Kufa Ufufuko Jahannam

SHUSHA KITABU

Download (DOC)
Maoni

SURA ZA KITABU

< <
6 / total: 8
KUFA UFUFUKO JAHANNAM - Harun Yahya
KUFA UFUFUKO JAHANNAM
   KUHARIBIWA KWA MBINGU

Katika siku ya hukumu, sio dunia tu itakayoharibiwa, bali anga na Ulimwengu mzima utaharibiwa. Mkakati wa kwisha kwa ulimwengu utagusa anga, mwezi jua, sayari na pia dunia na kila kilichomo ndani yake, milima na bahari. Qur’an inabainisha kwamba siku hiyo:

‘Hakika haya mnayoahidiwa, bila shaka yatatokea. Wakati nyota zitakapofutwa (nuru yake). Na mbingu zitakapopasuliwa. Na milima itakaposagwa sagwa. (Al-Mursalat: 7 - 10).

Siku hiyo, viumbe vyote vilivyonasibishwa na umilele vitaanguka na kuharibiwa na kuwa si cho chote si lolote. Huu ni ukweli pia kuhusu mbingu. Tangu mwanadamu adhihiri ulimwenguni, huona mbingu kama paa linalomlinda. Hata hivyo siku ya kufufuliwa, paa hili litaanguka na kupasuka vipande vipande. Hewa na anga ambavyo vinamzunguka mwanadamu na kumpa pumzi ya kupumuwa vitakuwa kama chuma kilicho yeyushwa. Qur’an inaeleza hivyo:

‘Siku mbingu zitakapokuwa kama shaba iliyoyeyuka. (Al-Maany: 8).

Na pia vitapasuka kwa kishindo kikubwa. Hewa itajaza mapafu ya mwanadamu si kwa ajili ya kuhuishwa bali kwa ajili ya kuunguzwa.

Ulinganisho unaoweza kuletwa kati ya woga wa majanga yanayotokea katika dunia hii na vitisho vya matukio ya siku ya kufufuliwa unaweza kutoa mwanga halisi wa siku hiyo itakavyokuwa. Matetemeko ya ardhi na milipuko ya volkano ni miongoni mwa majanga ambayo yanamuogopesha mwanadamu zaidi. Miamba ya ardhi inapasuka kwa tetemeko la ardhi au milipuko ya volkano hupelekea hali ngumu ya maisha ya kila siku kwa muda mfupi tu! Hali hii humfanya mwanadamu atanabahi kuhusu ardhi anayokanyaga juu yake kwa majivuno kwamba si chochote si lolote.

Pamoja na yote hayo yanayomuumiza Mwanadamu hutokana na matetemeko ya ardhi na milipuko ya volkano hutokea mara chache mno na hudumu kwa kipindi kifupi tu. Vidonda hupona, na maumivu husahaulika baada ya muda fulani. Lakini siku ya kufufuliwa, sio kama tetemeko la ardhi au milipuko ya volkano au majanga mengine. Uzito na mfuatano wa matukio haya ya kuangamiza kila kitu hutoa taswira kwamba kila kitu kimefikia hatua ya kutorudi nyuma tena. Kwa mfano, tukio ambalo hakuna anayelifikiria hali yake halisi kwamba ‘Mbingu zitapasuka na kuanguka vipande vipande’. Hii ni kuonesha kwamba ‘kanuni za maumbile’ zinazojulikana zitakuwa zimefikia ukomo wake. Mbingu na ardhi nazo kwa mamailioni ya miaka kadhaa iliyopita vimeonekana vitu madhubuti, lakini siku hiyo vitapondwa pondwa na yule aliyeutengeneza mara ya kwanza.

‘Mbingu zitakapopasuka. Na nyota zitakapopukutika. Na bahari zitakapopasuliwa. (Inftar: 1 - 3).

Inaelezea siku ya kufufuliwa hali itakavyokuwa, kwamba mbingu zitapasuka na kutengana, nyota zitapukutishwa, na bahari zitajaa na kufurika. Pia katika aya nyingine:

‘Mbingu zitakapopasuka. Na zitakapokinga sikio kwa Mola wake (kusikiliza amri) na zimepasiwa (na kusikiliza). (In-Shiqaq: 2 - 2).

Kila mwanadamu anachokiona kina thamani siku hiyo kitakuwa kimefikia ukomo. Kila kilichoko mbinguni kitakufa kimoja baada ya kingine.

‘Jua litakapokunjwa kunjwa. Na nyota zitakapopukutishwa. (At-Takwyr: 1 -2).

Jua ambalo ni chanzo cha mwanga kwa mamilioni ya miaka litakunjuwa kunjwa, likifanya lifanyalo chini ya kimaya yake. Hadi wakati huo wa tukio, miongoni mwa wanadamu waliojenga dhana kuwa nyota ni vitu ambavyo viko mbali sana na kwamba haviwezi kufikiwa kwa umbali na kustaajabisha, lakini katika siku hiyo, nyota zitapukutishwa kama mchezo wa mwanasesere. Milima isiyotetereka kama vigingi itasogezwa, bahari isiyo na mipaka nayo itaanza kuchemshwa. Kwa matukio yote haya, yule ambaye ni mmiliki halisi, mwenye nguvu aliyejuu ya kila kitu, ataeleweka vyema kwa kila mmoja. Uwezo wa Mwenyezi Mungu ni mpango wake vitatimia na hivyo mwanadamu kwa uchungu kabisa atatanabahishwa kuwa kule kukosa kwake muelekeo siku hiyo hakuna wa kumnusuru na kumsaidia. Sababu kubwa ya kukosa kwake muelekeo ni kule kushindwa kwake kupambanukiwa na nguvu za Mwenyezi Mungu wakati bado kifo kilikuwa hakijamkuta, Siku hiyo alama ya mmiliki halisi wa Ulimwengu na maisha atadhihiri na kujulikana.

‘Na hawakumheshimu Mwenyezi Mungu heshima ipasayo. Na siku ya kiama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume. Ameepukana na upungufu na yu juu kabisa kuliko yale wanayo mshirikishia. (Az-Zumari: 67).

HALI YA WATU ITAKAVYOKUWA

Hofu yote hii na kuchanganyikiwa katika siku ya malipo itatokana na makafiri kukosa muelekeo. Jinsi mwanadamu anavyozidi kuchupa mipaka kwa kughafilika, ndivyo atakavyozidi kujawa na wasiwasi na woga. Hali ya woga na maangamizi ambayo huanzia kwenye kifo haitakwisha milele. Kila tukio litakuwa chanzo cha woga. Kila tukio lililofichika linalomkabili pia huchochea kumuogopesha usoni. Woga huu unakuwa mzito kiasi kwamba inabadilisha rangi ya nywele za mtoto kuwa kahawia.

