Kufa Ufufuko Jahannam

SHUSHA KITABU

Download (DOC)
Maoni

SURA ZA KITABU

< <
3 / total: 8
KUFA UFUFUKO JAHANNAM - Harun Yahya
KUFA UFUFUKO JAHANNAM
   IMANI ZA KISHIRIKINA NA HAKIKA ZA UKWELI

Katika zama zote za historia, mwanadamu ameweza kufanikiwa kukabiliana na ama changamoto au tashiwishi mbalimbali za kimaisha. Lakini kifo kimebakia ni tatizo kwake na jambo lisiloepukika. Kila mmoja aliyewahi kuwepo katika dunia, bila kujali ni lini, alihitimisha maisha yake kwa kifo. Mwanadamu huishi hadi siku fulani kisha anakufa. Wengine hufa bado wangali wachanga, wengine hupitia hatua zote za maisha na kufariki dunia katika umri mrefu. Hakuna chochote anachomiliki mwanadamu, si vitu vyake, bahati, cheo, uwezo, watoto, ujasiri au mvuto wake unaoweza kuepusha kifo.

Bila ya upendeleo, wanadamu wote hawana cha kuwasaidia kuweza kuwaepusha na kifo na hali itabakia hivyo. Wengi katika watu hujizuilia kufikiria kifo. Haiwapambanukii kwao kwamba mwisho huu yaani kifo lazima siku moja utawakuta tu. Wanajenga fikra za imani za kishirikina kwamba, kama watajizuilia na fikra juu ya kifo, basi itakuwa kinga kwao juu ya kifo. Yanapofanyika majadiliano ya kila siku, wanaoleta mjadala juu ya kifo huzuiliwa na wenzao. Mwingine mwenye kuanza mazungumzo juu ya kifo, kwa kukusudia au bila kukusudia, na kurejea dalili za Mwenyezi Mungu, japo kwa kiwango kidogo tu, huibua wingu zito la kutokuwa na mwelekeo uliotanda katika macho ya watu.

Hata hivyo, wengi katika watu wanaofanya udanganyifu ndio njia yao ya maisha, hukosa utulivu wakati ukweli huu 'unaowachukiza' unapowasilishwa kwao.

Bado, jinsi wanavyojitahidi kuweka fikra zao juu ya kifo, ndivyo hivyo hivyo kifo nacho kinavyozidi kuwanyemelea karibu. Hali yao hiyo ya kutawaliwa na shetani (kumfanya ndiye mlinzi wao) kutadhihirisha ni kwa kiwango gani watataharuki na kutishwa na hali ngumu watakayokabiliana nayo wakati wa kifo, siku ya hukumu na katika adhabu ya milele.

Muda hufukuzana na mwanadamu. Je, mwanadamu amewahi kusikia mtu aliyezuia asizeeke au kufa? Au, mwanadamu anamjua mtu yeyote ambaye hatakufa? Hili si rahisi kupatikana. Haiwezi kupatikana kwa sababu mwanadamu hana ushawishi wa namna yoyote ile kuhusu mwili wake au maisha yake. Kwamba yeye mwenyewe hana maamuzi juu ya hata kuzaliwa kwake, kufanya jambo hili liwe wazi zaidi. Ushahidi mwingine ni pale mwanadamu anapokata tamaa katika kukabili kifo. Mmiliki wa uhai ndiye aliyempa mwanadamu uhai huo. Na hivyo pindi akipenda, huuchukua kwake. Mwenyezi Mungu, mmiliki wa uhai, anamfahamisha mwanadamu juu ya hili katika aya aliyomfunulia Mtume wake:

"Nasi hatukumfanya mwanadamu yeyote wa kabla yako aishi milele. Basi kama ukifa wewe, wao wataishi milele? (Al-Anbiyaa:34)

Kwa wakati huu, wapo mamilioni ya watu waishio ulimwengu mzima. Kutokana na hili tunahitimisha kwamba, idadi ya watu isiyo na hesabu wamekuwepo na kutoweka tangu kuumbwa mwanadamu wa kwanza kutokea duniani. Wote wamekufa bila ubaguzi. Kifo ni mwisho ulio hakika kabisa; kwa watu waliotangulia na wale ambao kwa sasa wako hai. Hakuna hata mmoja anayeweza kuepuka kifo. Kama Qur'an inavyothibitisha hili:

