya na kuunda nyota, sayari mbali mbali na maumbile mengine makubwa yanayoonekana Ulimwenguni hivi sasa. Mlipuko ulioanzisha uumbaji wa Ulimwengu huu unajulikana na wajuzi wa elimu ya anga (wanaastromia) kama ‘The big Bang’ yaani Mlipuko Mkuu.

Ulimwengu haukutokea kwa bahati nasibu kama wasemavyo baadhi ya mabobwe ila umefanyika kutokana na mlipuko huu mkubwa ambao asili yake anaijua Mwenyezi Mungu. Ulimwengu huu unaojiendesha kwa utaratibu madhubuti tangu mizunguko ya chembe chembe hadi mizunguko ya sayari, unatokana na mitawanyiko ya chembe chembe na nguvu ambayo ilikadiriwa ijiwekee mpango maalumu kuanzia pale ulipotokea mlipuko mkubwa. Muda mlipuko huo ulipotokea, Ulimwengu ulianza kujiweka katika umbile duara lililokusanya mabilioni na mabilioni ya maumbile mfano wa hilo, ambao kwa pamoja ukiendelea kukua na kutanuka hadi leo.

1. Matrilioni ya miaka nyuma kabisa huko hakukuwa na Ulimwengu

2. Ulimwengu umetokea baada ya mlipuko wa umbile moja.

3. Baada ya mlipuko huo, idadi isiyohesabika ya maduara madogo yalitokea yakafanya Ulimwengu, wakati huo huo, maduara hayo yalianza kuelekea mbali ya pale yalipotokea huku yenyewe yakijikimbiza na kujiweka mbali mbali.

4. Duara la Ulimwengu huu limekuwa likipanuka mithili ya puto au mpira ujaao upepo kadiri maumbile yaliyomo yanavyosonga mbele zaidi.

Huu ni ushahidi wa uwezo wa Mwenyezi Mungu usio na ukomo. Hata wanaadamu wakijikusanya wote kwa pamoja, hawawezi kuumba Ulimwengu wala kuuhisi ukubwa wake. Hata kama vifaa vinavyopatikana katika ardhi hii vitakusanywa pamoja, mwanaadamu hataweza kuiga mfano wa mlipuko mkubwa sawa na ule wa Mlipuko Mkuu wa uumbaji. Uwezo wote ni wa Mwenyezi Mungu, Aliyeumba kila kitu. Inaeleweka kuwa mlipuko wowote ule hauwezi kutoa utaratibu na mpangilio wenye nidhamu nzuri bali kinyume chake ambapo husambaratisha na kuharibu kila kitu. Mlipuko huangamiza kila kilicho karibu yake. Mlipuko mkubwa kabisa wa bomu huharibu majengo na kuyafanya yasiwepo kabisa. Bomu lenye nguvu sana Ulimwenguni ni bomu la Atomiki. Bomu hili likilipuliwa mahali, huangamiza kabisa kila kitu. Kwa mfano bomu la Atimiki lilipoangushwa katika miji ya Hiroshima na Nagasaki Japan wakati wa vita kuu ya pili miaka ya 1939-1945, liliharibu kila kitu na kuwaacha vilema wale wote walionusurika na mlipuko huo wa bomu hilo baya. Hadi leo vizazi bado vinaathirika. Kubwa linalojitokeza hapa na lenye kustaajabisha ni jinsi mlipuko mkubwa kabisa, zaidi ya mara mabilioni ya bomu la Atomiki ulivyotokea. Mlipuko huo badala ya kuangamiza ulitengeneza, ulitoa matokeo tafauti na yale anayoyajua mwanaadamu kuhusiana na mlipuko wa aina yoyote. Mlipuko huo ulianzisha utaratibu madhubuti wa Ulimwengu. Hivyo, Ulimwengu huu tunaoujua uliopangwa vizuri mno kutuwezesha sisi kupata kila tunachokihitajia, unatokana na mlipuko huo mkubwa. Kwa nini Mlipuko huu uweke utaratibu huo madhubuti badala ya kuangamiza?

Kwa hakika ni Mwenyezi Mungu Aliyeumba Ulimwengu kutoka pasipokuwa kitu kwa njia hii ya mlipuko mkubwa. Na ni Yeye aliyeweka utaratibu madhubuti unaoendesha Ulimwengu kwa namna ya ajabu kabisa bila ya migongano. Hivyo, yeyote anayejaribu kutoa jawabu ya uumbaji wa Ulimwengu huu wa ajabu kinyume na hili, kwa hakika hana jawabu sahihi ila kujaribu kuwazuga Wanaadamu kwa manufaa yake binafsi ya kidunia. Kwa mfano, mtu anayedai Ulimwengu huu umetokea tu wenyewe na kujiweka hivyo ulivyo bila ya Muumba kwa kweli ni mwongo pengine hana akili timamu. Kusema kwamba Ulimwengu huu wenye utaratibu eti umetokea kwa bahati nasibu baada ya mlipuko wa awali, maneno hayo si ya akili kabisa. Ni nini kitakachotokea katika mchanga iwapo bomu litaangushwa mahali hapo? Kwa hakika chembe chembe za mchanga zitaruka na kusambaa ovyo huku na kule. Je, atatazamwaje yule ambaye atasema nyumba imezuka mtaani baada ya bomu kuangushwa? Kwa kweli ataonekana ni mtu wa ajabu sana. Vivyo hivyo huonekana ni kichaa mtu anayedai kuwa mpangilio na utaratibu madhubuti unaoendesha maumbile ya Ulimwengu umejifanyiza wenyewe!