‘Basi ninyi mkikufuru, mtawezaje kujihifadhi na (balaa ya) ambayo itawafanya watoto kuwa wenye mvi (wazee)? Mbingu zitapasuka siku hiyo; ahadi yake (Mwenyezi Mungu) itatekekezwa tu (Al-Muzzammil: 12 - 13).

Hao wanaodhani kuwa Mwenyezi Mungu hana habari na yale wanayofanya watagundua wakati huo kuwa Mwenyezi Mungu anaakhirisha hukumu hadi siku ya kufufuliwa viumbe. Hili linafafanuliwa kama ifuatayo:-

‘Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayoyafanya madhalimu. Hakika yeye anawaakhriisha tu mpaka siku ambayo macho yatakodoka (Ibrahim: 42).

Katika aya nyingine, hofu inayohisiwa na makafiri inafafanuliwa kama ifuatavyo:

‘(Msiba) ugongao nyoyo! (Msiba) ugongao nyoyo ni upi huo? Ni jambo gani litakalo kujulisha ni upi huo (msiba) ugongao nyoyo? Siku ambayo watu watakuwa kama madumadu. (watoto wa nzige) waliotawanywa. Na milima itakuwa kama sufi zilizochambuliwa (zikawa zinapeperuha): (Al-qaariah: 1-5).

Uhusiano mzito wa dunia hii ni mapenzi na hisia za mama kumlinda mwanawe. Uzito wa siku ya kufufuliwa, utavunja hata uhusiano huu mzito vilevile. Mitikisiko itasbabisha kila kitu kiwe katika himaya. Mtikisiko huo utasababisha Mwanadamu kutaharuki na kupoteza fahamu. Wakati wamechaganyikiwa na kushtuka, watakimbia huku na kule kama walevi. Kinachowafanya wapoteze fahamu ni kutokana na uzito wa adhabu za Mwenyezi Mungu.

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu, hakika mtetemeko wa kiama ni jambo kubwa. Siku mtakapokiona (hicho kiama) - kila mwanamke anyonyeshaye, na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake (kabla ya wakati kufika). Na utawaona watu wamelewa; kumbe hawakulewa, lakini ni adhabu ya Mwenyezi Mungu (tu hiyo) iliyo kali: (Al-Hajj: 1 - 2).

Mbali na kuogopesha na kuhamaki, hisia nyingine iliyokuwa ngumu mno kwa watu itakuwa ile ya mwanadamu kukata tamaa. Mwanadamu huchukuwa hadhari za makusudi ili kujilinda dhidi ya majanga yenye kuweza kutokea, na dhidi ya njaa, matetemeko ya ardhi, mafuriko, vimbunga au hata vita vya kutisha kama nuklia. Mwanadamu hutafuta njia ya kujilinda na kujenga majumba. Hata hivyo, katika siku hiyo, hakuna kitakachosalia ambacho mwanadamu ataona kuwa ni salama kwake endapo anaweza kutafuta hifadhi. Hatapata msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Pia, hakuna yeyote au mamlaka ambayo itatoa msaada. Awali, mwanadamu akitafuta msaada na mwongozo kupitia sayansi na teknolojia. Lakini kwa wakati huo, kanuni zote za sayansi zimevunjika. Hata kama teknolojia imeendelea kiasi kwamba imemuwezesha mmoja kwenda mbali upenuni katika ulimwengu huu, bado ghadhabu za Mwenyewe Mwenyezi Mungu zitamfuata huko huko. Hiyo ni kwa sababu siku ya kufufuliwa imeenea ulimwengu mzima. Si dunia tu aliyoishi kwa salama bali vile vile nyota zilizoko mbali kabisa zitarejea kufuatana, na apendavyo Mwenyezi Mungu; Likiwemo jua.’ (Takwir: 1 - 2).

Kukata tamaa kutakakomsibu mwanadamu, kunaelezwa vizuri katika aya zifuatazo:-

‘Na Mwezi utakapopatwa, Na jua na Mwezi vitakapokutanishwa. Siku hiyo Mwanadamu atasema, “Nitakimbilia wapi? Hapana! Hakuna mahali pa kukimbilia. Siku hiyo ni kwa Mola wako (tu). (Al-Qiyaam: 8-12).

PARAPANDA LA PILI NA KUFUFULIWA VIUMBE

Wakati baragumu (parapanda) litakapopulizwa kwa mara ya kwanza, mbingu na ardhi vitavunjwa vinjwa na ulimwengu wote utafika kikomo. Hakuna nafsi itakayoachwa hai. Kwa maneno ya Qur’an:

(Ikimbukeni) siku ambayo ardhi hii itabadilishwa kuwa ardhi nyingine, na mbingu; nao watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu, Mmoja, Mwenye nguvu. (Ibrahim: 48).

Haya mazingira mapya yameandaliwa kwa ajili ya hukumu ya Mwisho. Ufafanuzi wake ni:

‘Na wanakuuliza habari za milima. Waambie: “Mola wangu ataivunja vunja. Na ataiacha (ardhi yote kama) uwanda uliokaa sawa. Hataona humo mdidimo wala kuinuka. (Taha: 105 - 107).

Huu ndio wakati ambao watu watafufuliwa, na kukusanywa na kusubiri hesabu ya matendo yao. Pia, hapo ndipo watakapojifunza kuwa wanaelekea wapi. Wakati umewadia kwa watu kufufuliwa na kuhudhurishwa kwa Mola wao, Al-Wahid, mwenye nguvu. Na ndipo baragumu litapulizwa kwa mara ya pili. Wale watu waliokanusa akhera na kufiliwa katika dunia hii, watafufuliwa kutoka makaburini mwao.

Hili ni jambo ambalo hawakuwa wanafikiriwa kuwa litatokea kweli. Qur’an imebainisha juu ya matukio haya kuwa:

‘Na litapigwa baragumu watoke roho watu waliomo mbinguni na waliomo ardhini ila yule amtakaye Mwenyezi Mungu. Tena litapigwa mara nyingine. Hapo watafufuka; wawe wanatazama. Na ardhi itang’ara kwa nuru ya Mola wake: (Az-Zumar: 68 - 69).