'Kila nafsi itaonja mauti. Na bila shaka mtalipwa ujira wenu kamili kamili siku ya kiama. Na aliyewekwa mbali na moto na kuingizwa Peponi, basi amefuzu. Na maisha ya dunia hii si kitu ila ni starehe idanganyayo. (Al-Imraan:185)

KUDHANIA KIFO NI JAMBO LA BAHATI NASIBU AU BAHATI MBAYA

Kifo hakitokei kwa bahati nasibu. Kama ilivyo kwa matukio mengine, hutokana na mpango wa Mwenyezi Mungu. Kama ilivyo kuwa tarehe ya kuzaliwa mtu imekwisha pangwa, ndivyo hivyo hivyo kwa tarehe na sekunde atakayokufa.

Mwanadamu anaharakishia kwenye mwisho wake, nyuma zikipita saa na dakika alizopewa kuishi. Kifo cha kila mmoja, mahali kitakapotokea na wakati, na pia namna mtu atakavyokufa, vyote vipo katika Qadar ya Mwenyezi Mungu, (au Mpango wa Mwenyezi Mungu).

Mbali na hili, watu wengi hudhania kuwa kifo ndio hatua ya mwisho katika mlolongo wa matukio, wakati ambapo sababu halisi anayezijua ni Mwenyezi Mungu peke yake. Kila uchao, habari za kifo katika vyombo vya habari kama magazeti, redio na runinga ndizo zinazotawala. Baada ya kusikiliza na kusoma taarifa hizi, pengine utasikia hoja za baadhi ya watu wajinga wakisema:

"Angenusurika kama tahadhari muhimu zingechukuliwa"

"Asingekufa kama hili na lile lingefanyika."

Hakuna sekunde inayoongezwa au kupunguzwa katika maisha ya mtu zaidi ya muda ule alioandikiwa na Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, watu ambao wako mbali na ufahamu utokanao na imani, hukitazama kifo kama moja ya matukio ya bahati nasibu. Ndani ya Qur'an, Mwenyezi Mungu ametahadharisha waumini dhidi ya hoja iliyopindishwa namna hii ambayo kimsingi ni maalum kwa Makafiri:

"Enyi Mlioamini msiwe kama wale waliokufuru na wakasema juu ya ndugu zao waliposafiri katika nchi au walipopigana: 'Kama wangalikuwa kwetu wasingalikufa wala wasingaliuwawa. Mwenyezi Mungu atawafanya wawe ni wenye kujutia maneno yao hayo katika nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuhuisha na kufisha. Na Mwenyezi Mungu anaona yote mnayoyatenda. (Al-Imraan: 156).

Kudhania kuwa kifo ni bahati nasibu ni ujinga ulio wazi. Kama aya hapo juu inavyobainisha, hili husababisha kuporomoka kwa imani na matatizo yasiyozuilika kwa mwanadamu.

Kwa makafiri au wale wasio na imani kwa mtazamo wa Qur'an, suala la kuondokewa na ndugu au yule unayempenda ni sababu tosha ya kukata tamaa na huzuni kubwa katika nafsi yake. Kitendo cha kukioanisha kifo na mkosi au balaa, watu hao hufikiri kuwa ni njia mbadala ya kukiepuka kifo.

Haya ni maamuzi ambayo hatima yake ni kuwafikishia majuto na maangamizi. Maangamizi na majuto haya si lolote zaidi ya kule kutokuamini kwake. Hata hivyo kinyume na mtazamo wa makafiri ulioainishwa hapo juu, ukweli ni kwamba kifo hakisababishwi na ajali, wala maradhi wala kingine chochote. Kwa hakika ni Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba sababu zote hizi. Pindi muda uliowekwa kwa ajili yetu unapokamilika, maisha yetu hukoma kwa kupitia hizi sababu zinazoonekana kwa nje kuwa ndio chanzo hasa. Wakati huo huo, hakuna kinga yoyote ya kimaada inayoweza kumuokoa yeyote kutoka katika kifo na kuleta uhai mwingine. Mwenyezi Mungu anaonesha kanuni hii yake katika aya ifuatayo:

'Na nafsi yoyote haitaweza kufa ila kwa amri ya Mwenyezi Mungu kwa ajali iliyopangwa... (Al-Imraan:145).