Ipo mifano mingi ya ulingano, uhusiyano na uwiano madhubuti katika Ulimwengu huu. Mifano hiyo hatuwezi kuilinganisha na ile nyumba ya mtaani ambayo kamwe haiwezi kuzuka baada ya milipuko tunayoijua katika maisha yetu. Mwezi septemba tarehe 11, 2001 ndege ziliyalipua majengo ya kituo cha biashara cha Dunia(World Trade Centre) na Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon. Majengo hayo yaliharibiwa vibaya sana.

Katika kuhitimisha mada hii, tumalizie na kauli kwamba, ukamilifu, umadhubuti na mpangilio uliopo, unathibitisha ukweli kwamba Ulimwengu haukutokea au kujifanyiza wenyewe. Ulinganifu, uwiano na mpangilio wa kila kitu uliofungwa chini ya mtandao mmoja uitwao Ulimwengu ni alama ya busara isiyo na ukomo ya Mwenyezi Mungu Muumba. Ametukuka kweli kweli Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Ardhi na vyote vilivyomo.

Katika mada hii ya mlipuko ulioumbisha Ulimwengu:

-Tumejifunza kuwa kumbe Ulimwengu ulifanyika pasipo chochote kabla yake.

-Tumejifunza kuwa Aliyeasisi Mlipuko huo na hatimaye maumbile yaliyotokea baada ya mlipuko huo ni Mwenyezi Mungu.

-Tumejifunza kuwa wanaastronomia yaani wanaanga wanauita Mlipuko uliyoumba Ulimwengu kuwa ni Mlipuko Mkuu,

-Tumejifunza piya kuwa tangu mlipuko mkubwa, Ulimwengu unazidi kutanuka, ulianza mdogo, sasa umepanuka na kuwa mkubwa zaidi na bado unaendelea kuwa mkubwa zaidi na zaidi.

Mafundisho ya Qur’an juu ya kuumbwa Mbingu na Ardhi

Qur’an ni Kitabu Kitukufu cha Mwenyezi Mungu kilichoshusha kuwaongoza watu. Kitabu hiki ndicho kinachotoa maelezo sahihi kabisa juu ya mambo mbali mbali. Maelezo ya kitabu hiki ni sahihi kwa sababu kila neno lililomo limetoka kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe Muumbaji na Mjuzi wa kila kitu. Wakati Qur’an ikiteremshwa kwa Mtume Muhammad(s.a.w), Ulimwengu ulikuwa bado haujapiga hatua kubwa kisayansi na kitekinolojia. Kwa hiyo baadhi ya maelezo yaliyomo kwenye Qur’an hayakuweza kufahamika wala kufanyiwa utafiti. Hivi leo yamepatikana maendeleo makubwa ya kisayansi na kiteknolojia, hivyo mafundisho na maelezo mengi ya Qur’an yameweza kufahamika vizuri zaidi. Mfano mmojawapo ni kuwa Qur’an inatufahamisha kwamba Mbingu na Ardhi zilikuwa kitu kimoja, baadaye vikaachanishwa:

“Je hawaoni wale waliokufuru kuwa Mbingu na Ardhi vilikuwa kitu kimoja, kisha tukaviachanisha.”(Suratil Anbiyaa aya 30).

Kwanza, neno Mbingu linawakilisha anga na vilivyomo katika eneo hilo. Pili, Kauli kwamba, Mbingu na Ardhi vilikuwa kitu kimoja inafahamisha kwamba mwanzo maumbile yote ya Ulimwengu yalikuwa katika duara moja lililoshikamanishwa. Hatimaye kauli kwamba, “Tukaviachanisha” inaweka wazi kuwa duara hilo lililipuliwa na mlipuko uliyoliachanisha katika mapande mapande mengi. Chochote kinachopingana na mafundisho ya Qur’an si sahihi na cha kutupiliwa mbali.

Katika maelezo tuliyoyaona, tunafahamu kuwa Qur’an ndiyo inayotoa maelezo ya hakika zaidi kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa Ulimwengu na ndiye aliyeiteremsha Qur’an, kwa hiyo, Yeye anajua zaidi Alivyoumba na Alichokiumba.

Ulimwengu

Jua, Dunia na Mwezi ni maumbile tunayo yafahamu. Yapo maumbile mengine mengi katika anga la Ulimwengu huu ambayo hayaonekani. Anga lililo juu ya upeo wa macho lina nyota nyingi, sayari na vimondo vinavyoweza kuonekana katika picha ya kimawazo. Maumbile yanayoitwa ya angani yanajiweka pamoja chini ya mikusanyiko maalumu inayoitwa mifumo ya Jua ambayo nayo imekusanywa katika mikusanyiko mikubwa sana inayoitwa Magalaksi.

Maumbile ya angani ni makubwa mno. Ili mtu aweze kujua ukubwa wa maumbile hayo hana budi kujua kuwa sayari yetu hii ya Dunia ni katika maumbile madogo sana yakilinganishwa na maumbile mengine ya angani yaliyokusanywa na Ulimwengu. Hata hivyo, licha ya udogo wa umbile la Dunia katika maumbile yaliyoko angani, kwetu ni kubwa lenye kutosha kuwakusanya wanaadamu wote, wanyama, milima, viumbwa vingine vyote vinavyonekana na visivyoonekana (mfano majini) na kila kitu kisichoweza kukifikirika. Ametukuka Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu na Ardhi.