KUTOKEA KWA WAFU KUTOKA MAKABURINI MWAO

Mwenyezi Mungu anaelezea kwa undani juu ya hali halisi wakati wafu watakapofufuka makaburini na kila sehemu walizofia. Kama ilivyotanabahishwa ndani ya Qur’an, tukio hili kubwa litatokea, hivyo, hadi wakati tarumbeta litakapopulizwa kwa mara ya pili watu wataitwa tokja walikozikwa au walikofishwa ambako ndiko makaburi yao:

‘Macho yao yatainama chini; wanatoka katika makaburi kama kwamba ni nzige waliotawanyika. (Al-Qamar: 7). ‘Na katika ishara zake ni kuwa mbingu na radhi vimesimama; kwa amri yake. Kisha atakapokuiteni wito mmoja tu, mtatoka ardhini. (Ar-rum: 25).

‘Siku itakapo wapasukia ardhi, (watoke) humo upesi upesi, huo ni mkusanyiko rahisi kwetu (Qaf:44).

Kama vile wanashambulia golini, watamfuata muitaji ambaye atawaita huku shingo zao zikielekezwa kwake. Wito huu utakuwa si wenye kufafana na wa aina yoyote uliyopata kusikika.

“Siku watakapotoka makaburini kwa wepesi kama kwamba wanakimbilia mfunda (mede), (mfundo wao wanaposhindana) (Ma’arij: 43).

‘Basi jiepushe nao. Na (wakumbushe) Siku atakapoita muitaji huyo kuliendea jambo zito (hilo la kiama) (Al-Qamar: 6).

‘Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu. Na zitanyenyekea Sauti kwa Mwingi wa Rehema na hutasikia mchakato ila wa miguu (Tahr: 108).

Wale ambao wamechupa mipaka ambayo ameiweka Mwenyezi Mungu, ambao hawakumtii Mwenyezi Mungu, wakikazania taratibu zao wenyewe za maisha, waliomkanusha Mwenyezi Mungu, na wakaendelea kuwa jeuri, watakuwa ghafla watiifu na kunyenyekea kwake punde watakapotolewa makaburini mwao. Bila kuuliza swali wataitikia wito huu. Kwa sababu majaribio au mitihani katika dunia hii imekwisha, hawatakuwa na chaguo lingine zaidi ya kuthibitisha lile walilolitenda. Hata kama wangependa kufanya hivyo, hawawezi tena kufanya kinyume chake. Hawawezi tena kujenga matumanio kama hayo. Hawana uwezo wa kuhimili wito huo. Ndio maana, uono wao uliojengeke katika hisia kali utakuwa, hii ‘Ni siku isiyo na pa kupenya.’

Macho yao yatainama chini, wanatoka katika makaburi kama kwamba ni nzige waliotawanyika. Wanamkimbilia muitaji huyo na huku wanasema hao makafiri: ‘Hii ni siku ngumu (kabisa, haina pa kupenya) (Al-Wamar:7-8).

Hivyo makafiri watakimbia mbele. Kila mmoja atadhihirisha utiifu wake. Siku hiyo kitu pekee ambacho watu watakuwa nacho kilicho muhimu ni Imani. Hata hivyo makafiri watakosa imani. Ndio maana nyoyo zao ni tupu. Tunafahamishwa katika Qur’an:-

(Wawe) wanakwenda mbio, vichwa juu, na macho yao hayapepesi, na nyoyo zao tupu (haziko, wanahemkwa mbio, mapepe): (Ibrahim: 43).

Tanafahamishwa kuwa watakuwa wanaelekea mahali maalum katika makundi ‘Siku itakapopigwa parapanda (baragumu), nanyi mtafika makundi makundi (An-Nabaa:18).

‘Na kisha litapigwa parapanda (bagagumu) (la kufufuliwa) tahamaki hao wanatoka makaburini kwenda mbiombio kwa Mola wao’ Watasema: ‘Ole wetu! Nani aliyetufufua malaloni petu?” (Waambiwe) ‘Haya ndio yale aliyoahidi (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa Rehema na waliyoyasema kwa haki Mitume. (Yasin: 51-52).

Maneno ‘Ah majuto yetu’ au ‘Ole wetu!’ ni kuonesha kuchanganyikiwa kukubwa na kukata tamaa. Kafiri ambaye atashuhudia kufufuliwa kwake atatambua kuwa Mitume ya Mwenyezi Mungu ambao walifikisha ujumbe huu katika kipindi chote cha uhai wake walisema kweli. Atagundua kwamba ataingizwa katika adhabu ya milele ambayo mitume waliwahofisha makafiri juu yake. Muda huo, atafunika aina zote za mashaka na kubakisha ukweli uchukuwe mkondo wake ya kuwa hakuna kitu kinachoitwa ‘Usingizi wa Milele’. Kukatishwa kwake tamaa kutazidishwa kwa matumaini ya kuokolewa kuyoyoma kutokana na adhabu iliyo mbele yake. Makafiri watajawa na hofu, woga na kukata tamaa. Hali yao kwa ujumla ni ya kuchanganyikiwa. Mwenyezi Mungu katika Qur’an anasema:

‘Nyuso nyingine zitakuwa na mavumbi yaike. Giza totoro litazifunika. Hao ndio makafiri watenda mabaya (Abasa: 40 - 42).

‘Na siku ya kiama utawaona wale waliomsingizia uongo Mwenyezi Mungu nyuso zao zitakuwa nyeusi. Je, si katika Jahannam makazi ya wale wanaotakabari? (Az-Zimar” 60).

Mwenyezi Mungu atawafufua makafiri katika siku hiyo hali yakuwa ni vipofu? Anasema:

‘Na atakayejiepushe na mawaidha yangu (hayo), basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na siku ya kiama tutamfufua hali ya kuwa ni kipofu. Aseme, ‘Ee Mola wangu! Mbona umenifufua kipofu, na hali nilikuwa nikiona?”” (Mwenyezi Mungu) Atasema: ‘Ndio vivyo hivyo, zilikuja aya zetu ukazisahau, (ukazipuuza), na kadhalika leo utasahauliwa (utapuuzwa). (Taha: 124 - 126).

Na ambaye Mwenyezi Mungu amemuongoa, basi yeye ndiye aliyeongoka; na anaewachia kupotea, basi wewe hutawapatia walinzi wasiokuwa yeye (Mwenyezi Mungu). Na tutawakusanya siku ya kiama, hali yakuwa wanakokotwa juu ya nyuso zao na hali yakuwa vipofu na mabubu na viziwi. Makazi yao ni Jahannam. (Na) kila ukifanya kusinzia kidogo tutauzidishia mwako. (Bani Israil: 97).