Muumini ana hakika juu ya maisha ya dunia hii kuwa ni ya muda tu. Anajua kuwa Mwenyezi Mungu, aliyemzawadia kila jema linalopatikana hapa Ulimwenguni, siku moja ataichukuwa roho yake katika mahali na muda alioupanga ili amuhesabu matendo yake. Hata hivyo kwa kuwa katika uhai wake wote ametumia neema za Mwenyezi Mungu, hakuwa ni mwenye kuhofia kifo. Mtume Muhammad (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) aliurejea mwenendo huu mwema katika moja ya dua zake kwa kusema:-

'Hakika Swala yangu, kujitoa kwangu Muhanga, uhai wangu, kifo changu ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Bwana wa Ulimwengu.'

Hadithi hii ilisimuliwa na Jabir bin Abdallah na kunukuliwa na At-Tirmidh, hadith namba 262.

KUELEWEKA VIBAYA KWA QADAR

Watu wengi wameendekeza mitazamo potofu kuhusu Qadar, hasa kama suala lililoko mbele yao ni kifo. Mawazo yasiyo na mashiko kama kusema 'Mtu anaweza kuishinda qadar yake' au 'mtu anaweza kubadili yaliyomo katika Qadar' yameenea mno. Kuchukulia matazamio yao na dhana zao kuwa ni Qadar, watu ambao si werevu na ambao ni wajinga huamini kuwa ni Qadar ndiyo iliyobadilika pindi tukio linapokwenda kinyume na matarajio yao au utabiri wao.

Wanadhani bila ya kutumia busara na kutenda kama vile wamesoma Qadar kabla na kwamba matukio hayakwenda sawa na vile walivyosoma. Upindishaji na kukosekana kwa mfuatano mzuri kiasi hicho, ni matokeo ya uelewa finyu unaokabili utoshelezaji wa ufahamu juu ya Qadar.

Qadar ni mpango wa Mwenyezi Mungu unaohusu uumbaji kamili wa matukio yote yaliyopita na yanayokuja bila ya kuwekewa mipaka ya muda. Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba dhana ya muda na nafasi bila ya maada yoyote, ndiye anayemiliki wakati na nafasi na hawekewi pingamizi na chochote kati ya hiyo. Mfuatano wa matukio ambayo yametokea kabla au yatakayotokea mbeleni, ni hatua kwa hatua, yamepangwa na kuumbwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba muda, hivyo hufungwi nao. Vivyohivyo, kwamba anafuata matukio ambayo yeye mwenyewe ameyaumba pamoja na yule anayeyatenda haikubaliki kiakili. Kwa mnasaba huu, hakuna haja ya kusema kwamba Mwenyezi Mungu hasubiri kuona namna tukio litakavyokamilika. Katika utaratibu wake vyote mwanzo na mwisho wa tukio viko wazi mno. Hali kadhalika, hapana shaka kwamba ni wapi tukio hili lipo katika mfumo mzima wa umilele. Kila kitu kimeshafanyika na kimekwisha. Hii ni sura ya picha katika mkanda wa filamu kama ambavyo picha haiathiri chochote katika mkanda na kumbadili, vivyo hivyo mwanadamu ambaye ana nafasi yake katika utendaji wa maisha hawezi kubadili mlolongo wa matukio uliorekodiwa na kuhifadhiwa katika mkanda wa Qadar. Wanadamu hawana lolote wanaloweza kubadili katika Qadar. Kinyume chake, ni Qadar ndiyo kigezo katika maisha ya watu.

Mwanadamu, ambaye ni mmoja katika mpango mzima wa Mwenyezi Mungu, kamwe hawezi kutoka na kuwa nje ya mpango huo. Si tu kwamba hawezi kuibadili Qadar, vivyo hivyo hawezi kwenda nje ya mipaka iliyo katika Qadar. Kwa uelewa mzuri zaidi; mtu anaweza kuoanisha baina ya mtu na muigizaji katika mkanda. Muigizaji hawezi kujitoa nje ya mkanda, na kuwa mwigizaji halisi na hivyo kuanza kubadili katika filamu kwa kuondoa matukio ambayo hayampendezi au kwa kuongeza matukio mapya. Kwa hakika hili litakuwa ni wazo ambalo halikubaliki kiakili.