Sura ya Tatu Magalaksi

Mabilioni ya nyota zilizojikusanya pamoja, wataalamu wa mambo ya anga huita Magimba au galaksi. Tunafahamishwa ya kuwa, gimba au galaksi moja kubwa kabisa linakusanya nyota trilioni tatu. Na galaksi la ukubwa wa wastani linakusanya nyota biliyoni 200 mpaka 300, wakati ambapo galaksi ndogo kabisa lina mkusanyiko wa nyota bilioni 100. Bilioni moja ni kitu gani? Kuelewa bilioni ni kitu gani, iandikwe namba moja kisha iwekwe sifuri mbili, hiyo itakuwa 100. Ikiongezwa sifuri moja mbele ya 100, itakuwa elfu, 1,000. Ikiongezwa sifuri nyingine mbele ya 1000 hiyo ni elfu kumi, 10,000. Zikiongezwa sifuri mbili katika ile 10,000, itakuwa milioni moja, 1,000,000. Zikiongezwa sifuri tatu zaidi katika hiyo 1,000,000, hapa itakuwa imefikia bilioni moja, 1,000,000,000. Na mwisho, zikiwekwa sifuri mbili zaidi baada ya namba 1,000,000,000, hapa itakuwa imefikia bilioni mia moja(100,000,000,000) ambayo ni idadi ya nyota zilizokusanyika katika galaksi iliyo ndogo kabisa. Galaksi zenye idadi hii ya nyota, nazo ziko nyingi sana. Galaksi ambamo ulimo mfumo wetu wa jua ambayo wataalamu wa mambo ya anga wanaiita “milky way” ni miyongoni mwa galaksi zenye ukubwa wa wastani.

Mpaka hapa tumeweza kuuona ukubwa wa Ulimwengu. Ni Mwenyezi Mungu Aliyeumba Ulimwengu mkubwa kiasi hicho. Mwenyezi Mungu Ameumba Ulimwengu mkubwa sana ambao hapana yeyote katika wanaadamu awezaye kuudiriki katika fikira na mawazo yake. Ulimwengu ni mkubwa sana, wanaadamu ni vijiumbile vidogo sana katika maumbile yaliyomo, ni kwa sababu hii Mwenyezi Mungu anatuuliza ili tuweze kutafakari:

“Je, nyinyi ni wenye umbo la nguvu zaidi au Mbingu? Yeye amezijenga”(Surat Anaziat aya ya 27).

Pamoja na kuumba Ulimwengu mkubwa kiasi hicho ambao nao ni sehemu tu ya maumbile yake mengi, Mwenyezi Mungu amekizunguka kila kitu Alichokiumba anakijua vyema na Amekikadiria na Analijua kila linalopitikana humo pamoja na shughuli ya kila kitu. Katika Qur’an, Mwenyezi Mungu Anatufahamisha hili:

“Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyomo Mbinguni na Ardhini. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliyevizunguka vitu vyote (4:126).

Uwezo wa Mwenyezi Mungu usiyodirikika na usiyo na Ukomo unaelezwa piya katika aya ifuwatayo:

“Sema: kama mkificha yaliyomo vifuwani mwenu au mkiyadhirisha, Mwenyezi Mungu anayajuwa; anayajuwa yaliyomo Mbinguni na yaliyomo Ardhini; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye Uweza juu ya kila kitu”(Al Imran aya ya 29).

Kwa yale magalaksi yenye ukubwa wa wastani au makubwa zaidi, katikati yake kipo kiini ambacho wanaanga hukiita “galactic centre” yaani kitovu cha Galaktiki. Kuzunguka “kitovu cha Galaktiki”, ipo mikondo ambayo wanaanga huiita “mikono” ambayo inazunguka kwa kasi kubwa sana. Mikondo au “mikono” hiyo imefanyika kwa mikusanyiko ya nyota, hewa na mawingu ya vumbi. Yakiwa na “mikono” na viini vyake, magalaksi ndiyo maumbile makubwa kabisa katika maumbile ya anga. Mfumo wa jua, unakusanya Jua lenyewe ambalo ni nyota na sayari zake, Sayari nazo zina miyezi, kwa mfano sayari ya Dunia ina mwezi mmoja unaoonekana uking’ara wakati wa siku za mbaamwezi. Kisha hii mifumo ya jua nayo kwa mabiliyoni inaunda galaksi moja na kuna mabilioni ya magalaksi yenye ukubwa tafauti. Galaksi kubwa kabisa linakusanya nyota zaidi ya trilioni tatu, wakati ambapo galaksi ndogo inakusanya takribani nyota biliyoni 200.

Tuliyojifunza katika mada hii ni:

Kwanza, tumeona kuwa magalaksi ni mikusanyiko ya mabilioni na hata Matrilioni ya nyota,

Pili, tukaona pia kuwa yale magalaksi makubwa au yale yenye ukubwa wa wastani yana vitu sehemu ya kati vinavyoitwa viini yaani “vitovu vya galaktiki”.

Tatu, tumeona pia kuwa “mikono au mikondo ya galaksi imefanywa kwa nyota, hewa na wingu zito la vumbi”. Na tumeona mikono hii inakizunguka kiini cha galaksi kwa kasi kubwa sana.

Tuzingatie kuwa galaksi lenye nyota bilioni moja ni galaksi dogo sana, hapa haijatajwa kuwa kila nyota ya ukubwa wa wastani ni sawa na hili jua letu. Zipo nyota zilizo kubwa kulizidi jua letu hili. Mbali ya hivyo, katika nyota hizo kuna mfuatano wa sayari nyingine zenye ukubwa sawa au kuizidi Dunia yetu.

Mabilioni haya ya nyota yaliyojiweka katika utaratibu huo wa ajabu yalikutana pamoja kwa bahati nasibu? Nyota zingeweza kwa ghafla kujiunda zenyewe na kujiweka katika utaratibu huo ambao hauna migongano kati yake na maumbile mengine?