Pia sehemu nyeupe ya jicho itafanywa kuwa buluu. Rangi hii ya macho itazidisha kuchanganyikiwa na sura ya kutisha kwa makafiri. Mwenyezi Mungu anabainisha kuwa:

Siku itakapopigwa Baragumu na tukawakusanya wakosa siku hiyo, hali macho yao yatakuwa kibuluu (kwa khofu) (Bani Israil: 102).

Kwa hali hii ya kuchukiza na ya kuvunja hadhi ya makafiri, itawatofautisha na waumini tangu awali. Huu ndio mwanzo wa Mwisho wa kundi la watu waliokuwa wanapinga aya za Mwenyezi Mungu na wakabakia kuwa jeuri.

HAKUTAKUWA NA URAFIKI, UDUGU NA USHIRIKIANO

Siku hiyo Mwanadamu atakuwa ametengwa mno kiasi cha kutojali wengine. Atamuacha hata mama yake, baba yake, mke na watoto pia. Kubwa litakalo mshughulisha kutokana na uzito na tishio ambalo halielezeki katika siku hiyo ya kufufuliwa ni kuhusu yale mambo yake aliyoyatanguliza Mwenyezi Mungu anaelezea siku ya kufufuliwa kama ifuatavyo:-

‘Na ni nini kitakachokujulisha siku ya malipo ni siku gani hiyo! Tena ni nini kitakachokujulisha siku ya malipo ni siku gani hiyo! Ni siku ambayo nafsi haitamiliki nafsi (nyingine) chochote; na amri siku hiyo itakuwa ya Mwenyezi Mungu tu. (Al-Infitar: 17-19).

‘Basi itakapokuja Sauti kali iumizayo masikio (Sauti ya baragumu la Kiama); siku ambayo, mtu atamkimbia nduguye, na mamaye na babaye, na mkewe na wanawe. Na kila mtu miongoni mwao, siku hiyo atakuwa na hali itakayo mtosha mwenyewe. (Abasa: 33-37).

Na uhusiano wa kijamii utakosa thamani siku hiyo na utaakuwa na mwisho wa uchungu. Mtikisiko wa siku hiyo utasababisha uhusiano wa kindugu usiwe na maana. Kitu pekee chenye thamani kitakachobaki ni Imani.

‘Basi litakapopulizwa Parapanda, hapo hautakuwepo ujamaa baina yao siku hiyo, wala hawataulizana. Ama wale ambao mizani ya amali zao (nzuri) itakuwa nzito, hao ndio waliozitia hasarani nafsi zao, na katika Jahannam watakaa muda milele (Al-Muuminuun: 101 -103).

Uhusiao wa kifamilia utavunjika kiasi ambacho watu watakuwa radhi kuwatoa wawapendao katika watoto wake, ndugu na hata ndugu zao wote ili wao wapate kujiokoa. Hakuna rafiki mzuri atakayeuliza juu ya rafiki yake, japo wanaweza kuonana. Muovu atatamani ajitakase na adhabu ya siku hiyo kwa kuwatoa watoto wake au mke wake, au ndugu yake au familia yake iliyomhifadhi au yeyote katika dunia, kama hicho ndicho kitakachofaa kumuokoa.

‘Wala Jamaa hatumuuliza jamaa (yake). (Ingawa) watafanywa waonane. Mwenye kosa atatamani ajikomboe katika adhabu ya siku hiyo kwa kuwatoa watoto wake. Na mkewe na nduguze,. Na jamaa zake waliomzunguka kwa kila upande, Na kuvitoa vyote vilivyomo katika ardhi, kisha aokoke. Lakini wapi! Kwa hakika huo ni moto uwakao barabara. (Al-Ma’anj: 10-15).

‘Ofa’ hii kwa kweli ni alama juu ya kukosa shukurani na mawazo finyu ya makafiri wakati manufaa ya yanapotetereka. Ofa hii pia inatoa funzo juu ya yale yanayopiganiwa katika dunia hii. Mara nyingi Mwanadamu hushindana kutafuta yale malengo yanayoonekana; na kwa ajili ya fedha atafanya kazi maisha yote. Hata hivyo kama Qur’an inayotufahamisha, katika juhudi zake ambazo tayari zimemkatisha tamaa za kutaka kujikomboa, mtu atakuwa radhi kulipa, sio mwanamke mmoja tu, bali wanawake wote ulimwenguni au vitu vyote alivyonavyo ili tu aweze kuokoka. Hizi zote ni juhudi zisizo na matunda. Mwenyezi Mungu ndiye ambaye mkononi mwake imo miliki ya kila kilichopo ulimwenguni. Ukombozi kwa Upande mwingine, hubaki nyuma, katika maisha ya kidunia. Kwa wakati huo, mtu atakuwa amekwishachelewa. Kama ilivyokwishaahidiwa, moto umekwisha kokwa tayari ukisubiri.

KUKUSANYWA KWA WATU ILI WOTE HESABU YA MATENDO YAO

Qur’an inaelezea maana halisi ya Maisha:

‘Ewe Mtu! Hakika wewe unajikusuru kusuru (katika kufanya mambo yako) mpaka (siku utakayokutana na) Mola wako; basi (amali zako hizo) utazikata (Al-Inshiqaq:6)

Bila kutazama lipi analofanya katika maisha yake aya, mwishowe atasimama mbele ya Mwenyezi Mungu. Lengo kuu la maisha haya ni kuwa mtumwa wake. Muda muhimu, kwa upande Mwingine, ni siku ya kufufuliwa, wakati mwanadamu atakapotoa hesabu juu ya vitendo vyake katika maisha yake ya dunia hii. Kila siku inavyopita ndivyo mtu anavyoisogelea siku hii na wakati huu. Kila siku inayopita ndiyo mtu anavyoisogelea siku hii na wakati huu. Kila siku inavyopita ndivyo mtu anavyoisogelea siku hii na wakati huu. Kila saa ipitayo, dakika au hata sekunde ni hatua kuelekea kifo, kufufuliwa na muda wa kuhesabiwa. Maisha kama mshale wa saa, hutembea bila kusimama kuelekea huko. Hakuna njia ya kuusimamisha muda, au kuurejesha nyuma. Watu wote hufuata mkondo huu:-

‘Hakika marejeo yao ni kwetu. Kisha, bila shaka, hisabu yao ni kwetu. (Al-ghashujah: 25 – 26).