Kwa mtazamo huo, dhana kwamba mtu anaweza kuishinda Qadar au kupindisha mfuatano wa matukio yaliyo katika Qadar ni upuuzi mtupu. Yeyote anayesema 'Nimeishinda Qadar' hana zaidi ya kujidanganya mwenyewe na ukweli kwamba amefanya hivyo ndio Qadari iliyoko juu yake. Elimu na taaluma ya Qadari iko nje ya ufahamu wa Mwanaadamu.

Mtu anaweza kuwa mahututi kwa siku kadhaa. Inaonesha kwamba yaelekea hataweza kurejea tena na kuwa buheri wa afya. Hata hivyo, pindi atakapokuwa amepona, hii haina maana kwamba 'ameishinda hatima yake, au 'madaktari wamebadili hatima yake'. Kwa wepesi kabisa hii inaashiria kwamba muda wake wa kuishi bado haujakwisha. Kurejea kwake katika afya njema si chochote zaidi ya dalili kuwa hawezi kukwepa mwisho wake, yaani kifo. Mwisho wake ni sawa na wanadamu wengine mbele ya mpango wa Mwenyezi Mungu:-

"Na mwenye kupewa umri hapewi umri zaidi wala hapunguziwi umri wake kuliko ule ulioandikwa katika kitabu. Bali haya ni sahali kwa Mwenyezi Mungu (Al-Fatir:11)

Mtume Muhammad (SAW) katika kitabu cha Imam Muslim - Sahih Muslim hadithi namba 6438 amesema yafuatayo kwa Muumin ambaye amemuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amuwezeshe kunufaika kutoka kwa ampendae. 'Umeomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu juu ya umri ambao tayari umekwishapungua, na urefu wa masiku ambayo tayari yako kwenye mpango na kuendeleza fungu ambalo fungu lako tayari limekwisha kukadiriwa. Mwenyezi Mungu hafanyi chochote ama kukatisha au kukichelewesha kwa muda ambao umekwisha kadiriwa.' Hali kama hizo ndiyo njia ambazo Mwenyezi Mungu anamdhihirishia mwanadamu elimu yake isiyo na ukomo, busara zake, aina na rehema zilizorithishwa viumbe vyake na pia njia anayotumia kumjaribu Mwanadamu. Aina kama hizo za mifano iliyotolewa hapo juu huongeza kuridhishwa kwake, kustaajabu na hali ya kipekee katika Imani za waja wake.

Kwa upande wa makafiri, wao kinachoongezeka ni hisia kati ya mashaka, kukerwa na kurejea nyuma katika maovu. Kinyume na matarajio yao yaliyojengeka katika ujinga wa kiakili hupelekwa watu hawa wawe na fikira za kuwa waasi zaidi kwa Mwenyezi Mungu. Wakati huo huo, ufahamu wa waumini juu ya kundi hili linaloendelea kubobea katika maasi, wao huzidi kumshukuru Mola wao kwa kuwaridhia kuwa na Imani na busara, vitu ambavyo huwafanya wawe bora kuliko makafiri.

Kutokana na 'kipande cha busara' kilichopokelewa toka kwa kundi la wenye shaka juu ya Qadar, kifo cha mtu mwenye umri wa miaka 80 na zaidi ni 'Qadar' lakini anayekufa akiwa bado mtoto mchanga au mwenye umri wa kati ni kitendo cha kuhuzunisha. Kifo kitahesabika ni kitendo cha kawaida kwao wao kama kitawafikiana na matakwa yao. Kwa mfano, mtu anapougua kwa muda mrefu, kifo kinaonekana kukubalika. Lakini kama mtu ameugua ghafla au kutokana na ajali mtu akafariki dunia, hilo ni janga lisilotegemewa. Ndio maana watu wengi hukutwa na kifo hali ya kuwa wanakichukia huku wakidhihirisha uasi wao kwa Mwenyezi Mungu.