Kwa nini, kwa mfano, Dunia yetu haijapata kugongana na sayari nyingine au kugongana na huu mwezi unaoonekana kuwa jirani yake hasa ikizingatiwa kwamba Dunia na maumbile mengine ya anga yanazunguka kwa kasi kubwa sana. Haya yote yanadhihirisha kwamba yupo Muumbaji Ambaye ni Mwenyezi Mungu aliyepanga utaratibu huo wa maumbile na kuuweka katika mpango mzuri kabisa.

Mwenyezi Mungu huumba bila mfano

Wanaanga wamefanya kazi nzuri sana ya kuichunguza anga, hivyo wametupatia maelezo mazuri kabisa. Utafiti wa anga umesaidia sana kuonesha ujinga wa wale wanaodai kuwa Ulimwengu huu haukuumbwa ila umetokea tu wenyewe! Kutoka wapi? Hawana jibu. Kwa kweli uvumbuzi wa Wanaastronomia pia umeonesha kuwa Ulimwengu huu umeumbwa kama kilivyoumbwa kila kiumbe. Mtu wa kwanza kabisa kuubaini ukweli huo miongoni mwa Wanaanga tukiwaacha mitume na manabii wa Mwenyezi Mungu, inaelezwa kuwa ni Bwana mmoja aliyeitwa Edwin Hubble. Mtu huyo akitumia viona mbali vyenye nguvu sana, aliweza kushuhudia nyendo za nyota. Ilikuwa mwaka 1929 Mwanaanga huyo alipobaini hilo. Mwendo wa nyota alioushuhudia Bwana Hubble haukuwa huu wa kawaida tunaouona bali aliona jinsi nyota zinavyosonga mbele mbali zaidi na sisi. Zaidi ya hivyo aliweza kuona jinsi nyota moja inavyosonga mbele na kujiweka mbali zaidi na nyingine. Kwa hiyo kutokana na kusonga mbele zaidi kwa nyota, Ulimwengu wetu huu unaokusanya kila kitu unakua mkubwa zaidi kadiri siku zinavyosonga mbele. Ni miaka isiyozidi 100 tu iliyopita tangu watu walijue hilo. Wanasayansi wote wamebaini sasa kuwa kumbe nyota zinakimbiana na kujiweka mbali zaidi, na vile vile zimeendelea kuwa mbali zaidi na Dunia yetu. Mwendo huu wa nyota ni habari muhimu sana kwa mnasaba wa kuumbwa kwa Ulimwengu huu. Ukweli huu wa nyota kuendelea kusonga mbele kutoka mahali zilipokuwa, unadhihirisha kwamba, katika wakati fulani zote hizo zilikuwa kitu kimoja. Wanasayansi hao wanakadiria kwamba zaidi ya miaka bilioni 15 iliyopita maumbile yote yaliyomo Ulimwenguni, yalikuwa kitu kimoja katika umbile mithili ya ncha ya sindano. Kwa hiyo Ulimwengu wetu ulitokea kutokana na mlipuko wa umbile hilo moja.

Tulivyoviona katika mada yetu hii:

Kwanza, tumefahamu kuwa nyota zinakwenda daima.

Pili, kila nyota moja inajiweka mbali zaidi na nyingine na kujiweka mbali zaidi na Dunia yetu hii.

Tatu, iwapo itatokea zijirudishe nyuma zilikotoka tungaliweza kuona nyota hizo zikirudi hadi kufikia kuwa kitu kimoja.

Nne, hivi ndivyo itakavyoendelea hadi kufikia Ulimwengu wote kuwa kitu kimoja.

Tano, tukisonga mbele zaidi tutaona kuwa kitu hicho kimoja nacho kitafikia kutokuwepo. Kwa hiyo hii ina maana kuwa Ulimwengu wetu umetokea kwa kuumbwa na Mwenyezi Mungu. Ametukuka kweli kweli Muumba wa Ulimwengu na vyote.

Ni dhahiri kuwa sasa, itakuwa imeeleweka kuwa nini maana ya Ulimwengu kutokea pasipo kuwepo kitu. Maswali mepesi ya kujibu ni kama yafuatayo:

1. Ulikuwa na umri gani mwaka mmoja uliyopita?

Huenda jibu likawa ni miaka pungufu mwaka mmoja ya miaka ya sasa.

2. Iwapo mtu atahesabu miaka yake kinyumenyume mwaka mmoja mmoja atapata miaka mingapi mwisho wa kuhesabu huko?

Jibu ni mwaka mmoja tu. Mwaka mmoja tu baada ya mtu kuzaliwa alikuwa na umri wa mwaka mmoja. Na wakati anazaliwa hakuwa na umri wowote. Hapa tunaweza kusema alikuwa na umri sifuri.

3. Je mwaka mmoja kabla hajazaliwa alikuwa na umri gani? Alikuwa wapi wakati huwo? Jawabu hapa ni kwamba hakuwepo katika Ulimwengu huu.

4. Na mwili wa mtu ukirudishwa kinyumenyume utaonekana ukipungua kidogo kidogo na mwisho wake utakuwa umepotea kabisa. Kila mwaka mwili utapungua kuwa mdogo zaidi na zaidi, mpaka mwisho utarejea kuwa mtoto anayesimama dede, atarejea kutambaa, atarejea kukaa, atarejea katika uchanga wa kurusharusha miguu kitandani, ukirudi nyuma tena atakuwa hawezi hata kurusharusha hiyo miguu, amekuwa kichanga kisichojimudu, kidogodogo hatimaye atapotea kabisa katika Ulimwengu, watu watakuwa hawamjui.