Kuna takriban watu bilioni sita katika ardhi leo hii. Ukiongeza idadi ya wale walioishi kabla itakupa picha juu ya msongamano wa watu watakaokusanyika siku hiyo ya kufufuliwa. Watu wote, tangu wakati wa Nabii Adamu (juu yake amani), mtu wa kwanza hapa duniani hadi mtu wa mwisho asiyeamini ambaye ameishi katika dunia hii watakuwepo siku hiyo bila kusahauliwa hata mmoja. Kundi hili la watu litaonesha picha ya kustaajabisha. Hata hivyo, wakati hayo yakijiri, kwa hakika itakuwa hali ya kutisha kweli kweli. Hali ya watu wote mbele ya Mwenyezi Mungu imeelezwa katika Qur’an kama ifuatavyo:-

‘Siku hiyo watamfuata mwitaji asiye na upotofu. Na zitanyenyekea sauti kwa (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa Rehema na hutasikia ila mchakato tu wa miguu. Siku hiyo hautafaa uombezi (wa yeyote) ila wa yule aliyemruhusu Mwingi wa Rehema na kuiridhia kauli (yake). (Mwenyezi Mungu) anajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala wao hawawezi kumjua (Mwenyezi Mungu) vilivyo. Na nyuso nyingine zitadhalilika (siku hiyo) mbele ya Mwenyezi Mungu aliye wa milele daima, anayepitisha mambo yote. Na watakuwa wenye kuharibikiwa kila mwenye kufanya dhuluma. (Taha: 108 = 111).

Muda wa kutoa hesabu, ambao makafiri walikanusha muda wote wa uhai wao, ambapo waumini walijitahidi kujiandaa kwao, umewadia. Mahali patukufu pameandaliwa kwa ajili ya mahakama hii. Kwa mujibu wa Qur’an, siku hiyo:=

‘Na mbingu zitapasuka, basi siku hiyo, zitakuwa dhaifu kabisa. Na malaika watakuwa kandoni mwake (hizo mbingu) na malaika wa namna nane watachukuwa kiti cha enzi cha Mola wako juu yao. (Al-Haqqah: 16-17).

Siku ambayo zitasimama roho (za viumbe wote) na malaika safusafu: Hatasema siku hiyo ila yule ambaye (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa Rehema amempa idhini (ya kusema) na atasema yaliyo sawa. (An-Nabaa: 38).

Mola wa mbingu na ardhi, atahitaji hesabu ya matendo ya waja wake. Chanzo cha mateso yenye kuwasiliana, utukufu na nguvu zake, vyote vitadhihirika. Moto uwakao utaendelea kuwaka huko Jahannam. Mwenyezi Mungu, aliyeumba kila kitu kwa namna ya kipekee, ameandaa adhabu iumizayo kwa makafiri. Hakuna yeyote awezaye kuadhibu mfano wa kuadhibu kwake siku hiyo, kabla na baada yake.

Katika Qur’an Mwenyezi Mungu anasema:=

‘Sivyo hivyo! (Kumbukeni) itakapovunjwa ardhi vipande vipande. Na kufika (amri ya) Mola wako, na malaika safu safu. Basi siku hiyo italetwa Jahannam. Siku hiyo mwanadamu atakumbuka, lakini kukumbuka huko kutamfaa nini? Atasema: “Laiti ningalitanguliza (wema) kwa ajili ya uhai wangu ( huu wa leo).” Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake (Mwenyezi Mungu). Wala hatafunga yeyote jinsi ya kufunga kwake (Mwenyezi Mungu). (Al-Fajr: 21-26).

Kama mwanadamu atashindwa kumtumikia Mola wake katika dunia hii na kujiandaa kwa siku iliyokuu, basi ataambulia majuto. Atatamani arejeshwe kuwa udongo kuliko kufufuliwa. Hata hivyo, kujuta kwake huko hakutamsaidia lolote. Kinyume chake, itakuwa ndio chanzo cha huzuni na kuongeza sehemu ya adhabu iliyoandaliwa huko motoni.

“…Siku ambayo mtu atakapoona yaliyotangulizwa na mikono yake miwili, na kafiri atasema: Laiti ningalikuwa udongo(An-Nabaa 40)

KUDHIHIRISHWA KWA VITABU NA MIZANI YA HAKI

Kabla ya kupata fursa ya kushinda mitikisiko iliyosababishwa na kufufuliwa, wanadamu watakuwa wamepigwa na hofu kubwa na kutetemeka mno. Hii ni kwa sababu watatoa hesabu ya matendo yao mbele ya Mwenyezi Mungu. Matendo yao yote waliyoyafanya wakati wa uhai wao na pia fikra zao zote zitadhihirishwa. Hakuna hata jambo linaloonekana dogo litakalosahauliwa. Aya ifuatayo inafafanua hilo kwa uwazi:=

Ewe Mwanangu! Kwa hakika jambo lolote lijapokuwa na uzito wa chembe ya hardali, likawa ndani ya jabali au mbinguni au katika ardhi, Mwenyezi Mungu atalileta (amlipe aliyefanya); bila shaka Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa mambo yaliyofichikana; (wa) ni mjuzi wa mambo yaliyo dhahiri. (Luqman:16).

Hiki ni kipindi karibu kabisa na peponi au motoni. Watu wataona waliyoyatanguliza kwa ajili ya maisha yao ya milele. Hili ameelezwa katika Qur’an kama ifuatavyo:=

‘Siku hiyo watu watatoka (makaburni) vikundi vikundi ili waoneshwe vitendo vyao. Basi anayefanya wema (hata) wa kiasi cha uzito wa mdudu chungu ataona jaza yae. (Az-zilizahah: 6-8).

Kama ilivyobainishwa katika Qur’an, makafiri watapewa madaftari yao kwa mkono ya kushoto, wakati waumini watapewa madaftari yao kutoka kuliani. Hali ya watu wa kuliani inafafanuliwa tena ifuatayo.

‘Siku hiyo mtadhihirishwa - haitafichika siri yenu yoyote. Basi ama yule atakayepewa daftari lake kwa mkono wake wa mkono wake wa kuume (kulia) atasema (kwa furaha); Haya! Someni daftari langu (nililopewa sasa hivi). Hakika nilijua ya kuwa nitapokea hisabu yenye (kwa vizuri, kwani nitafanya mazuri).” Basi yeye atakuwa katika maisha ya raha katika pepo tukufu. Vishada vya matunda yake vitakuwa karibu. (Waambiwe) ‘Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya vitendo mlivyofanya katika siku zilizo pita: (Al-Haqqah: 18–24.