Tabia hii ni wazi kwamba muhusika amekosa imani juu ya Qadari na hivyo juu ya Mwenyezi Mungu. Hao wanaonawirisha fikra hizo vichwani mwao wameandaliwa maisha ya fedheha na shida katika maisha haya. Kwa hakika huu ni mwanzo tu wa adhabu ya milele ambayo ni matokeo ya kukosa imani.

IMANI KUWA ROHO HUENDA KUISHI KWENYE MWILI MWINGINE BAADA YA KIFO

Moja kati ya imani potofu inayoshikiliwa na watu kuhusu kifo ni ile inayodai kuwa 'Kuna uwezekano wa roho ya mtu kupachikwa katika mwili mwingine na kuendelea kuishi hapa hapa duniani. Tafsiri ya maneno hayo ni kuwa kifo kinapomkabili mtu, mwili ndio hufa, lakini roho yake ama huhamishiwa katika mwili mwingi au huzaliwa upya katika mwili mwingine kwa nembo tofauti kwa wakati na mahali pengine. Hivi karibuni, hali hii imekuwa mkakati unaovutia wengi miongoni mwa makafiri na wafuasi wa Imani za Kishirikina.

Katika mtazamo wa kitaalam, sababu zinazochukuliwa kuwa ndio hasa zinazozusha imani hizi za kishirikina kuungwa mkono - (bila ya kuwa na hoja madhubuti) ni ile hali ya wasioamini wanayoifanyia kazi. Kwa kukosa kwao imani juu ya Akhera, watu wanahofia kurejeshwa na kuwa si chochote baada ya kifo. Wale wenye imani dhaifu, kwa upande mwingine, hukosa utulivu juu ya fikra kwamba kuna kupelekwa motoni kwani wanafahamu, au walau, wanafikiria kwamba kutokana na Mwenyezi Mungu alivyokuwa muadilifu, wao hawana makazi mengine zaidi ya motoni.

Kwa yote mawili, kuhofia kurejeshwa kuwa daraja la chini, na kukosa utulivu juu ya kupelekwa motoni, wazo la kuzaliwa upya kwa roho katika mwili mwingine katika zama tofauti na mahali pengine linaonekana ndilo lenye uwezekano mkubwa. Hivyo, kundi fulani lililobuni fikra hizi hasi limefanikiwa kuwachota watu na kuamini uongo huu kwa msaada wa muono finyu wa mawazo. Ya kwamba wafuasi wao hawahitaji ushahidi zaidi na hivyo kuwapa nguvu ya kuzidisha undumila kuwili wao.

Kwa bahati mbaya, imani hii potofu imepenyezwa ndani ya mduara wa Waislamu. Waislamu hawa wengi wao ni wale ambao wanaghera ya kukuza taaluma na uhuru wa kujiona. Kuna mtazamo mwingine kuhusu hili unaohitaji kudokezwa: Watu hao hufafanua mambo yao na kutoa ushahidi kutoka katika kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa tafsiri yao. Kwa hili, wanapindisha maana iliyo wazi ya aya za Qur'an na kubuni tafsiri yao. Lengo hapa ni kusisitiza kwamba imani hii iliyopinda ni kinyume kabisa na Qur'an na Uislamu wa aina hiyo kwa ujumla unapingana na aya za Qur'an ambazo kwa hakika ziko wazi mno na zenye kueleweka.

Makundi haya hudai kwamba zipo aya chache ndani ya Qur'an ambazo zinafungamana na mawazo yao hayo potofu. Miongoni mwa aya hizo ni:

'Watasema, "Mola wetu! umetufisha mara mbili na umetuhuisha mara mbili! Basi tunakiri dhambi zetu. Basi je, iko njia ya kutoka?" (Al-Muumin:11).

Kwa mnasaba wa aya hii waumini wa nadharia ya kuzaliwa katika kiwiliwili kingine hutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:

Mwanadamu amepewa maisha mengine baada ya kuishi katika maisha hayo kwa muda na kisha kufariki dunia. Hii ni mara ya pili anayofanywa kuwa kiumbe tena na pia ndicho kipindi ambacho roho yake inakamilika. Hadai kwamba, ni baada ya kifo kinachofuatiwa uhai huu wa mara ya pili, ndipo mtu atafufuliwa akhera.