Mtu amfikirie nduguye aliyekufa kabla ya yeye kuzaliwa, nduguye ambaye ameona picha yake. Mtu huyo hamjui kwa kuwa hakuwepo wakati yeye akiwepo na pengine awe aliishi katika nyumba hiyo hiyo anayoishi na labda alikuwa akilala kitanda hicho hicho alicholala. Jambo muhimu hapa si kwamba umri umerudi kinyumenyume bali waliokufa waliishi na kukamilisha muda wao kwa kadiri siku zilivyokuwa zikienda. Siku moja inaposonga mbele mtu ajue muda wake wa kuishi Duniani nao unapungua, yaani anaisogelea siku ya kufa kwake, kama ilivyokuwa siku ya kuzaliwa. Kwa hiyo hapakuwa na Ulimwengu kabla ya Mwenyezi Mungu hajauumba. Iwapo tutarudisha nyuma wakati, tutaona jinsi Ulimwengu unavyorudi hadi kuwa mchanga kama ulivyokuwa awali. Utaendelea kuwa mdogo, mdogo na mwisho utapotea kabisa, utakuwa haupo. Yote haya yanadhihirisha kuwa Ulimwengu umeumbwa.

Katika mada hii tumejifunza:

- Kuna maumbile ya anga yaitwayo Galaksi

- Kumbe haya magalaksi ni mkusanyiko wa mifumo ya nyota yenye umbile la mduara

- Wanajimu wanakadiria kuwepo kwa magalaksi zaidi ya bilioni 300

- Kumbe galaksi yetu ni katika zile zenye ukubwa wa wastani

- Kumbe yako magalaksi makubwa yenye kukusanya mifumo ya nyota zenye idadi kubwa isiyoweza kuhesabika

- Mfumo wetu wa jua uko katika kiini cha galaksi yetu ukizunguka na kukamilisha mzunguko wake kwa muda wa miaka bilioni 220.

Sura ya Nne Nyota zing’arazo Angani

Nyota na sayari, kama ilivyo kwa maumbile mengine, zimekuwepo kutokana na kutokuweko kufuwatia mkandamizo wa ujazo wa gesi na vumbi vumbi katika eneo ambalo Wanaastronomia huliita “nebulae”. Nebulae au unyenyezi, ikiwa ndicho chanzo cha maumbile ya angani, ina jukumu kubwa katika Ulimwengu huu. Nyota zilizo kwenye “Nebulae” hazina mwanga kama zilivyo nyota nyingine, kwa hiyo ni vigumu sana kuziona. Nyota zilizoko kwenye Nebulae huonekana pale tu zinapoakisi mwanga kutoka nyota nyingine. Pia tunaweza kuziona pale zinapopitiwa na vyanzo vyengine vya mwanga. Nyota zina joto, mwanga na nishati. Mbali ya zile nyota ndogo ndogo, zipo nyota kubwa sana. Katika kundi hilo la nyota kubwa, jua letu nalo ni nyota lakini halimo. Jua letu limezidiwa ukubwa na nyota nyingi. Nyota nazo huishi na kufa licha ya kwamba zenyewe hazina uhai. Kama ilivyo kwa viumbwa vyenye uhai, nyota nazo huzaliwa, huishi na hatimaye hufa. Nyota hutoka kwenye unyenyezi unaotokana na Nyota kubwa iliyoishi umri mrefu ambayo baadaye hulipuka na malighafi yote iliyotumika kuumbisha nyota hiyo husambaratika kule na huko. Kutokana na msambaratiko huo hutokea vipande vipande ambavyo huzaa viasili yaani elementi ambazo hujikusanya tena kuunda nyota ndogo na sayari. Wataalamu wanatwambia kuwa mabilioni ya miaka iliyopita, Jua letu na sayari zake, ambamo ndani yake mna hii Dunia yetu, limetokea kufuwatia mlipuko wa nyota kubwa inayotoka katika kundi la unyenyezi.

Baada ya kuona asili ya nyota, hebu sasa tuingie kuutazama kwa undani kidogo mfumo wetu wa jua.

Mfumo wa Jua

Katika mfumo wetu wa jua, kuna sayari nane(kabla ya watafiti wa anga kuiondolea Pluto ilifahamika ziko tisa) ambazo kwa ujumla zina miezi 54 na vijiumbile vingine vidogo visivyo idadi. Maumbile yote hayo yanazunguka umbile moja kubwa linaloitwa jua. Juwa likiwa kubwa zaidi linalozivuta sayari zote hizo, limewekwa katikati ya mfumo huu. Ndiyo maana mfumo huu unaitwa mfumo wa jua. Sayari zote nane ambazo ni sehemu ya mfumo wa jua, hujizungusha zenyewe wakati zikilizunguka jua katika utaratibu uliopangwa vizuri. Sayari tisa zilizo katika mfumo wa jua tukianza na ile iliyo jirani kabisa na juwa; ni Mekyure, Venasi, Duniya, Maazi, Jupita, Satuni, Uranasi na Neptuni ( kabla ya utafiti mpya ya mwisho ilikuwa Pluto). Katika mpangilio huo, Dunia yetu ni sayari ya tatu kutoka kwenye jua. Hata hivyo, hayo si kwamba ndiyo majina halisi ya sayari hizo bali yametolewa na wanajimu. Kila sayari iliyo katika mfumo wa jua ina hali tafauti na nyingine. Wakati halijoto katika baadhi ya sayari hizi iko juu sana kiasi cha kuweza kuyeyusha chuma, hali ya hewa katika sayari nyingine, ni ya barafu iliyozingira sayari yote. Sayari nyingine zimezingirwa na gesi. Zaidi ya hivyo baadhi ya sayari ni ndogo sana kama ulivyo mwezi. Kuna uhusiano mkubwa baina ya umbile kubwa na mfuasi wake. Kwa mfano, Dunia ni mfuasi wa jua na mwezi ni mfuasi wa Dunia. Hii ina maana kuwa Dunia inalizunguka jua na mwezi unaizunguka Dunia na kwa pamoja maumbile hayo mawili yanalizunguka jua bila ya kuachana. Kisha jua, sayari na miezi yake kwa pamoja yanazunguka kiini cha galaksi. Urari wa uvutano kati ya Dunia na mwezi ndiyo unaofanya sayari isitoke katika njia yake licha ya kuzunguka kwa kasi kubwa sana. Kwa mfano, iwapo mwezi utazunguka kwa kasi ndogo, utakuwa umeachwa na Dunia kwa kasi kubwa. Na ikitokea hali hii huu ndiyo utakuwa mwisho wa uhai katika Dunia. Kadhalika mwezi ukizunguka kwa kasi inayozidi Dunia utakuwa umekwenda mbali ya Dunia na hautakuwa tena mfuasi wa sayari hii.