Sauti na furaha na bashasha ya Waumini, makafiri wao watakuwa katika hali ya majonzi makubwa kabisa. Watatamani kufa au kutoweka kabisa. Hali yao ya kukata tamaa inabainishwa kama ifuatavyo:-

‘Walakini atakayepewa daftari lake katika mkono wake wa kushoto basi yeye atasema” “Oo! Laiti nisingalipewa daftari langu.” “Wala nisingalijua ni nini hisabu yangu.” Laiti (mauti) yangemaliza (kila kitu changu).” “Mali yangu haikunifaa.” Usultani (ukubwa) wangu umenipotea.” (Al-Haqqah: 25 - 29).

‘Lakini atakayepewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake, Basi yeye atayaita mauti (yamjie, ili afe apumzike, wala hayatamjia), Na ataingia Motoni. Maana alikuwa na furaha (za maasia) pamoja na watu wake. (Na) alidhani kuwa hatarejea (kwa Mwenyezi Mungu). Kwanini (asirejee)? Mola wake alikuwa akimuona; (Inshiqaq: 10 - 15).

Matendo yanayohifadhiwa katika vitabu yatapimwa kwa uadilifu. Haya yanabainishwa katika aya ifuatayo:-

‘Nasi tutaweka mizani ya uadilifu siku ya kiama, na nafsi yoyote haitadhulumiwa hata kidogo. Na hata kama ilikuwa (jambo hilo lina) uzito mdogo wa chembe ya hardali nalo tutalileta; Nasi tunatosha kuwa wajuzi (wazuri kabisa) wa hisabu. (Anbiyaa: 47)

Kila tendo lililofanyika katika maisha haya japo liwe la kiwango kidogo, litawekwa katika mizani. Alama katika mizani itaonesha ama mtu atatumbukizwa motoni kwenye adhabu ya milele au atakuwa katika furaha ya ukombozi wa milele. Kama mizani itaelemea kwenye uzito ina mema, mja atahukumiwa amefuzu na hivyo kuingizwa peponi. Kama haikuwa hiyo, basi atahukumiwa kuwa yeye ni mtu wa motoni. Hakuna yeyote, wala hakuna nguvu itakayomsaidia:-

‘Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito. Huyo atakuwa katika maisha yanayompendeza. Na yule ambaye mizani yake itakuwa nyepesi, Hayo maskani yake yatakuwa katika Hawiya. Na jambo gani litakalokujulisha (hata ukajua) ni nini hiyo (Hawiya)? Ni moto uwakao kwa ukali (kwelikweli). (Al-Qariyah: 6-11.

Kisha, watu wote tangu kuumbwa kwa dunia watatoa hesabu ya mmoja baada ya mwingine. Hapa, nafasi na vyeo vya duniani havitakuwa na thamani. Rais wa nchi au mtu wa kawaida watakuwa sawa. Wanapata huduma inayofanana mbele ya Mwenyezi Mungu. Hapa, wataulizwa katika maswali yaliyo magumu, yasiyopendezesha, kuonesha kama amemtumikia au hakumtumikia Mola wake na kutii amri zake. Dhambi zote, vitendo viovu na fikra za ndani za makafiri, zitadhihirishwa:-

‘Siku zitakapodhihirishwa Siri. Basi hatakuwa na nguvu wala msaidizi. (Tariq: 9-10).

Utaratibu huu unaudhi kwa wale ambao hawakuishi kwa kufuata sheria za Mwenyezi Mungu bali walifuata matamanio ya nafsi zao au kwa kufuata sheria zilizopindishwa, imani na kanuni za jamii. Katika aya ifuatayo Mwenyezi Mungu anaeleza hali halisi itakavyokuwa siku hiyo iliyokuu:-

‘Na mtoto mwanamke aliyezikwa hali ya kuwa yuhai atakapoulizwa. Kwa makosa gani aliuawa. Na madaftari (ya amali) yatakapokunjuliwa (kila mtu akapewa lake). Na utando wa mbingu utakapotanduliwa. Na Jahannam itakapochochewa. Na peoo itakaposogezwa karibu, (wakati huo), kila nafsi itajua ilichokihudhurisha. (At-Takwyr: 8-14).

Mtumwa hana fursa ya kukanusha yale aliyoyatenda mbele ya Mwenyezi Mungu. Matendo yake yote mema na mabaya yatadhihirishwa. Hata kama atakanusha, watakuwepo mashahidi watakaoeleza ukweli. Watu waliomshuhudia katika wakati wa uhai wake wataletwa mbele kutoa ushahidi:

‘Na ardhi (siku hiyo) itang’ara kwa nuru ya Mola wake, madaftari (ya vitendo) yatawekwa; na wataletwa manabii na mashahidi na wengine ambao hawakutegemewa dhidi ya makafiri. Masikio, macho, na ngozi ya mwanadamu vitapewa uwezo wa kuzungumza kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na kutoa ushahidi dhidi yao. Kuumbuliwa kwa mwanadamu na viungo vyake alivyoviona kuwa ni mali yake hapa duniani, kunaongeza huzuni ambayo itakuwa kwa kafiri siku hiyo. Ukweli huu unaelezwa na Mwenyezi Mungu kwa maneno yafuatayo:-

Na (wakumbushe) siku watakapokusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu katika moto, wakawa wanatengwa makundi mbalimbali. Hata watakapoujia (huo moto), hapo ndipo masikio yao, na macho yao na ngozi zao (viungo vyao vingine) zitakapotoa ushahidi juu yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. Na wao waziambie (hizi) ngozi zao: “Mbona mnatushuhudilia?” Nazo ziwaambie: “Mwenyezi Mungu aliyekitamkisha kila kitu ndiye aliyetutamkisha, naye ndiye aliyekuumbeni mara ya kwanza. Na kwake (hivi sasa) mnarudishwa. Na hamkuwa mkijificha hata masikio yenu na macho yenu na ngozi zenu (viungo vyao vyengine) zisiweze kutoa ushahidi juu yenu, bali mlidhani ya kwamba Mwenyezi Mungu hayajui mengi katika (hayo) mnayofanya. Basi hiyo ni dhana yenu mliyokuwa mkimdhania Mola wenu. imekuangamizeni; na mumekuwa miongoni mwa wenye kukhasirika. Basi wakistahamili, moto ndio maskani yao (ya wakitostahmili pia moto ndio maskani yao); Na kama wakitoa udhuru hawatakuwa miongoni mwa wanaokubaliwa nyudhuru zao.’ Haa mym (Sajidah: 19-24).