Kama mtu atajiepusha na uegemezi wa fikra na kuamua kuwa huru, uchambuzi wa aya hii utakuwa kama ifuatayo:

Kutokana na aya ni dhahiri kuwa mwanadamu hujuta katika hatua mbili za uhai na vifo. Kwa mnasaba huu, kwamba kuna uhai wa mara ya tatu au kifo cha mara ya tatu hakina nafasi hapa.

Kama hali ndio hii; swali moja huja katika akili: 'Ni ipi kati ya awali ya mwanadamu? Kuwa hai au kuwa mfu? Jibu lake linapatikana katika aya ifuatayo:

"Vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu, na hali mlikuwa wafu, akakuhuisheni kisha atakufisheni, kisha atakuhuisheni? Kisha kwake mtarejeshwa?" (Al-Baqara:28)

Aya inajieleza yenyewe na kujitosheleza; awali, mtu alikuwa mfu. Kwa maneno mengine, kwa namna mwanadamu alivyoumbwa, alianza na vitu ambavyo havina uhai kama vile, maji, udongo na kadhalika kama aya zinavyobainisha. Kisha, umbo hili litokanalo na vitu visivyo na uhai vikapewa uhai, 'akauumba na kuupa sura'. Hiki ndicho kifo cha kwanza na hivyo uhai wa kwanza kutoka kwenye umaiti.

Kisha, baadhi ya huu uhai wa kwanza kutoka kwenye umauti, uhai hukoma na mwanadamu hufa tena. Anarudi katika udongo tena kama ilivyokuwa katika hatua ya awali na anarudishwa na kuwa si chochote. Hii ni hatua ya pili ya mpito kuelekea katika kifo. Hatua ya pili na ya mwisho ya mtu kufufuliwa kutoka katika umauti itatokea Akhera. Kwa kuwa hali iko hivi, hii ingelazimisha kuwepo na mfufuko wa tatu. Hata hivyo hakuna aya hata moja inayoainisha kuwepo kwa mfufuko wa tatu.

Ukizingatia aya zilizonukuliwa hapo juu, yaani Al-Muumin:11 na Al=Baqara:128 hakuna inayogusia kuwepo kwa mfufuko wa mara ya pili katika dunia hii. Kwa upande mwingine, aya hizi zinadhihirisha juu ya kuwepo mfufuko wa kwanza duniani na wa pili Akhera.

Cha kusikitisha wanaoamini juu ya uhai zaidi ya mara moja hapa hapa duniani egemeo lao ni katika aya hizi mbili tu. Aya ambazo, badala ya kuthibitisha ufufuo wa pili hapa duniani zinakanusha uwezekano wa kuwepo kwa hali hiyo. Kwa nyongeza, aya kadhaa ndani ya Qur'an zinabainisha wazi kwamba kuna uhai wa mara moja tu hapo duniani ambao mwanadamu yuko katika mtihani na kwamba hakuna kurejea tena duniani baada ya kifo. Hili limebainishwa katika aya ifuatayo:

'Hata yanapomfikia mmoja wao mauti, husema 'Mola wangu! Nirudishe (ulimwenguni) ili nifanye mema sasa badala ya yale niliyoyaacha! (Ajibiwe) 'Haiwezekani! Kwa hakika hili ni neno tu analolisema yeye; na mbele yao kuna maisha ya baada ya kufa mpaka siku ya kufufuliwa. (Al-Muuminun:99 - 100).

Majadiliano yaliyo katika aya hizi, ni ushahidi kuwa baada ya kifo cha pili hakuna tena kurejea katika dunia hii. Kwa upande mwingine, aya hii inatufahamisha kwamba katika hali ya kukata tamaa, makafiri watatamani wapewe uhai wa mara ya pili hapa hapa duniani kabla ya ule wa Akhera ili warekebishe mwenendo wao. Aya inabainisha kuwa hilo ni muhali tena bali wasubiri ufufuo wa pili utakaokuwa Akhera, tayari kwa malipo ya matendo ya wanadamu wote, kila mmoja na hesabu yake.