Tumejifunza yafuatayo katika mada hii:

- Mfumo wa jua una sayari tisa, miongoni mwa hizo ni hii Dunia

- Pamoja na sayari hizo pia kuna miezi na maumbile madogo yasiyo na hisabu.

Umbile la Jua

Jua ndilo umbile kubwa zaidi katika maumbile yanayounda mfumo wa juwa. Jua ni kubwa mara 1000 ya ukubwa wa sayari ya jupita ambayo nayo ni kubwa kuliko Dunia kwa mara 318, yaani Dunia ziwe 318 ndiyo Jupita moja. Kwa hiyo Jua ni kubwa mara zaidi ya 300,000 kuliko Dunia. Yaani dunia ziwe laki tatu ndiyo ukubwa wa jua moja. Kipenyo chake tu ni kikubwa zaidi ya sayari hii ya dunia kwa mara zaidi ya 21. Jua lina joto kali lisilomithilika, vile vile lina gesi. Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya anga, Jua lina kipenyo chenye upana unaokadiriwa kuwa kilometa1, 400, 000, ambao ni mara 10 ya sayari ya Jupita. Upana wa kipenyo cha Jua ni mara nne ya umbali wa kutoka Duniyani hadi kwenye Mwezi. Mzingo wa umbile la Juwa una kilometa milioni nne. Kuweza kusafiri eneo lote hili kwa ndege yenye kasi ya mara tatu ya sauti, itachukuwa miyezi miwili kukamilisha safari hiyo! Karibu asilimia 99.9 ya chembe chembe za Jua ni haidrojeni na Hiliamu. Kila sekunde ya hali ya Juani hutokea milipuko mikubwa inayolizidi bomu la Atomu kwa mara matrilioni. Milipuko hiyo hutoa macheche makubwa yanalolizidi umbile la Duniya kwa zaidi ya mara 40 mpaka 50. Juwa ni mithili ya umbile la mpira ambalo usoni mwake hutowa mwanga na joto kali na mwanga unaoziangazia sayari zote zilizo katika mfumo wake. Kwa ajili hiyo, wanaanga wanakadiria kuwa kasi ya mzunguko wa Jua katika njia yake ni ya chini kulinganisha na kasi za sayari inazoziangaziya. Kasi ya Jua kuzunguka katika Obiti yake ni kilometa 220 kwa dakika, kadhalika kasi ya jua kujizungusha lenyewe katika muhimili wake ni ndogo, huchukuwa siku 24 za dunia kukamilisha mzunguko wake mmoja.

Kama jua lisingalikuwepo, katika Dunia yetu hii, muda wote kungekuwa ni usiku au kiza totoro na Dunia yote ingalikuwa imezingirwa na barafu. Na kubwa zaidi kusingalikuwa na uhai katika ardhi. Anga ni eneo ombwe lenye kiza kikubwa. Dunia yetu ni ya umbile linaloelea katika eneo ombwe tupu hilo, kubwa na lenye kiza, ambapo hakuna umbile lolote lililo jirani lenye kuimulika, kulipa joto na mwanga mbali ya jua. Mwanga unaotoka kwenye jua ni mkali sana, usiyoweza kutazamika na macho ya kawaida. Katika kipindi cha joto, miyonzi na miale ya juwa ni mikali zaidi. Hata hivyo, juwa lipo umbali mkubwa sana kutoka Duniani. Ni mamilioni ya kilometa na ni sehemu moja tu kati ya mionzi ya joto 2000 itolewayo na jua ambayo huweza kuifikia Dunia. Pamoja na umbali lilipo jua, hali ya hewa ya Dunia ni ya joto linalotosheleza.