Makafiri watajuta mno kwa kumuasi Muumba wao aliyemuumba na kumjaalia maisha yakawezekana juu yao. Ndio maana katika siku ya kufufuliwa hawataruhusiwa kujitetea wenyewe. Hakuna fursa itakayotolewa kwao kunyanyua sauti zao. Wakiwa taabani na wenye majonzi, watataraji wapewe nafuu, lakini Mwenyezi Mungu anafafanua hali itakavyokuwa:

Ole wao siku hiyo hao wanaokadhibisha! Hii ni siku ambayo hawatasema (kitu). Wala hawatapewa ruhusa (kutoa udhuru) wakapata kutoa. Ole wao siku hiyo hao wanaokadhibisha! (Waambiwe) “Hii ni siku ya hukumu, tumekukusanyeni ninyi na wale waliotangulia. Hivyo kama kuna ubishi wowote, ufanyeni sasa hivi mbele yangu’ (Mursalat: 34 - 40).

Kwa hakika wale waliokufuru watanadiwa (wataambiwa) ‘Bila shaka kukuchukieni Mwenyezi Mungu ni kukubwa kuliko kujichukia ninyi nafsi zenu. (Kumbukeni) mlipokuwa mnaitwa katika Uislamu na ninyi mkakufuru: (Al-Muumin: 10).

KUKATA TAMAA KWA MAKAFIRI

Siku hiyo kafiri atataka kuridhia amri zote, bado, hataweza kufanya hivyo. Hii ni kwa sababu, hana tena uwezo wa kufanya au kukanusha chochote. Wakati atakapoitwa arukuu, atataka kufanya hivyo. Hata hivyo hatafanikiwa kuweza kufanya hivyo. Kama vile mtu aliyeota njozi mbaya, atataka aiondoshe lakini hawezi. Kamwe hawezi kusogeza mguu au mkono. Hofu, uoga na kukata tamaa vitamuacha kiasi cha kuonekana amepata ganzi.

(Na nawalete) hiyo siku kutakayokuwa na mateso makali, na wataitwa kusujudu lakini hawataweza. Macho yao yatainama chini, unyonge utawafunika. Na hakika walikuwa wakiitwa kusajudu walipokuwa salama (na walikataa). (Al-Qalam: 42-43).

Kumuita asiyeamini asujudu inatimiza lengo: Yaani kuzidisha majuto na majonzi anayohisi kutokana na kutokubaliana na wito huo alipokuwa duniani; na kumkumbusha kuwa kutotii huko, leo hakuwezi kufidiwa na hivyo kuwa chanzo cha majuto na kukosa matumaini milele. Inajulikana wazi kwa Mwenyezi Mungu kuwa kafiri hawezi kusujudu tena. Ni kwake tu, kama Mwenyezi Mungu alipenda, kuwa hawawezi kusujudu, kuabudu na kuwa watumwa wake. Hali kadhalika, waumini wametunukiwa imani. Hii ni kutokana na kupenda na kutaka kwake Mwenyezi Mungu. Qur’an pia inatuelezea juu ya namna waumini na makafiri watakavyoonekana siku hiyo. Furaha ya ndani kabisa watakayokuwa nayo waumini itaonekana katika nyuso zao zitakazong’ara kweli kweli. Makafiri kwa upande wao; watagundua juu ya kukosa kwao shukurani na kukosa kwao busara katika vitendo vyao. Wataanza kusubiri adhabu iliyoandaliwa kwa ajili yao. Kinyume na furaha inayoonekana katika nyuzo za waumini, makafiri nyuso zao zitakuwa nyeusi na zilizokunjamana”-

‘Sivyo! Bali ninyi mnapenda maisha ya hapa duniani. Na mnaacha (kuyashughulikia) maisha ya Akhera. Nyuso (nyingine siku hiyo zitang’ara (kweli kweli). Zinamtazama Mola wao (au neema alizowapa). Na nyuso nyingine siku hiyo zitakunjana zitajua kuwa zitafikiwa na msiba uvunjao uti wa mgongo. (Qiyamah: 20 - 25).

KUONA MOTO

Inaaminiwa na wengi kwamba ni makafiri tu ndio watakaoona moto. Hii, kwa hakika, ni sehemu tu ya ukweli. Mwenyezi Mungu anatufahamisha katika Surat Maryam kwamba watu wote, waumini na makafiri, watakusanywa kuuzunguuka moto wakiwa wamepiga magoti.

Na (baadhi ya) wanadamu husema, “Je! Nitakapokuwa nimekufa, kweli nitafufuliwa mara ya pili kuwa hai (mara ya pili)?” Je! Mwanadamu hakumbuki ya kwamba tulimuumba (kabla yake hii), hali hakuwa chochote?

Basi naapa kwa Mola wako kwa yakini tutawakusanya wao pamoja na mashetani, kisha tutawahudhurisha pembezoni mwa Jahannam, wapige magoti (hapo). Kisha kwa yakini tutawatoa, katika kila Taifa, wale miongoni mwao waliomuasi zaidi (Mwenyezi Mungu) mwingi wa Rehema. Tena hakika sisi tunawafahamu sina wanaostahiki (Wanaostahili) zaidi kuunguza humo. Wala hakuna katika ninyi ila ni mwenye kuifikia (hiyo jahannam). Na wajibu wa Mola wako uliokwishahukumiwa. Kisha tutawaokoa wale wamchao (Mwenyezi Mungu); Tutawacha madhalimu huko wamepiga magoti. (Maryam: 66 - 72).

Kama tunavyoona katika aya hizi hapo juu, katika siku ya kufufuliwa, watu watakusanywa kuuzunguka mtoto wa jahannam, wakiwa wamepiga magoti. Makafiri na Waumini wote watasikia Sauti ya kutisha na yenye kutokota ya moto wa Jahannam kwa pamoja huku wakishuhudia picha za kutisha. Hata hivyo waumini wataokolewa baada ya kipindi fulani na makafiri wataachwa hapo wakiwa wamepiga magoti. Kisha watatumbukizwa katika moto wa Jahannam.

Ili kuelewa vizuri ghadhabu za Mwenyezi Mungu na kuwa na shukurani kwake, inaweza kuchukuliwa kuwa ni moja ya sababu ya kuwepo Waumini katika kundi lililokusanywa karibu na moto. Muumini kwa kushuhudia namna moto unavyofanana, ataelewa ni kwa kiwango gani ametunukiwa neema ya imani na Mola wake. Kwa kuwa motoni ni sehemu inayotosha, hata kule kuokolewa kutokana na adhabu hiyo huwa na maana ya rehema kwa mwanadamu.