Kuhusu watu wa peponi na watu wa motoni pia baada ya kufufuliwa Akhera, watu wa peponi: 'Humo hawajaonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na atawalinda na Adhabu ya Jahannam. Kwa fadhila zitokazo kwa Mola wako; huko ndiko kufuzu kukubwa. (Ad-Dukhan:56 - 57). Kuhusu watu wa motoni: 'Waliokufuru wanadai kuwa hawatafufuliwa. Sema kwanini? Kwa haki ya Mola wangu ninyi lazima mtafufuliwa; kisha lazima mtajulishwa mliyoyatenda. Na hayo ni sahali kwa Mwenyezi Mungu. (Taghaabun: 7.) Na walisema: Haukuwa (uhai) ila ni uhai wetu huu wa dunia, tunakufa na tunaishi, wala hakuna kinachotuangamiza ulimwengu; lakini wao hawana elimu ya hayo wanadhani tu (Al-Jathiyah:24)

'Je sisi ni wenye kufa tena? Ila kifo chetu cha kwanza! Wala sisi hatutaadhibiwa? Kwa hakika huku ndiko kufuzu kukubwa.' (As-Saaffah:58 - 59).

Baada ya aya hizo, wazo au nafasi ya maswali zaidi kuulizwa inakuwa haipo. Kwa kuukamilisha mjadala huu ni kwamba, pamoja na umauti kutajwa kuwa ni mara mbili, lakini kifo atakachohisi mwanadamu ni kimoja tu, kile ambacho hufuatia baada ya uhai wa hapa duniani. Wakati huo mwanadamu anakuwa na hisia zote na kufahamu kila linalotokea. Kifo cha kabla ya uhai wa duniani mwanadamu huwa hana analotambua.

Kwa mtazamo huu, kushikilia kuwa roho huhama na kuvikwa kiwiliwili kingine cha mnyama au mwanadamu mwingine na kuendelea kuishi hapa duniani, au kwamba kuna kufa zaidi ya mara mbili, ni dhana ambazo hazina lengo jingine zaidi ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na Qur'an.

Hali kadhalika, kama Mwenyezi Mungu ameumba mfumo wa maisha ambao moja ya matukio ya mfumo huo ni roho kuhamishiwa katika kiwiliwili kingine na kuendelea kuishi hapa hapa duniani, asingesita kumtambulisha hilo mwanadamu katika muongozo aliouleta yaani Qur'an. Aya za Qur'an zinaanisha uhai wa namna mbili tu. Wa kwanza ni huu wa hapa duniani, na wa pili ni ule wa baada ya huko Akhera.

'Yeye ndiye aliyekuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha kwa pande la damu, kisha akakutoeni katika hali ya mtoto mchanga; kisha mkafikia wakati wa nguvu zenu kamili; kisha muwe wazee. Na wengine katika ninyi hufishwa kabla (ya kufikia uzee au ujana au utoto). Na ili mfikie muda uliowekwa ili mpate kufahamu. Yeye ndiye anayehuisha na kufisha; na anapolihukumia jambo (liwe), basi (mara moja tu) huliambia 'kuwa' nalo likawa (Al-Muumin: 67 - 68).

'Na kwa yakini wale wanaozisopotoa aya zetu (ili wasizifuate na wapoteze wengine) hawatufichiki. Je! atakayetupwa motoni ni bora au atakayetajwa kwa amani siku ya kiama? Fanyeni mnayopenda, kwa yakini yeye anayaona yote mnayoyatenda. (Haa mym Sajidah (Sussilat):40).


    
3 / total 8
You can read Harun Yahya's book Kufa Ufufuko Jahannam online, share it on social networks such as Facebook and Twitter, download it to your computer, use it in your homework and theses, and publish, copy or reproduce it on your own web sites or blogs without paying any copyright fee, so long as you acknowledge this site as the reference.
About this site | Tengeneza kurasa yako ya nyumbani | Add to favorites | RSS Feed
Mambo yote yanaweza kuynakiliwa, kuchapwa na kusambazwa kwa kurejea katika kurasa hii
(c) All publication rights of the personal photos of Mr. Adnan Oktar that are present in our website and in all other Harun Yahya works belong to Global Publication Ltd. Co. They cannot be used or published without prior consent even if used partially.
© 1994 Harun Yahya.www.harunyahya.com
page_top