Wanasayansi wamejaribu kufanya makadirio mbali mbali juu ya maumbile ya anga na hali iliyopo angani. Hata hivyo haiwezekani kufananisha halijoto ya juwa kwa kulinganisha na halijoto ya kitu chochote tunachokijuwa katika Dunia hii, ingawa joto lililopo katika kiini cha ndani kabisa ya dunia, linalizidi joto la uso wa juu wa Jua. Hali joto iliyopo kwenye kiini cha tabaka la ndani kabisa ya Dunia ni nyuzi za sentigredi 7,500(13,500 F). Halijoto iliyopo katika uso wa jua ni nyuzi za Sentigredi 6000 (au faranihait 11, 000), katika kiini cha kati cha tabaka la ndani la umbile la jua halijoto hufikia hadi nyuzi za sentigredi 12,000,000(21,000,000 F). Hakuna joto la kitu chochote kijulikanacho katika maisha haya, linaloweza kulinganishwa na joto hili. Mtu hushindwa kuvumilia kuweka kidole chake katika maji yachemkayo sana ambayo joto lake halizidi nyuzi za Sentigredi 50 tu (120 F). Hata katika kipindi cha joto sana, halijoto ya Dunia hufikia nyuzi 40 hadi 50(105-120 F) tu. Mfano huu unaonesha jinsi Mwenyezi Mungu alivyokadiria umbali kati ya Dunia na Jua kwa namna ya ajabu kabisa. Iwapo juwa lingalikuwa karibu kidogo na Dunia yetu, kila kitu kingaliyeyuka, kukauka kabisa na kubaki majivu. Na kama Dunia yetu ingalikuwa mbali zaidi ya hapa ilipo, kila kitu kingaliganda na kukauka kwa barafu. Na kwa hakika uhai usingalikuwepo. Maeneo ya pola ambayo hupokea mwanga na joto dogo kutoka kwenye jua yanazingirwa na barafu kali. Eneo la kati ya Dunia au lenye kupitiwa msitari wa kufikirika, unaogawa Dunia sehemu mbili, hufikiwa na miyonzi mingi ya juwa, lina joto sana. Mwenyezi Mungu Ameumba maeneo haya kama mfano kwetu. Maeneo mengine yana hali inayoimarisha uhai wa mwanaadamu. Hii inaonesha jinsi Rehema ya Mwenyezi Mungu ilivyo juu yetu. Hiyo ni kwa sababu, kama Mwenyezi Mungu asingaliuweka umbali huu kati ya Jua na Dunia ingekuwa vigumu kwa Mwanadamu kuweza kuishi. Na kwa hakika kusingekuwa na uhai ila kwa kutaka Mwenyezi Mungu.

Kama ilivyoelezwa awali, Mwenyezi Mungu Ameumba Juwa na Mwezi ili kuwezesha maisha ya Wanadamu katika sayari hii. Katika Qur’an Mwenyezi Mungu Anatufahamisha kwamba Jua na Mwezi vinakwenda na kuogelea kwa Amri yake:

“Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziinua Mbingu bila ya nguzo mnazoziona hivi. Kisha Akatawala juu ya Arshi. Na Akaliitisha juwa na mwezi. Na kila kimoja kinaendeleya mpaka muda uliowekwa. Yeye ndiye anayeliendesha kila jambo. Anazipambanuwa aya hivi ili mpate yakini ya kukutana na Mola wenu”. (13:2).

Katika mada hii tumeona:

- Umbile la jua, ukubwa na joto lake lisilo na mfano.

- Joto la jua ni kali mno kuweza kuyeyusha au kugeuza hata jivu kuwa na hali nyingine tafauti.

- Umbali kati ya jua na sayari iliyo jirani yake umeifanya sayari hiyo kuitwa sayari nyekundu kutokana na mwanga unaotoka kwenye jua.

-Ukali wa jua ni wa kutisha kwa sababu sayari yetu hii ya Dunia iko mbali sana na jua lakini ina joto ambalo mahali pengine huweza kuathiri.

Nguvu ya uvutano ya jua

Nguvu ya uvutano ya jua inazivuta sayari zote zilizo katika mfumo wa juwa. Maumbile ya angani yasiyo na idadi yanaogelea katika utaratibu uliopangwa vyema bila ya mgongano. Mwenyezi Mungu ameweka njia maalumu zinazopitiwa na maumbile hayo ambazo wanajimu yaani wataalamu wa mambo ya anga huziita Obiti. Obiti ni njiya ambazo sayari na nyota yenye mkia hupita katika mwendo wao wa kulizunguka jua. Hakuna sayari inayoweza kupita nnje ya Obiti yake kuelekeya mahali pengine angani. Hiyo ni kwa sababu sayari zote zipo chini ya milki ya nguvu ya uvutano ya juwa. Dunia yetu inazunguka katika njia yake kwa kasi ya kilometa 108, 000(maili 70,000) kwa saa kulizunguka jua. Mifano michache yaweza kusaidia kuelewa kasi hii: Kasi ya mwisho kabisa ya gari ni kilometa 200(maili 125) kwa saa. Hii ina maana kwamba kasi ya Dunia kujizungusha yenyewe wakati ikilizunguka jua ni mara 540 zaidi ya kasi ya gari. Risasi inakwenda kasi ya kilometa 1,800 (maili 1,100) kwa saa. Kasi ya Dunia kulizunguka jua ni mara 60 ya kasi ya risasi.

Kwa sababu ya kasi hii kubwa ya mwendo wa Dunia, nguvu ya uvutano ya juwa ni muhimu sana. Iwapo jua litalegeza nguvu hiyo ya uvutano, wanaadamu watajikuta wamerushwa mbali nje ya Dunia wakiachwa wakiogelea katika anga kama ziogeleavyo sayari na maumbile mengine ya anga hali ambayo itafanya uhai usiwepo tena Duniani. Kwa upande mwingine, iwapo jua litaongeza zaidi nguvu ya uvutano, Dunia yetu pia itavutwa jirani na jua na itaungua tiki tiki pamoja na vilivyomo. Na kwa hivyo itakuwa mwisho wa uhai katika Dunia. Zaidi ya hivyo, nguvu ya uvutano ya jua vile vile hudhibiti sayari ziendelee kubaki kwenye njia zake (Obiti), zisitoke nje ya hapo na hivyo kusababisha kugongana zenyewe. Hivi jua bila ya uumbaji uliotukuka wa Mwenyezi Mungu lingeweza lenyewe peke yake kuzivuta na kuzimiliki sayari zake kwa nguvu yake ya uvutano?