Kwa kushuhudia moto, Muumini ataweza kulinganisha na hivyo kuelewa vyema na kuridhia Pepo, mahali penye Rehema ambapo yatakuwa makazi yake milele. Hata katika maisha haya, jambo kubwa mwanadamu analolifurahia ni kuepushwa na maumivu. Kwa mfano, mtu anayekabiliwa na hatari ya kuganda katika mabarafu mlimani hupata faraja pale anapopata kijibanda kikuu kuu chenye sehemu ya kuwashia moto. Atakichukulia kibanda hiki kama chumba cha hoteli kilichosheheni vitu vya anasa. Kwa yule ambaye anajua hajakula chochote kwa siku kadhaa, kipande cha mkate kwake ni sikukuu. Mwisho wa maumivu ni furaha isiyo na kifani, amani na kushukuru kusiko na kifani pia. Muumini anayeona moto jirani yake na kuokolewa nao hufikia daraja la juu zaidi la furaha kuliko hili. Zaidi ya hilo, kule kuzawadiwa Pepo hufikia daraja la ushindi aliloainishiwa katika Qur’an. Kwa kuona hali ya kutosha ya adhabu ya motoni, muumini ataelewa vizuri thamani ya pepo ambayo imesheheni rehema. Kwa muda wote uliobakia milele, kama hatasahau kwamba Jahannam (motoni) kukoje na hivyo kuwa mwenye furaha zaidi huko peponi.

Katika siku ya hukumu, watu watasikia maneno yafuatayo kwa wale watakaowafahamu waumini na makafiri katika nyuso zao. Kutakuwa na ukuta unaotenganisha kati yao na katika muunuko kutakuwepo watu watakaowatambua kila mmoja, kwa anavyoonekana. Watawaita watu wa peponi ‘Amani iwe kwenu! Lakini bado hawajaingia humo japo wangependa kufanya hivyo. Watakapogeuza nyuso zao upande mwingine wa wale watu wa motoni; watasema: Ee Mola wetu, usitutumbukize na kutufanya pamoja na watu waovu hawa.’

Watu waliopo kilimani watawaita watu waliowatambua kwa alama zao watawaita watu wa peponi ‘Assalaam Alaykum’ Wao wenyewe bado hawajaingia humo wanatumai. Na macho yao yanapogeuzwa kwenye watu wa motoni, husema; ‘Mola wetu usituweke pamoja na watu madhalimu; Na hao watu wa sehemu iliyonyanyuka watawaita watu wanaowafahamu kwa Alama zao waseme ‘Haukukusaidieni wingi wenu wala mlivyokuwa mkijivunia. “Je hawa sio wale mliokuwa mkiwaapia kwamba Mwenyezi Mungu hatawafikishia Rehema? (Sasa wameambiwa) Ingieni peponi, hakuna khofu juu yenu, wala hamtahuzunika.” (Al-A’araf: 46:49).

Huu ni wakati ambapo waumini, viumbe bora kabisa ‘(Al-bayyinah: 7) na makafiri ‘Viumbe dhalili kabisa’ (Al-Bayyinah: 6) watakapotenganishwa. ‘Na mitume watakapokusanywa, Kwa siku gani hiyo wamewekwa muda huo? Siku ya hukumu. Na nini kitakachokujulisha siku ya hukumu? Ole wao siku hiyo hawa waaokadhibisha! Je, hatukuwaangamiza (watu) wa zamani (kabisa)? Kisha tukawaandamizia (watu) wengine. Basi hivi ndivyo tutakavyowafanya wakosa (wengine). Ole wao siku hiyo anaokadhibisha! (Al-Mursalat: 11-19).

Siku ya hukumu, huanza kwa kifo, kisha kuendelea kwa kufufuliwa na kuhesabiwa na kumalizika kwa watu kupelekwa kwenye makazi yao ya kudumu. Katika Surat Qaf, safari ya waumini na makafiri kuelekea kwenye makazi yao ya kudumu imefafanuliwa katika aya zifuatazo:-

‘Na kutoka roho kutakapomjia kwa haki, (Hapo ataambiwa), hayo ndiyo uliyokuwa ukiyakimbia.” Na itapulizwa parapanda; hiyo ndio siku ya makamio, Na itakuja kila nafsi pamoja na mchungaji (wake) na shahidi (wake). (Aambiwe) ‘Kwa hakika ulikuwa umo katika ghafla na jambo hili. Basi tumekuondolea (leo pazia), kuona kwako leo kumekuwa kukali. Na yule aliyekuwa pamoja naye atasema ‘Hayo ndiyo yaliyowekwa tayari kwangu (yameandikwa na malaika). (Wakati huo kutasemwa), Mtupeni katika Jahannam kila kafiri aasi Atakatazae kheri, arukaye mipaka, aliyekuwa akijipa shaka. Aliyeweka miungu mingine pamoja na Mwenyezi Mungu, basi mtupeni katika adhabu kali.” ‘Mwenzake asema “Ee Mola wetu! Sikumpoteza mimi bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotofu wa mbali kabisa: Aseme (Mwenyezi Mungu). ‘Msigombane mbele yangu. Nilikwisha kukutangulizieni onyo (langu). Kauli yangu haibadilishwi kwangu, wala mimi siwadhulumu waja wangu. Siku tutakapoiambia Jahannam. “Je! Umejaa?” Nayo itasema, “Je! Kuna zaidi?” Na pepo italetwa karibu, kwa wamchao Mwenyezi Mungu haitakuwa mbali (nao). Haya ndiyo mnayoahidiwa kwa kila aelekeaye (kwa Mwenyezi Mungu), ajilindae (na maasia). Na anayemuogopa (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa kurehemu, hali ya kuwa hamuoni, na akaja kwa moyo ulioelekea (kwa Mwenyezi Mungu). (Waambiwe) ‘Ingieni (Peponi) kwa salama.” Hiyo ni siku ya kukaa daima (katika starehe za huko peponi). (Qat: 19-34).


    
6 / total 8
You can read Harun Yahya's book Kufa Ufufuko Jahannam online, share it on social networks such as Facebook and Twitter, download it to your computer, use it in your homework and theses, and publish, copy or reproduce it on your own web sites or blogs without paying any copyright fee, so long as you acknowledge this site as the reference.
About this site | Tengeneza kurasa yako ya nyumbani | Add to favorites | RSS Feed
Mambo yote yanaweza kuynakiliwa, kuchapwa na kusambazwa kwa kurejea katika kurasa hii
(c) All publication rights of the personal photos of Mr. Adnan Oktar that are present in our website and in all other Harun Yahya works belong to Global Publication Ltd. Co. They cannot be used or published without prior consent even if used partially.
© 1994 Harun Yahya.www.harunyahya.com
page_top