Jibu la swali hilo li wazi. Ni Muumba, Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu na uwezo usiyo na mipaka, Ambaye Ameumba na kuweka vipimo vinavyoendelea kuweka urari asilia wa maumbile. Mbali ya hilo, si jua pekee lenye nguvu inayovuta bali Sayari zilizomo kwenye mfumo wa jua letu nazo kadhalika zina nguvu za uvutano . Kwa mfano, nguvu ya uvutano ya Dunia inauvuta na kuudhibiti mwezi. Kwa sababu ya nguvu hii ya uvutano, mwezi umedhibitiwa kukaa umbali maalumu. Kwa namna hii, Dunia haiwezi kugongana na mwezi. Bila shaka, yote haya hayawezi kujifanyiza yenyewe bali ni Muumba aliyeweka mpango huu na kuudhibiti kwa sheria na kanuni za kimaumbile alizoziweka. Ni Mwenyezi Mungu Anayeuzuia mwezi usianguke juu ya Dunia na si Mwezi unaojizuia kwa kujiwekea wenyewe kanuni hizo! Ipo nguvu nyingine inayovuta ifananayo na hiyo ya Jua, iliyowekwa kuwawezesha Wanaadamu kuishi. Hiyo ni nguvu iliyomo ndani ya ardhi inayowapa wanaadamu uzito. Nguvu ya uvutano inayowapa uzito, huwafanya wabaki katika hii Ardhi, kuwawezesha kutembea na kukimbia kwa urahisi bila ya kutoka katika eneo la Ardhi.

Hebu tujaaliye, tumeshika mipira mikononi mwetu; kisha tuwe tumeiyachia mipira hiyo. Tujiulize nini kitatokea? Kwa hakika mipira hiyo itaanguka chini kwa sababu kuna uvutano unaoelekeza kila kitu kurejea chini katika ardhi. Lakini, ukitoka nje ya duara ya sayari hii ya Dunia ukiwa umeshika mpira huo kisha ukauwachia, hautaanguka chini bali utaelea kwa kuwa kuna nguvu ndogo ya uvutano. Kuwepo kwa nguvu ya uvutano ndani ya ardhi ni muhimu sana kwetu. Lipo jambo jengine muhimu la kuzingatiya. Nguvu ya uvutano haitakiwi ipungue au izidi hii iliyopo. Iwapo itakuwa ndogo, wanaadamu watakuwa wakitembea hewani na hawataweza kuigusa Ardhi kwa miguu yao. Hawataweza kutembea wanavyotaka, watakuwa wakienda kwa kurukaruka kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Vivyo hivyo, nguvu ya uvutano ya Dunia ingalikuwa kubwa zaidi ya hii, watu wasingaliweza kutembea kwa sababu wangaligandamizwa chini Ardhini. Kitu ambacho wangeweza kufanya pengine, ni kusota na kujiburuza kwenye udongo. Hayo yote hayawezi kutokea ila ni kwa sababu ya Rehema ya Mwenyezi Mungu, Muumba ambaye Ameumba na kukadiria nguvu zinazowezesha maisha yawezekane katika Dunia hii. Ili kulifahamu vyema somo hili, hebu tuchukuwe mfano ufuatao: Mwezi, kama Dunia, una nguvu ya uvutano. Hata hivyo, nguvu hii ya mwezi ni ndogo kuliko ile ya Dunia. Kwa sababu hiyo haiwezekani kwa mwanaadamu kuishi katika mwezi. Katika ile picha ya Apollo 11, wanaanga waliotua mwezini mwaka 1969, wanaonekana jinsi wanavyotembea kwa kunyata na kurukaruka wakilazimika kutembea kwa hatua ndogo. Iliwalazimu wanaanga wale kutembea hatuwa ndogo sana tena kwa taratibu sana ili wasiruke ruke zaidi. Ni vipi Wanaadamu wangaliweza kuishi katika mazingira hayo bila ya idhini ya Mwenyezi Mungu?

Katika mada hii tumeona:

- Nguvu za uvutano kati ya jua na sayari na kati ya sayari na miezi jinsi zinavyofanya mpango wa maumbile hayo uende kama ulivyopangwa bila ya kutokeya mgongano wowote.

- Ni Mwenyezi Mungu aliyeweka urari asilia wa maumbile ya anga unaoyawezesha kuogelea katika Obiti zao bila ya kwenda mbali ya hapo.

- Sayari ni maumbile ya anga yanayojizungusha yenyewe katika mihimili yake na wakati huo huo kuzunguka nyota kubwa zilizo katikati yao.

- Juwa ni nyota kubwa inayozungukwa na sayari pamoja na jumla ya miezi zaidi ya 54 iliyopo katika sayari zote zilizomo katika mfumo wetu wa jua.


    
4 / total 5
You can read Harun Yahya's book Nani Mwenyezi Mungu? online, share it on social networks such as Facebook and Twitter, download it to your computer, use it in your homework and theses, and publish, copy or reproduce it on your own web sites or blogs without paying any copyright fee, so long as you acknowledge this site as the reference.
About this site | Tengeneza kurasa yako ya nyumbani | Add to favorites | RSS Feed
Mambo yote yanaweza kuynakiliwa, kuchapwa na kusambazwa kwa kurejea katika kurasa hii
(c) All publication rights of the personal photos of Mr. Adnan Oktar that are present in our website and in all other Harun Yahya works belong to Global Publication Ltd. Co. They cannot be used or published without prior consent even if used partially.
© 1994 Harun Yahya.www.harunyahya.com
page_top